Fidelis Butahe, dodoma
WABUNGE vijana wameishauri Serikali kubadili mfumo wa elimu wakieleza kuwa umekuwa chanzo cha vijana wengi nchini kushindwa kujiajiri na kutegemea kuajiriwa.
Wakizungumza katika semina kwa wabunge vijana iliyofanyika jana mjini Dodoma, wabunge hao walisema hata wale wanaosaka ajira, hukwama kwa kigezo cha uzoefu huku baadhi wakihoji sababu za wanafunzi waliofeli kutowekewa utaratibu wa kuendelea na masomo.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Lucy Mollel alisema: “Mfumo wa usimamizi wetu wa elimu umekuwa janga, hatujui tunataka kuzalisha kundi lipi la vijana.”
Aliongeza: “Miaka ya nyuma kulikuwa na utaratibu wa watu walioshindwa Kidato cha Sita kufanya mitihani fulani na kuendelea na masomo ila kwa sasa hakuna. Juzi tumeshuhudia jinsi wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma walivyofukuzwa badala ya kusaidiwa. Uamuzi ule wa Rais Magufuli (John) umewanyima fursa ya kuweza kujikwamua.”
Alisema Serikali haipo kwa ajili ya kuwahukumu vijana na kwamba wanafunzi kufukuzwa kwa kigezo cha ufaulu mdogo, si jambo la busara.
Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi alisema ni muhimu kwa Serikali kuboresha Sera ya Elimu ili iendane na mazingira ya sasa na kuwaandaa vijana vizuri.
“Ili tuweze kufanya jambo lazima tuboreshe sera ya elimu ili imuandae kijana awe na fikra za ujasiliamali na kujipatia kipato,” alisema Shangazi.
Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Chacha alisema elimu ni tatizo kubwa kwa vijana kwa maelezo kuwa ni ngumu kumkuta kijana aliyemaliza chuo amejiajiri na kutoa mfano jinsi miaka ya nyuma wanafunzi walivyokuwa wakifundishwa elimu ya kujitegemea, jambo alilosema kwa sasa halipo.
“Kama vijana lazima tuhakikishe kuwa mfumo wetu wa elimu unabadilika na hili tuliseme bungeni, lazima tuhoji hawa wanafunzi wanaofeli na kushindwa kuendelea na masomo wanasaidiwa vipi?” alihoji.
0 comments:
Post a Comment