KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema Tanzania inapoteza kiasi kikubwa cha mapato kutokana na kushindwa kuhifadhi mafuta yanayoingizwa nchini hivyo kusababisha waagizaji kuhifadhi kwenye maghala binafsi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dotto Biteko alipokuwa akifanya majumuisho ya vikao vya kamati hiyo kwa waandishi wa habari.
“Kamati inaisisitiza Serikali kujenga mahali maalumu pa kuhifadhi mafuta yanayopakuliwa kutoka kwenye meli, kabla ya kwenda kwa wanunuzi ili kuisaidia kuwa na uhakika wa kiasi cha mafuta yaliyoagizwa nchini,” alisema.
Aliongeza kwamba hilo pia litasaidia kupata uhakika wa kodi stahiki za Serikali kujua kama zimelipwa, usalama pamoja na kuondoa mianya ya wizi inayoweza kujitokeza.
Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe (CCM) alisema mafuta yanapoagizwa yanaposhuka bandarini yanapaswa kufika katika kituo kimoja ambacho, wafanyabiashara wote wa nishati hiyo watachukua.
Alisema hatua hiyo imekuwa ikisababisha mianya ya wizi huku akiitaka Serikali kuhakikisha inakuwa na sehemu moja ya kuhifadhia mafuta kabla hayajasambazwa.
“Kamati yetu imeafanya kazi na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), tulipowauliza kuhusu utaratibu wa usambazaji mafuta, wamekiri ni Tanzania pekee ambayo unaweza kuyaingiza nchini na kila mfanyabiashara akaweka kwenye ghala lake, nchi nyingine yanawekwa kwenye ghala la pamoja la Serikali kwanza kabla ya kwenda kwa wafanyabiashara binafsi,” alisema.
Alifafanua kuwa, “kwenye mnyororo wa mafuta, TPA ndiye anahifadhi mafuta, lakini anahifadhi mafuta kidogo sana na kila muagizaji anahifadhi kwenye ghala lake, wakati umefika Serikali itengeneze eneo malumu la kuyahifadhi yakitoka kwenye meli”.
Alisema hali hiyo itasaidia Serikali kuwa na uhakika wa kiasi mafuta yaliyoagizwa nchini, itakuwa na uhakika wa kulipwa na kodi stahiki za Serikali, usalama wa mafuta na kuondoa mianya ya wizi mdogo mdogo unaofanyika.
Pia kamati hiyo imeiagiza Serikali kupeleka majibu ya kutosha kwa kamati hiyo kuhusu sakata zima la uagizaji mafuta mabovu na upungufu wa mafuta ya taa ili jambo hilo lisijitokeze tena nchini.
Alisema wameiomba Wakala wa Uagizaji Mafuta wa Pamoja (PPA ) watoe maelezo ya kutosha kwa nini kulitokea changamoto ya upungufu wa mafuta ya taa nchini na hatua zilizochukuliwa.
0 comments:
Post a Comment