Videos

Wasomi CUF wamkataa Lipumba

JUMUIYA ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tawi la CUF Mlimani (UDSM) imeunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) hivi karibuni Zanzibar kuwavua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Abdul Kambaya.

Pia imeunga mkono uamuzi wa kuwasimamisha uanachama viongozi hao na aliyekuwa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Jidawi Chande, alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam ambapo alisema uamuzi huo una lengo la kukifanya chama kizidi kuendelea.

“Sisi kama jumuiya ya vyuo vikuu wa CUF tawi la Mlimani tunakubaliana na kupongeza uamuzi wa Baraza Kuu na tunaziomba mamlaka zingine ndani ya chama ziendelee kufanya uamuzi mgumu wa kujenga chama chetu pale inapobidi,” alisema Chande.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Jumuiya hiyo inalaani fujo na kauli za kibaguzi zinazoendelea kutolewa na Profesa Lipumba na baadhi ya wafuasi wake kama ile ya Sakaya kuwa chama kina mpasuko wa Bara na Visiwani kama alivyonukuliwa na magazeti nchini.

“Ikumbukwe, kuwa Profesa Lipumba alikuwa Mwenyekiti wa Cuf kwa mujibu wa Katiba ibara ya 91 (1) na kwa kuheshimu na kutambua umuhimu wa Katiba pia Profesa Lipumba alitumia Katiba ya chama ibara ya 117 (1) inayompa uhuru kiongozi kujiuzulu wadhifa wake na alifanya hivyo kama Katiba inavyoelekeza.

“Pia ibara ya 117 (2) inaelekeza kiongozi atakayejiuzulu lazima barua yake ipelekwe kwenye mamlaka iliyomteua au kumchagua ili kukubali au kukataa kujiuzulu kwake, na ndivyo ilivyokuwa kwenye mkutano mkuu wa Agosti 21 na kukubali kujiuzulu kwake, hivyo basi kutokana na hayo ni wazi fujo na vurugu zinazofanywa na Profesa Lipumba hazina nia njema na Cuf bali ku-gawa chama,” alisema.

Alisema wao wanazuoni wanamshauri Profesa Lipumba kuachana na mpango wake wa kuvuruga chama kwa kuwa anachofanya anajidhalilisha na kujishushia heshima aliyojijengea miaka mingi katika jamii ndani na nje ya nchi.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment