Videos

CCM yakataa ‘Ukawa’ wa Mrema



Suleiman Msuya na Celina Mathew

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeelezea utayari wake kushirikiana na vyama vyote, ikiwamo chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kujenga nchi, lakini hakifikirii kuanzisha makundi yasiyo rasmi na vyama vingine nchini.

Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu kauli ya Mwenyekiti  wa TLP, Augustine Mrema kuwa chama chake na vingine vya upinzani viko tayari kuanzisha umoja na CCM.

Mrema akihojiwa kwenye kituo cha radio cha TBC Fm kwenye kipindi cha Busati, alisema vyama vinavyopenda maendeleo na amani nchini, viko tayari kuanzisha ‘Ukawa’ yao na CCM

Akizungumzia kauli hiyo, Sendeka alisema CCM ni chama kilichosajiliwa na kilicho tayari kufanya kazi na chama kingine cha siasa chenye usajili wa kudumu na usio wa kudumu.

Aliongeza kuwa kiko tayari kutoa mafunzo ya kuimarisha uzalendo wa kujenga nchi na kwamba kama vyama vingine vitahitaji ushauri vinakaribishwa, maana lengo ni kushirikiana na vyama vyote.

Hata hivyo, wanachama wa TLP walimpinga Mrema kwa kauli yake ya  kuungana na CCM.

Aidha, walimtaka achague TLP au Parole kwa kinachodaiwa kuwa ameanza kulewa madaraka.

Wakizungumza na JAMBO LEO baadhi ya wanachama hao walisema kiongozi huyo anafanya mambo kinyume na Katiba na taratibu za chama hivyo hawako tayari kushirikiana na CCM.

Mwanachama James Haule aliweka bayana kuwa anachofanya Mrema sasa ni kinyume na chama hicho, kwani hajawashirikisha katika mapendekezo yake ya kujiunga na CCM.

Haule alisema Mrema amelewa madaraka ya Parole hata achanganyikiwe, hivyo anashindwa kuongoza chama na kufanya kazi za Parole na kujikuta akitoa matamko yasiyo shirikishi.

Aidha, alisema Mrema anapaswa kutoa tafsiri sahihi ya yeye kutaka kuungana na CCM, kwani anaonekana kuacha maswali mengi juu ya muungano anaotaka.

Mwanachama huyo alisema umuhimu wa Mrema ndani ya TLP ni mkubwa hivyo kutokana na kupewa madaraka mengine, ameonekana kuanza kukiacha chama hivyo sasa ni wakati mwafaka kupisha watu wengine waongoze.

"Napenda kumwambia Mwenyekiti aamue jambo moja, kufanya siasa akiwa TLP au Parole, kwani naona ameanza kulewa madaraka ndiyo maana leo unamwona yuko kwa watumia dawa za kulevya, kesho waendesha pikipiki," alisema.

Dickson Rutabanzibwa wa Bukoba, Kagera, alisema hawako tayari kuungana na CCM kwa alichodai ni lengo la chama cha Upinzani kukiondoa chama tawala madarakani.

“Atupishe, kwanza anavunja Katiba ya chama, sisi hatuko tayari kuungana na CCM, lengo letu ni kukamata Dola, kama yeye amechoka siasa ahamie huko atuachie chama chetu,” alisema.

Akizungumzia malalamiko hayo, Mrema alisema hawezi kuacha nafasi ya uenyekiti kwa sababu ya kuwa kwenye Bodi ya Parole, kwa kuwa hakuna anachokosea na wanaosema hayo ni wabaya wake kisiasa.

Mrema alisema ataondoka kwenye uenyekiti wa TLP kwa kufuata taratibu zinazopaswa kufuatwa kichama na si kwa kauli za wanaojiita wanachama.

Kuhusu kuungana alisema hakumaanisha kuungana na kuwa chama kimoja ila ni kutekeleza majukumu, kwani anaona CCM ya sasa inafanya mambo ambayo yeye na chama chake wanafanya.

"CCM ya sasa inapingana na ufisadi, rushwa na kuhitaji uwajibikaji kazini hayo ndiyo malengo yetu ya kila siku, ndiyo maana nikasema tuungane kufanya kazi na si kuunganisha vyama.

“Ila mbona Rais John Magufuli ni Mwenyekiti na Rais, kipi kimeharibika nadhani tunapaswa kuheshimu nafasi hii tuliyopewa," alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment