IGP Mangu |
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ramadhani Nganzi aliiambia JAMBO LEO kwa njia ya simu jana kutoka Musoma kwamba mwanamke huyo alikamatwa akiwa na mabinti watano akitaka kuwauza..
Kamanda Nganzi alisema mabinti hao wenye umri wa kati ya miaka 15 na 23 ni wakazi wa kijiji cha Muruvyagiza, wilayani Ngara mkoani Kagera, ambako ndiko mwanamke huyo aliwatoa akiwasafirisha hadi Masinki, kwa nia ya kuwauza na kuwaozesha kwa wanaume kwa bei ya kati ya Sh 150,000 hadi Sh 300,000 kila mmoja kulingana na umri, uzuri na tabia.
Alisema Polisi baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya biashara hiyo ya binadamu, waliweka mtego na Septemba 4 walimkamata mwanamke huyo na baada ya kumhoji alikiri kuwachukua mabinti hao mkoani Kagera kuja kuwauza.
Alisema jitihada zinafanyika ili kuwasiliana na wazazi wa mabinti hao kwa ajili ya kuchukua watoto wao.
Hata hivyo, Kamanda Nganzi hakutaja mabinti hao kwa majina kwa ajili ya usalama.
Alisema wanaendelea na uchunguzi kujua mtandao wa mwanamke huyo na pia kama biashara hiyo anaifanyia Mara pekee au na hata nje ya mkoa.
Alisema baada ya upelelezi kukamilika watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma ya kufanya biashara ya binadamu kinyume cha sheria.
Kamanda Nganzi alisema katika tukio lingine polisi, kwa kushirikiana na Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU) walikamata watu wawili Godfrey James (39) wa Chalinze, Pwani na Adeus Evarist (34) wa Mwanza, wakiwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria.
Alisema watu hao walikamatwa juzi kwenye kijiji cha Hunyari, Bunda, baada ya kupekuliwa na askari na kukutwa na vipande vitatu vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 15 ambavyo thamani yake ni zaidi ya Sh milioni 18 na kwamba upelelezi ukikamilika watawafikisha mahakamani.
Aidha, Kamanda Nganzi alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi kukabiliana na vitendo ya uhalifu.
0 comments:
Post a Comment