NA EMERCIANA ATHANA
HOJA ya kutaka aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF) Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu arudi kwenye nafasi yake, jana ilisababisha mpasuko kwa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho ambapo ulivunjika bila kupata uongozi mpya.
Chama hicho kilikutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili na kupitisha majina ya wagombea uenyekiti na makamu mwenyekiti wake kufuatia kujiuzulu kwa Lipimba wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na makamu wake Juma Haji Duni aliyekwenda kuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa wa Chadema katika nafasi ya urais.
Awali, chama hicho kilitangaza majina ya waliopitishwa kugombea uenyekiti na umakamu huku Duni akitangaza kujitoa kwa kilichoelezwa kukosa sifa kuwania nafasi hiyo kikatiba.
Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango wa CUF, Shaweji Mketo, alisema Duni alijiondoa kutokana na baadhi ya maadui wa Ukawa kutaka kukihujumu chama hicho.
"Katiba ya chama inasema kama kiongozi alijiuzulu na kuhamia chama kingine, basi itamlazimu kukaa ndani ya miaka miwili kisha kuwania tena nafasi hiyo,” alisema.
Alitaja majina ya wagombea hao akisema uteuzi wao ulifanyika juzi katika mkutano mkuu wa dharura wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mketo, aliwataja wanachama watakaowania nafasi ya Mwenyekiti kuwa ni Riziki Mngwali, Twaha Taslima na Juma Nkumbi.
Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti, waliopitishwa kuwania ni Mussa Hajji Kombo na Salim Abdalla Bimani. Majina yao yalifikishwa kwenye Kamati Kuu ya CUF kwa ajili ya kupigiwa kura.
Mketo alisema majina 34 ya wanachama waliojitokeza kuwania nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa yalipitishwa yote kwenda Kamati Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura ili kupata wajumbe watakaoziba nafasi zilizoachwa wazi.
Pia, Mketo alisema mkutano huo wenye wajumbe 832 ulipokea rasmi taarifa ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa baada ya kujadili hoja ya Lipumba kuliibuka mvutano kati ya wajumbe 832 waliohudhuria mkutano huo na kusababisha mkutano kusimama kwa muda.
Habari zinasema baada ya kurejea, walishindwa kupata mwafaka hali iliyosababisha waamue kupiga kura.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa viongozi waliopo walitumia ubabe kulazimisha kupigwa kura ya wazi, jambo ambalo linaloelezwa ni kinyume cha Katiba ya CUF na misingi ya demokrasia.
“Haki haikutendeka, ni ubabe wala mkutano haukuzingatia kutimia kwa akidi. Tulilazimishwa kupiga kura kwa kunyoosha mikono wakati kwa mazingira yaliyopo na usahihi kura ni siri,” alisema mmoja wa wakjumbe wa mkutano huo aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa sababu si msemaji wa chama.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa katika kura hizo Lipumba alipata kura 14 zilizotaka arejee kwenye nafasi yake, huku wajumbe 476 wakimkataa kati ya wajumbe 832, jambo lilizozua tafrani na mkutano kuvunjika.
Awali, nje ya ukumbi wafuasi wa chama hicho walitanda huku wengine wakiwa wamevalia fulana zenye picha ya Lipumba ambaye baada ya kuwasili walimshangilia na kuisikika wakisema; ‘Lipumba kwanza mengine baadaye.’
Wafuasi hao kwa nyakati tofauti walisikika pia wakisema hawawezi kukubali kumwacha Lipumba kuondoka na kukiacha chama hicho kife.
Habari za ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa muda mfupi baada ya kuanza kujadili barua ya Lipumba, baadhi ya wafuasi walitaka mkutano usitishwe na kumsubiri hadi atakapofika huku wanachama wengine wakipinga ujio wa Lipumba.
Kwa mujibu wa taarifa hizo baada ya Lipumba kuwasili alikwenda mbele kwa ajili ya kusalimiana na viongozi waliokuwa Meza Kuu, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambao walikataa salamu yake kwa kutompa mkono, badala yake aliamriwa kukaa kwa ajili ya kuendelea kuijadili barua yake ya kujiuzulu.
0 comments:
Post a Comment