MAJAMBAZI watatu wameuawa na wenzao katika majibizano ya risasi na Polisi wakati walipokwenda eneo la mapori ya Vikindu, Mkuranga kuonesha yalipo maficho ya wenzao.
Kwa mujibu wa Polisi, majambazi hao walikuwa wakiwaongoza kuelekea walikojificha wenzao wanaodaiwa kuhusika na tukio la wizi kwenye tawi la CRDB Mbande, wilayani Temeke na mapigano na polisi hivi karibuni Vikindu.
Mmoja wa majambazi hao akiwa ni raia wa Kenya, wamehusika na tukio lililotokea hivi karibuni na askari wanne kuuawa na wanaodaiwa kuwa ni majambazi kupora silaha na kukimbilia msitu wa Vikindu, Mkuranga.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema Jeshi lake limekamata majambazi zaidi ya saba mmoja akiwa raia wa Kenya, kati ya zaidi ya 14 waliohusika na tukio la Vikindu na kumwua Ofisa wa Polisi Mwandamizi.
Alisema Jeshi hilo limekamata mtandao wa majambazi watatu ambao walipatikana wakiwa na silaha 23 na risasi 835.
“Majambazi hao walikuwa na fulana tatu 3 zisizopenya risasi, sare za Polisi, pingu 48 na radio za upepo tunazotumia zipatazo 12,” alisema.
Alisema Septemba 3 Jeshi hilo likiwa kwenye operesheni ya ufuatiliaji wa tukio la Septemba 29 Veta, Chang’ombe Dar es Salaam majambazi wapatao 10 waliingia katika ofisi hizo huku baadhi wakiwa wamevalia sare za Polisi na kuwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kupiga risasi moja angani.
Sirro alisema baada ya kuwaweka chini ya ulinzi, walimwamuru Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Jerry Oge (28) kulala chini na kumpora Sh milioni 35 na kutoweka nazo kwa kutumia gari aina ya Noah ikiwa na namba bandia za usajili T549 BPK.
“Baada ya tukio hilo, uchunguzi na upelelezi ulifanyika na kutokana na taarifa za raia wema majambazi watatu walikamatwa,” alisema.
Alisema majambazi hao walipohojiwa walikiri kuwapo kwa mtandao wao kutoka Kenya na nchi zingine jirani na kuwa na silaha nyingi.
Alisema pia waliwaonesha nyumba walimokuwa wamepanga na kuendesha ujambazi maeneo ya Mbezi Chini na Kawe.
Aliongeza kuwa walikuwa wakifanya ujambazi kila wiki na kugawana fedha ndani ya nyumba hiyo huku wenzao kutoka nchi za jirani wakirudi kwao.
“Baada ya kufika kwenye nyumba hiyo tulifanya upekuzi na kukuta silaha za kijeshi bunduki tatu aina ya SMG na magazini nane na risasi 120, bunduki aina ya shotgun, pump action tatu na risasi 130, bastola 16, magazini tupu moja na risasi 548, radio za upepo 12 na vijaza umeme vitatu vya redio hizo.
“Vionambali vitatu, pingu za plastiki 45, fulana tatu zisizopenya risasi, mkasi wa kukatia vyuma vigumu, mtaimbo mmoja wa kuvunjia milango, risasi baridi za kutishia 37, kasha moja la vifaa vya kusafishia silaha, nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, mashine ya kuhifadhi kumbukumbu moja na seva za kamera za CCTV na panga moja,” alisema.
Vingine vilivyokamatwa ni gari namba T 950 DGC aina ya Noah la rangi ya fedha likiwa na namba bandia T 549 BPT, Toyota Alphad namba T 987 CLH.
Kamanda Sirro alisema mbali na matukio hayo, uchunguzi wao ulibaini kuwa walipora bunduki aina ya shotgun namba 006091830 ikiwa na risasi moja maeneo ya Mbozi Chang’ombe ikiwa ni miongoni mwa bunduki tatu za aina hiyo zi-lizokamatwa.
“Baada ya kuwahoji walisema wanahusika na mtandao wa majambazi wa msitu wa Vikindu na kwamba wana silaha nyingi ziki-wamo zilizoporwa kituo cha Polisi cha Stakishari, na walipofika tuliwatanguliza kuongoza askari wenzao lakini wakawapiga risasi na kuwaua,” alisema.
Alisema wakiwa msituni humo ghafla walisikia milio ya risasi kwa mbele na askari walilala huku zikisikika sauti za ‘mmetuua sisi’ ambapo askari hao walishuhudia majambazi hao wakichelewa kulala chini wakati risasi zinapigwa, huku wakiwa wamejeruhiwa tumboni na kifuani na kuvuja damu nyingi.
“Wakati askari wanakimbia mbele, wakakuta SMG ikiwa na magazini tupu. Kimsingi wale majambazi watatu waliokuwa waki-sumbua Jiji walipelekwa Muhimbili na daktari akathibitisha kuwa walishapoteza maisha,” alisema.
Alisema upelelezi unafanyika na silaha zinazifanyiwa uchunguzi kubaini kama zitakuwa ni miongoni mwa silaha zilizoporwa kwenye tukio la CRDB Vikindu.
Kamanda Sirro alisema Jeshi hilo lilikamata watuhumiwa sita waliohusika na kuvunja nyumba na kuiba ambao ni Selema Mohamed (24), Twenye Abdalah (35), Bimu Yahaya (26), Abdala Mohamed (25) na Deogratius Oscar (19).
Aliongeza kuwa walikamata pia watuhumiwa wanne kwa wizi wa magari manane likiwamo la kibalozi.
0 comments:
Post a Comment