Videos

Makonda ahimiza kusaka wahalifu ‘gesti’


Paul Makonda
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema Jeshi la Polisi linafanya msako dhidi ya wahalifu ambao hulala kwenye nyumba za wageni.

Makonda alikuwa akitolea ufafanuzi taarifa anayodaiwa kuitoa kwa wakuu wa wilaya kukamata wanaolala kwenye nyumba za wageni muda wa kazi.

Alisema: “Kulala mchana si kosa, msako unaofanyika ni wa kutafuta wahalifu ambao wengi hukaa kwenye nyumba za wageni ili kufanya uhalifu usiku.”

Hata hivyo, baada ya ufafanuzi wa Makonda baadhi ya wananchi walipinga msako huo wakidai ni vigumu kugundua wahalifu na wasio wahalifu ndani ya nyumba hizo hivyo msako huo utaumiza wasio na hatia.

“Kauli za Makonda mara kadhaa zimekuwa zikileta mkanganyiko katika jamii, anatoa ufafanuzi kwamba si wanaolala mchana, lakini ni msako wa wahalifu katika nyumba za kulala wageni, hivi unawezaje kujua kwamba huyu ni mhalifu na mwingine sio?’’ alisema Ludovick Materu wa Temeke.

Alisema polisi wanapofanya msako huchukua watu wote walioko kwenye nyumba, hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi wasio na hatia ambao wamepumzika.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema litaendelea na operesheni dhidi ya watuhumiwa wanaofanya biashara ya nyumba za wageni kinyume cha sheria.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Jeshi hilo kubaini kuwa baadhi ya nyumba zimekuwa zikitumika kuhifadhi wahalifu, dada poa na kaka poa, hivyo Polisi inawajibika kufuatilia na kuwakamata.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema ni wajibu wa Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za wageni, hoteli, migahawa, vilabu vya vileo, kumbi za starehe zinazokesha na zisizokesha.

“Kimsingi niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na operesheni za kusaka watuhumiwa wakiwamo wanaofanya biashara ya nyumba za wageni kinyume cha sheria, majambazi na wahalifu wengine,”alisema.

Aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi kuwajibika kutambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na kuwachukulia hatua stahiki ili kuimarisha usalama.

*Imeandikwa na Sharifa Marira, Hussein Ndubikile na Salha Mohamed
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment