Videos

Msekwa ataka polisi wakamate CCM



Waandishi Wetu

SPIKA mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa amesema kazi ya Jeshi la Polisi ni kutekeleza maagizo ya Rais na si kubeba chama tawala.

Aidha, Msekwa alitaja adui wa Chama Cha Mapinduzi, akisema adui huyo yupo karibu lakini anaweza kuwa mbali na atatokea na kukidhuru iwapo kitafanya makosa.

Msekwa alitoa kauli hiyo hivi karibuni kwenye mahojiano maalumu aliyofanya na gazeti hili nyumbani kwake Dar es Salaam.

Alikuwa akijibu swali lililomtaka aeleze mtazamo wa baadhi ya watu kwamba kwa kubaki madarakani muda mrefu, CCM imefanya taasisi zote za Serikali ikiwamo Polisi na wanachama wake.

Kwa nyakati tofauti wapinzani wamekuwa wakilalamika kuwa Polisi haiwatendei haki. Imekuwa ikizuia mikutano yao na kuwadhibiti wanapotaka kufanya maandamano lakini CCM iko huru kufanya siasa.

Majibu 

“Polisi hawatakiwi kupendelea chama cha siasa, wanachotakiwa ni kutekeleza maagizo ya Rais na kutenda haki kwa vyama vyote. Kama Rais amezuia mikutano ya hadhara, agizo hilo libane pia CCM,” alisema Msekwa na kuongeza:

“Labda nichukue fursa hii kueleza kuwa kama polisi wanadhani wanatakiwa kupendelea CCM wamekosea na kama kuna watu wanaamini kuwa polisi ni tawi la CCM ni fikra potofu, kwani hata Lowassa (Edward) angeshinda Uchaguzi Mkuu mwaka jana, polisi haohao wangetekeleza maagizo yake.”

Adui wa CCM

Kuhusu adui wa chama hicho tawala, Msekwa alimtaja kuwa ni CCM yenyewe iwapo itafanya makosa katika kuteua wagombea uongozi.

Alikuwa akijibu swali lililotaka kujua kwa mtazamo wake kwa sasa ni nani adui wa CCM.

Kauli hiyo ya Msekwa inafananishwa na iliyopata kutolewa na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere kwamba: “Mpinzani wa kweli wa CCM, atatoka CCM.”

Nyerere alitoa kauli hiyo kukihadharisha chama hicho, kwamba iwapo kitafanya makosa na baadhi ya watu wenye nguvu wakatoka na kugeuka wapinzani, wataipa wakati mgumu CCM.

Naye Msekwa alisema: “Adui wa CCM ni CCM yenyewe kama itafanya makosa ya kuleta mgombea asiyetakiwa. Kama ingefanya makosa ya kumpitisha… tungefanya makosa ya kumleta …tusingepita.

“Walikuwa wanatwambia, ‘mkimpitisha (anamtaja), mtakwenda na maji’.  Watu wanachukia mtu. Adui mkubwa wa CCM ni madhara ya kujitakia wenyewe. Unaleta mgombea ambaye hatakiwi, lazima utaanguka tu.”

Alitaja mifano mingi ya watu kutokubalika akisema katika mambo ya siasa kikubwa si chama au chombo anachoongoza, bali kiongozi anavyokubalika.

“Kuna mifano mingi, baadhi ya majimbo katika uchaguzi watu walisema akigombea huyu, hata akiwekwa na jiwe tutachagua jiwe,” alisema.

Alipotakiwa kueleza kama adui huyo wa CCM yupo karibu au mbali, Msekwa ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wazee ndani ya chama hicho alisema: “Hiyo ni ramli sasa, hatuwezi kujua inategemea mazingira.”

Baraza la Wazee ndani ya CCM linatajwa kuhusika kuchuja na kukata majina ya wana CCM waliotaka kuteuliwa kuwania urais, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa na Benard Membe aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, walioonekana kuzua mvutano ndani ya chama hicho, kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi.

Katika mchujo wa Baraza hilo, jina la Lowasa lilikatwa bila kufika mchujo wa tano bora, huku Membe akikatwa baada ya kufika hatua ya tano bora, ndipo Dk John Magufuli akapenya na kuongoza hata kupata nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM kuwania urais na kushinda.

Akifafanua kuhusu alipo adui wa CCM, Msekwa alisema: “Anaweza kuwa yupo karibu kwa maana ya miaka mitano ijayo utakapofanyika uchaguzi, lakini kwa kuwa tunaye Rais Magufuli, hatutafanya makosa kutomweka Magufuli, tunajua atamaliza miaka 10 hadi 2025, hivyo adui yuko mbali kwa maana hiyo.”

Msekwa alisisitiza kuwa adui mkubwa wa CCM ni CCM yenyewe, hasa pale itakapokuwa ikienda kinyume na matakwa ya Katiba yake kwa ajili ya maslahi ya watu wachache wenye utashi na dhamira ya kujilimbikizia madaraka.

Alisema CCM ina misingi yake ambayo imewekwa na Katiba ya chama hicho, hivyo haina budi kufuatwa hata kama inahatarisha maslahi ya chama, kwani kwenda kinyume na Katiba ni dhambi ya kukiua chama.

“Usisubiri adui wa CCM atoke nje ya chama au kiwe chama kingine, haiwezekani na kamwe haitawezekana. Adui wa CCM ni CCM yenyewe, kwa maana kuwa pale viongozi wanapoanza au kuamua kupitisha jambo au mambo fulani ili kulinda maslahi yao.

“Mara watakapoanza kufanya hivyo na kwenda kinyume na Katiba, basi chama kitakuwa na muda mfupi wa kuishi. Fanya makosa mengine yote lakini si ya kwenda kinyume na Katiba, kwani lazima chama kisambaratike na kupoteza mwelekeo moja kwa moja,” alisema Msekwa.

Bunge

Katika hatua nyingine, Msekwa alijibu maswali kadhaa kuhusu uendeshaji wa Bunge, akisema anavyoona hakuna jipya kwa kuwa hata vurugu za Upinzani zilipata kutokea enzi zake akiwa Katibu wa Bunge.

“Kama ni vurugu hata enzi zile zilikuwapo, lakini tulifanikiwa kuzidhibiti na hali ilikuwa shwari,” alisema Msekwa akitaja wanasiasa machachari wa wakati huo kuwa ni pamoja na Dk Masumbuko Lamwai, Steven Wasira, Mabere Marando na Paul Ndobho.

Hata hivyo, Msekwa alieleza tofauti za wanasiasa hao na wabunge wa sasa wa upinzani kuwa ni uvumilivu akisema:

“Hawa (Marando, Lamwai, Wasira na Ndobho) walikuwa machachari kuliko wabunge wengi wa sasa, lakini mambo yetu tuliyamaliza bungeni. Siku hizi nashangaa kuona mwakilishi wa wananchi anasusa Bunge!

“Bunge unamsusia nani? Wewe umetumwa kuwakilisha wananchi halafu unatoka bungeni, unasusa! Hiyo ndiyo tofauti kubwa ninayoiona, ni ajabu kweli.”

Msekwa alipuuza madai kuwa wabunge wa sasa wanasusa Bunge wanapoona mambo hayaendi sawa, kwa sababu ni damu changa zinazohitaji mabadiliko ya haraka, akisema: “Kila wakati kuna vijana wake, hata mimi niliwahi kuwa kijana. Bunge nililoongoza nalo lilikuwa na vijana kwa wakati ule, lakini hawakufanya haya.”

Msekwa hakuweka wazi kuwa tatizo la wabunge wa sasa ni elimu. Lakini akasema “Elimu hutafutwa, na Biblia inasema usimwache elimu akaenda zake. Kwa nini wasitafute elimu?”

Alisema ni wajibu wao kutafuta elimu ili iwasaidie katika kuwakilisha wapiga kura wao bungeni badala ya kudhani wanajua kumbe wanaboronga.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment