Sharifa Marira
MAANDAMANO ya Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) yaliyokuwa yamepongwa kufanyika leo yalizua hofu na taharuki miongoni mwa wananchi huku wengi wakieleza yangetokea wasingefanya shughuli zao.
Maandamano hayo yaliyoasisiwa na Chadema, hata hivyo yalitangazwa kusitishwa kwa muda wa mwezi mmoja hadi Oktoba mosi, ambapo mwenyekiti wake Freeman Mbowe alisema wamefanya hivyo ili kuwapa nafasi viongozi wa dini kutafuta suluhu na serikali ya Rais John Magufuli.
JAMBO LEO lilifanya mahojiano na baadhi ya wananchi kutokana na mategemeo yao juu ya siku hiyo ambapo walikuwa na maoni tofauti huku wengine wakidai kwamba wangejifungia ndani.
Semambe Mshana, mkazi wa Mbuyuni jijini Dar es Salam alisema endapo (Ukuta) ungetokea asingetoka katika shughuli zake za kila siku kwani alishuhudia Askari wakifanya mazoezi ya wazi maeneo mengi hivyo alijua kutatokea vurugu.
“Kesho (leo) nisingetoka kwenye pilika pilika zangu, sababu nilitegemea itakuwa siku ya fujo, na ghasia tuu, hivyo basi ningebaki nyumbani tuu ila nilikuwa naomba muwafaka upatikane kati ya serikali na vyama vya upinzani ili kuwe na utulivu na watu tuendelee na kupambana na maisha”alisema Mshana
Alieleza kuwa alijawa na hofu kutokana na kuona nguvu za viongozi wa dini na wanasiasa wakijitahidi kutafuta suluhu lakini Chadema wakiendelea na msimamo wao wa kudai maandamano yapo pale pale hivyo alikuwa anamuomba mungu pekee kuepusha.
Zainab Issa ambaye ni Mwalimu Mkazi wa Makongo Juu alisema hakuwa anategemea kufanya chochote zaidi ya kukaa nyumbani kusikiliza yatakayojiri.
“Nilijua kabisa polisi watakuwepo barabarani na leo (jana) niliona ndege za wanajeshi zikipita mapema asubuhi nikaambiwa ni za kivita hivyo niliona ni vyema kutulia nyumbani kuliko kwenda barabarai kuumizwa wakati siwezi kufaidika na chochote kutokana na maandamano hayo”alisema
Judith Mvella wa Mwanza alisema alitegemea kutembelea familia za watu walioumia kwani alishajua polisi wamekasirika kwa kuwa walishakemea maandamano hivyo ambaye angefanya hivyo angekuwa ametafuta kupigwa.
“Naishi na dada angu hapa Mwanza lakini tulishaamua kama familia hakuna watoto kwenda shule,biashara yetu ya duka la nguo tusingefungua kwasababu hatukujua maandamano yangeanzia wapi,tulikuwa tunaogopa kupata hasara ya kujitakia”alisema Mvella
Zuhura Masoud wa Tabata Dar es Salaam alisema alitegemea kuendelea na shughuli zake na endapo atakutana na maandamano njiani angeweza kuunga mkono jitihada hizo za kutetea demokrasia.
“Nilijua Ukuta utafanyika ili wanademokrasia wenzangu wafikishe ujumbe kwa serikali kama tunataka nchi iwe yenye uhuru na demokrasia na mfumo wa vyama vingi uheshimiwe”alisema Masous na kuongeza kuwa
“Chadema wamefanya jambo jema kuwasikiliza viongozi wa dini lakini wasiishie hapo wanapaswa kupaza sauti zao bila kuchoka kutokana na kuwa wanachokipigania wananchi tunakihitaji,natamani itokee tena siku ya Ukuta’’
David Kahumbi ,kutoka Shinyanga alisema alijua kama maandamano hayo hayawezi kufanyika kutokana na watanzania wengi kuwa waoga wa kudai demokrasia lakini pia vitisho vya polisi vilichangia kuwarudisha watu nyuma.
“Huku migodini tungeendelea na shughuli zetu kama kawaida,nawajua watanzania walivyo vitisho vya polisi ilikuwa ni njia moja wapo ya kuwafanya warudi nyumba,ila Chadema waendelee kudai demokrasia kwa njia nyingine”alisema Kahumbi
Jackline Yeuda mkazi wa Mbezi Tangi Mbovu alisema anaishi na wadogo zake wawili ambao alishawaagia katika shule wanazosoma kwamba kwa siku ya Ukuta wasingeweza kwenda shule kutokana na kwamba wakati wa kupigwa mabomu hayachagui aliyeandamana na ambaye hajafanya hivyo.
Alisema kwa kuwa ni kijana anayependa demokrasia alihamasisha vijana maeneo mbalimbali kuandamana bila kujali ni kiasi gani wameumizwa na polisi lakini ujumbe ungefika.
Rashidi Mahanyu wa Mlalo Tanga alisema wananchi wa maeneo hayo hawakuwa wanafuatlia jambo lolote kuhusu Ukuta hivyo hata ungefanyika kusingekuwa na madhara yoyote.
Boniface Mteketa,wa Gongo la Mboto alisema Ukuta ungemfanya ashindwe kula kwani anamiliki kibanda cha kuuza vifaa vya simu ambacho kipo barabarani hivyo endapo kurupushani zingetokea alijua atakuwa muathirika wa kwanza hivyo aliamua kutokufanya kazi.
Salma Mahamdu,alisema”Katika vitu ambavyo nilikuwa sivipendi ni huo Ukuta,sikuwa najua maana yake na haikuwa unatusaidia chochote,nimeshukuru kusikia hayafanyiki kwa kuwa yangeumiza watu wasiokuwa na hatia,wamuache rais afanye kazi ya kutuletea maendeleo”
Abdallah Hamisi, wa Mabibo Dar es Salaam alisema Kusitisha maandamano ni jambo zuri kwani serikali ilikuwa inatumia nguvu kubwa na haikuwa na dhamira ya nzuri kwa wananchi hivyo yanghetokwea machafuko makubwa ambayo ni bora Chadema walivyoyaepusha.
“Kwa namna nyingine naona jinsi serikali inavyotumia majeshi yake kukandamiza demokrasia hivyo naona kama ni kifo cha demokrasia kwani watakuwa hawako huru” alisema Hamisi.
0 comments:
Post a Comment