SIKU nne tangu madereva 15 wa malori kutoka Tanzania na Kenya kutekwa na waasi wa kundi MaiMai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamesimulia walivyoishi na waasi hao kambini na jinsi walivyofanikiwa kuwatoroka.
Wakizungumza jana katika mahojiano maalumu na JAMBO LEO wakiwa nchini Congo, walisema walikuwa wakilazimika kusota wakitumia tumbo kwa mwendo mrefu msituni, baada ya kuamriwa na askari hao ili kukwepa wasionekane na majeshi ya Serikali ya nchi hiyo wanayopambana nayo.
Mmoja wa madereva hao, Amdani Zarafi (41) ambaye alishikiliwa na waasi hadi kwenye kambi yao, alisema walitumia wastani wa saa kumi njiani kabla ya kufika kwenye kambi hiyo ambako kila dereva aliamriwa kupiga simu kwa bosi wake na kumweleza kilichotokea.
“Tulianza safari kuelekea porini saa 2:00 asubuhi baada ya kuchomewa magari na tulifika kwenye kambi yao saa kumi jioni. Mwendo ulikuwa ni mchaka mchaka tu, ulikuwa ni pori kwa pori,” alisema Zarafi.
Alisema walipofika kambini waliendelea kuwekwa chini ya ulinzi huku simu, leseni, fedha na funguo za magari wakiwa wamenyang’anywa na waasi hao.
Aliongeza kuwa waasi hao waliwaamuru kuwa watulivu huku wakisisitiza ombi lao kwa kila mmoja kuzungumza na bosi wake na kumweleza hali halisi kwamba wanatakiwa kulipa Dola 4,000 za Marekani kila mmoja ili aachiwe.
Alisema waasi hao walitoa angalizo kwa mabosi wao kwamba endapo taarifa zitafika kwa wanajeshi wa Jeshi la DRC na wao kufuatwa walipojificha, basi madereva hao wangeuawa.
Zafari alisema wakati wakiwa porini siku ya pili huku wakiendelea kuwasiliana na mabosi wao wale waasi walimtuma mmoja wao kwenda mjini kununua unga kwaajili ya kuwalisha madereva
hao.
“Wakati yule muasi akirudi kutoka kununua unga, wanajeshi wa DRC ambao walikuwa wanatufuatilia walimuona na kuanza kumfuatilia nyuma hadi wakafanikiwa kufika kambini,”alisema na kuongeza:
“Wakati akiwa njiani kuja kambini, yule muasi aliwaona wale wanajeshi akawa anakimbia na alipofika tu kambini aliwaambia waasi wenzake kambi imevamiwa na wanajeshi. Walipoambiwa hivyo, wale waasi walituamuru tuondoke hapo na kuwafuata watakako kwenda, ikabidi tuaze kuwafuata baada ya muda tukasikia risasi zinalia tukaanza kukimbia nao.
Alisema baada ya hapo tulitawanyika kila mmoja kwake wale wanajeshi wakaendelea kupiga risasi na waasi wakakimbia ndipo wanajeshi wakawaokoa madereva na kuwahifadhi kwenye kambi yao ya jeshi.
Naye Kumbuka Suleimani (40) ambaye alifanikiwa kutoroka mikononi mwa waasi hao, alisema walitembezwa umbali mrefu kukatisha misitu hata kulala njiani ili kufika kwenye pori lingine ambalo ni maficho ya waasi hao.
0 comments:
Post a Comment