Videos

Bandari Dar kuboreshwa kwa bilioni 145/-


Mwandishi Wetu

BANDARI ya Dar es Salaam inatarajia kutumia dola milioni 690 sawa na Sh bilioni 145 kwa ajili ya kufanyiwa maboresho, imeelezwa.

Akizungumza na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko alisema sehemu ya fedha hizo itatokana na mkopo nafuu.

Alisema maboresho hayo yanatokana na uchakavu wa miundombinu ya bandari hiyo, pamoja na kina kifupi cha maji ambacho ni meta tisa na ufinyu wa lango la kuingilia meli lenye upana wa meta 140.

“Lango hili linaruhusu meli za urefu wa usiozidi meta 243 tu meli kubwa kuzidi hapo haziwezi kuingia, hivi sasa meli zinazotengenezwa duniani huko ni kubwa tu na ndizo zinazotakiwa kutia nanga hapa hivyo kwa lango hili hazitaingia,” alisema.

Akifafanua kuhusu mkopo huo, Kakoko ambaye ni Mhandisi alisema Benki ya Dunia kupitia mfuko wa Benki ya Kimataifa ya Ujenzi na Maendeleo (IBRD) itatoa dola milioni 600.

Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID) litatoa ruzuku ya dola milioni 30 huku TPA yenyewe ikichangia dola milioni 60.

Miradi itakayohusika na mkopo huo, Kakoko aliitaja kuwa ni uboreshaji na uongezaji kina kufikia meta 14 kuanzia gati namba moja hadi saba na nane hadi 11 sambamba na kujenga gati mpya namba 13 na 14.

Mingine ni ya ujenzi wa gati mpya ya kushushia magari eneo la Gerezani Creek, uchimbaji wa kuongeza kina cha lango la kuingilia meli hadi meta 14 na sehemu ya kugeuzia meli na kupanua lango.

Kakoko alisema pia wanatarajia kufunga mfumo wa kushusha mizigo kwa mkanda na kujenga maghala ya kuhifadhia nafaka na kuhamisha gati na mabomba ya mafuta ya KOJ.

Mtandao wa reli ndani ya bandari hiyo utajengwa na mwingine kuboreshwa ikiwa ni pamoja na kujenga sehemu ya kupakilia na kushushia mizigo kwenye mabehewa.

Hali kadhalika aliwambia wahariri hao kuwa jengo la ghorofa lililoko barabara ya Sokoine ambako kutakuwa na kituo kimoja cha huduma kwa wateja, litakamilishwa hivi karibuni na kuanza kazi.

“Pia tutaboresha na kupanua barabara ya Bandari na Mivinjeni ili kupunguza msongamano wa magari ya mizigo yanayoingia na kutoka bandarini,” alisema huku akizungumzia pia uimarishaji wa usalama na kuongeza mitambo ya kukagulia mizigo bandarini hapo.

Lakini pia alisema ili kupunguza usumbufu kwa wateja mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) utaboreshwa  ili kurahisisha upakiaji na upakuaji mizigo na malipo ya huduma za bandari kwa elektroniki.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment