Videos

Pius Msekwa aibua siri ya kuhamia Dodoma


Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa
Na Kizitto Noya

MAKAMU mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amesema Serikali haikukurupuka kufikiri kuhamia Dodoma, bali inatekeleza mchakato huo ambao ulianzia bungeni mwaka 1966 kwa hoja binafsi ya mbunge Joseph Nyerere.

Msekwa alisema hayo alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

“Kuna watu hawajaelewa historia ya Serikali kuhamia Dodoma. Huu ni mchakato ulioanzia bungeni wakati mimi nikiwa Katibu wa Bunge.

Mbunge Joseph Nyerere alisimama bungeni na kutoa hoja binafsi kutaka Serikali ihamie Dodoma,” alisema Msekwa. Aliendelea “Msingi wa hoja yake ni kwamba kama Serikali itafanyia shughuli zake Dodoma itakuwa rahisi kuiangalia nchi kwa kuwa mkoa huo upo katikati. Ni rahisi wakandarasi wakatokea Dodoma kwenda mwanza kuliko kutoka Dar es Salaam.”

Hata hivyo, Msekwa alisema kwa taratibu za wakati huo, hoja ikitolewa bungeni, Serikali inapewa muda wa kuijadilia na kuiridhia. “Katika kuijibu hoja hiyo, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Paul Bomani aliliambia Bunge kuwa pamoja na kwamba hoja ina tija, Serikali kwa wakati ule haina pesa kwa sababu hesabu zilionyesha kuwa zilihitajika Sh3 Bilioni kutekeleza mradi huo,” alisema.

“Majibu hayo yalimfanya mbunge huyo aiondoe hoja yake, lakini alikuwa mjanja sana alitaka hoja isitishwe mpaka wakati ambao serikali ingepata pesa. Angelazimisha wapige kura wakati ule hoja hiyo ingetupwa,” alisema.

Msekwa alisema hoja hiyo ilifufuliwa tena mwaka 1972 katika mkutano wa Kamati ya Siasa ya Chama cha TANU mkoa wa Mwanza. “Kama hiyo ilijadili hoja hiyo na kutoa mapendekezo yake kwenye chama ngazi ya taifa. Kwenye ngazi hiyo ya taifa uamuzi ulifanyika mwaka 1973.

Ilikubaliwa iitishwe kura ya maoni ya wanachama wote na kura hizo zilipigwa kwenye matawi yote ya TANU wakati huo.

Kwa mujibu wa Msekwa matawi yaliyopiga kura hiyo yalikuwa 1,800 na kati yake matawi 800 yalikataa hoja hiyo na matawi mengine yaliyobaki 1,000 yakaridhia.

“Kwa wakati ule wa chama kimoja, kama wazo litaamuliwa kwenye chama Serikali lazima litekeleze. Hivyo Serikali sasa ikachukua wazo la kuhamia Dodoma na ikajipa miaka 10 kuanzia 1973 hadi 1983. Kwa kuanzia, Rais Nyerere akaunda Wizara ya Ustawishaji Makao Makuu na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA). Hilo lilifanyika mwezi Oktoba,” alisema.

Kwa nini haikufanikiwa?

Msekwa alisema kwa bahati mbaya wazo hilo lilikwama kutekelezeka katika kipindi cha miaka mitano tu kutokana na changamoto za wakati huo. “Kulikuwa na mambo matatu yaliyokwamisha utekelezaji wa mradi huo wa kuhamia Dodoma; Vita ya Kagera, Kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kupanda kwa bei ya mafuta duniani,” alisema.
Vita ya Kagera

Msekwa alisema vita ya Kagera iliifanya serikali ishindwa kupata Sh3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuhamia Dodoma kwakuwa rasilimali nyingi za taifa zilielekezwa kwenye mapambano dhidi ya nduli, Idd Amin.

Alisema hata baada ya kumalizika kwa vita ya Kagera, athari zake ziliendelea kulitafuna taifa kwa muda mrefu kiasi ambacho bado ilikuwa vigumu kupata fedha hiyo inayohitajika.
Kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki Msekwa alitaja sababu nyingine iliyofanya Serikali ichelewe kuhamia Dodoma kuwa ni kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisemabaada ya tukio hilo, serikali ililazimika kutumia rasilimali zake nyingi kujiendesha tofauti na ilivyokuwa wakati wa uhaiwa jumuiya hiyo.

“Tulipokuwa katika ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mambo mengi tuliyafanya kwa umoja sasa ilipovunjika ilibidi taifa lianze kujitegemea. Hilo nalo lilikuwa kikwazo cha utekelezaji wa mradi huo,” alisema.

Kupanda kwa bei ya mafuta duniani “Katika kipindi cha miaka ya 70 bei ya mafuta duniani ilipanda sana na kama nchi ili kukabiliana na tatizo hilo, ilibidi tutumie fedha nyingi za kigeni kununulia mafuta.

Hapa napo ndipo tulipoanza kuyumba na kupoteza ndoto ya kuhamia Dodoma,” alisema na kuendelea; “Kama inakumbukwa hiki ndicho kipindi ambacho Mwalimu Nyerere alitangaza kuwa nchi iko katika hali ya kufunga mkanda kwa miezi 18, lakini muda huo uliongezeka sana, tulipita muda mrefu tukiwa katika hali ya kuyumba kiuchumi kama taifa.”

Nani alaumiwe?

“Haikuwa uzembe wa mtu, ni suala la mazingira tu, ila kuna kosa moja ambalo lilifanyika. Ni kufikiria kwamba mradi wa kuhamia Dodoma lazima utekelezwe na Serikali tu,” alisema.

“Viongozi walifikiri kwamba lazima Serikali iwajengee kwanza nyumba wafanyakazi wake wote ndipo wahamie Dodoma na ikaona suala hilo ni jukumu lake peke yake.

Lakini kwa nini iwe hivyo?

Kwani wafanyakazi wote wa Serikali wanaoishi Dar es Salaam wanaishi kwenye nyumba za Serikali?”


Rais Magufuli anawezaje?

“Rais Magufuli ana kitu kimoja cha pekee katika suala hilo; dhamiri ya kweli. Hilo ni muhimu sana kwani kama nilivyosema, mradi wa kuhamia Dodoma ni wa nchi na siyo Serikali kwa maana hiyo kila mdau ana wajibu wa kufanya jambo katika kuutekeleza,” alisema na kuendelea; “Ndiyo maana Rais alipoonyesha utashi, sekta binafsi zikatangaza kumuunga mkono na hapa ndipo kwenye siri ya mafanikio yake katika kutekeleza mradi huo.”

Alifafanua kuwa ili kiongozi afanikiwe anahitaji mambo matatu; kupuuza ramli, kufanya maamuzi bila kujali ramli na kukubali kujirekebisha akiona amekosea. “Ramli ni mawazo ya matokeo ya jambo kabla jambo lenyewe halijafanywa, sasa kwa nini tuogope matokeo ya jambo ambalo hatujafanya?

Alihoji na kuendelea “ili afanikiwe kiongozi anatakiwa kufanya maamuzi bila kujali hizo ramli lakini akiona amekosea, awe tayari kujirekebisha na Mwalimu Nyerere amejirekebisha mara nyingi,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment