Videos

Mahakimu 34 watimuliwa kazi


Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman
JAJI Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman ametangaza kutimua watumishi 34 wa Mahakama wakiwamo mahakimu 11 kwa utovu wa nidhamu, huku mahakimu 60 wakiwekwa kiporo.

Katika mahakimu hao, wamo wa ngazi ya wafawidhi, mahakimu wa mahakama za mwanzo za Rombo, Temeke, Bahi na Chamwino.

Jaji Chande alisema hayo, Dar es Salaam jana, baada ya kukabidhiwa ripoti ya utendaji kazi wa Mahakama na wasajili kuanzia Januari hadi Agosti, kutokana na kujiwekea utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kwa uwazi.

Alisema watumishi hao walifukuzwa kazi Agosti 18, baada ya kikao cha Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ndiyo ya nidhamu kukaa na kutoka na uamuzi.

“Tumefukuza kazi watumishi 34 kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu ambapo mahakimu ni 11 na maofisa wengine 23 wa Mahakama.

“Lakini pia mfahamu hii ni idadi ndogo ya watendaji ya Mahakama, ambapo Machi tulikuwa na watendaji 6,406 na waliofukuzwa kazi 34 ni asilimia 0.005, ambao ni wafanyakazi wachache, lakini kwa Mahakama ni doa kuwa na mahakimu au watendaji wenye kasoro au dosari,” alisema Jaji Chande.

Alisema walifikia hatua hiyo kwa mmoja wa mahakimu hao aliyetumia muhuri wa Mahakama kinyume na utaratibu na sheria kwa masuala binafsi, hili ni kosa la kinidhamu, kwa hiyo alifunguliwa mashitaka mashahidi wakaitwa na Kamati ya Maadili ikaamua na Tume ikathibitisha wakafukuzwa kazi.

Alisema mwingine alichangia kusaidia mtu kufungua kesi moja kwenye mahakama mbili tofauti, ambayo hiyo iliathiri utendaji haki kwa kutolewa hukumu mbili katika kesi moja.

Pia alisema hakimu mwingine alifungua shauri la mirathi bila hati ya kuthibitisha kifo, mashitaka yake yalithibishwa kwa kiwango kinachotakiwa na kuchukuliwa hatua ya kufukuzwa kwa sababu ni makosa ya kinidhamu.

Alifafanua kuwa kuna makosa ya kisheria ambayo hakimu au jaji hawezi kuchukuliwa hatua kama alijichanganya katika vifungu vya sheria, lakini katika mzaha wa sheria hao ndio wanapelekwa katika kamati za maadili kwa kukosa sifa.

Mahakimu viporo

Alibainisha kuwa wapo mahakimu 28 au 30 walioshinda kesi za rushwa, lakini Tume ikaona kwamba kutokana na tuhuma kuwa nzito ipo haja ya kuwajadili ili waone hatima yao.

Alisema wamefanya hivyo, kwa sababu tayari kuna vitendo vya utovu wa nidhamu kwa hiyo ni lazima wakae na kuamua ni hat-ua gani wachukuliwe kwa sababu walishaingia doa.

Jaji Chande alisema mahakimu wengine 32 walishinda kesi za jinai, lakini ni vema wawafungulie mashitaka ya maadili, bila kujali walishinda mashitaka ya jinai.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment