Videos

Wazee wamwomba JPM akutane na viongozi wa dini


Rais John Magufuli
BARAZA la Wazee wa Chadema, limemwomba Rais John Magufuli (pichani) apokee na kuwasikiliza viongozi wa dini nchini ambao wanataka kumwona ili kutatua mgogoro baina ya vyama vya siasa na Serikali.

Aidha, wametoa angalizo kwa Serikali kuhusu taarifa za kutaka kukifuta chama hicho, wakisema uamuzi huo utahatarisha amani ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Baraza hilo, Roderick Lutembeka alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, siku saba baada ya Chadema kuahirisha maandamano na mikutano ya kupinga wanachamini ni ukiukwaji wa demokrasia nchini.

Chadema kupitia Kamati Kuu yake ya Agosti 27 walitangaza mkakati mpya wa kudai demokrasia ambao ulipewa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ambao ulisababisha taharuki nchini kwa kilichohofiwa kuwa ni uvunjifu wa amani.

Lutembeka alisema uamuzi wa viongozi hao wa dini kuingilia kati mgogoro huo na kuomba Chadema isubiri kabla ya kuchukua hatua, ulikuwa wa busara hivyo kumwomba Rais Magufuli awapokee na kuwasikiliza.

Alisema viongozi wa dini ni muhimu katika jamii iwapo Rais atashindwa kuwasikiliza, atadhihirisha kwa jamii kuwa ni jeuri na mwenye kiburi.

Alisema uamuzi wa viongozi na Kamati Kuu kuahirisha maandamano na mikutano ni ishara tosha kuwa chama hicho ni cha kidemokrasia na haki, kwa kuonesha usikivu na uvumilivu.

Lutembeka alisema wanatumia nafasi hiyo kupongeza wadau walioshiriki kuepusha mgogoro ambao ungetokea kwani ishara zilionesha kuwa Serikali na Jeshi la Polisi walijipanga kuleta machafuko nchini.

Kuhusu mpango wa kufuta chama hicho, Katibu huyo alisema katika uchunguzi wao, walipata taarifa zinazopangwa na Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Vyama ili kuifuta Chadema.

Alisema iwapo Serikali itafikia uamuzi huo ni dhahiri inataka kuhatarisha amani na upendo uliopo nchini kwani hawatakuwa tayari kukubaliana nayo.

“Wakati kukiwa na jitihada za kurejesha uhusiano mzuri baina ya pande ambazo zinakinzana kwa mujibu wa Sheria na Katiba tumepata taarifa kuwa upo mkakati wa kufuta chama, kwa hili hatutakubali,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment