ALIYEKUWA mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, anajiandaa kuweka wazi ushiriki wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba katika mchakato wake wa kuhamia Chadema mpaka kuwa mgombea urais.
Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hii akiwa Nairobi nchini Kenya jana, Lowassa ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu, wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, alisema akirudi kutoka safari hiyo, atafafanua mbele ya vyombo vya habari, tuhuma dhidi yake zilizotolewa na Profesa Lipumba.
“Kwa sasa naomba uniache kwanza maana nipo safarini Nairobi, nikija Dar es Salaam nitazungumzia suala hilo kwa undani kupitia vyombo vya habari, hivyo subirini nirudi,” alisema Lowassa.
Madai ya Lipumba
Hivi karibuni Profesa Lipumba alitupa lawama moja kwa moja kwa Lowassa, kwamba ujio wake ndani ya Ukawa, unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, ndiyo ulisababisha matatizo katika vyama hivyo kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, kabla ya kujiunga kwa Lowassa Ukawa, vyama hivyo walikaa kikao ambacho aliwashauri viongozi wenzake wa Ukawa kutazama mtu anayeweza kuendana na mahitaji yao awe ndani au nje ya umoja huo.
Alisema ni kweli aliona wangeweza kupata ushindi kupitia Lowassa, lakini hata ushindi huo ungepatikana, wangeenda kusimamia mambo gani? Maana suala ni kusimamia katika eneo fulani.
Alifafanua kuwa suala lililopo katika siasa ni baada ya kuchaguliwa, uunde serikali ili usimamie misingi fulani ambayo itakidhi mahitaji ya wananchi. “Sisi tulisema tunahitaji serikali inayowajibika, itakayopambana na rushwa, itakayotumia rasilimali za nchi vizuri, na itakayohakikisha mali ya asili ya Tanzania inawasaidia Watanzania wote,” alisema na kuongeza kuwa hayo Lowassa asingeweza.
Baada ya kikao hicho cha kumjadili Lowassa, Profesa Lipumba alisema walifanya kingine wakiwa na Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa Chadema); Mbatia (James, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na Lowassa kujadili suala hilo kwa mara ya pili kuwa ni vyema CUF, wakaribishwe kwanza ambapo walikuwa hatua za mwisho.
Alisema baada ya mchakato huo kwisha, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alianza vikao vingine visivyomshirikisha yeye Lipumba, kwa kumwalika Mbowe ili wafanye mazungumzo. Lipumba alidai kuwa Mbowe alipoitwa na Maalim Seif kwenda Zanzibar, alimfuata na kumweleza kuwa ameitwa na Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
“Mbowe alinipigia simu akaniambia kuwa ameitwa kwenye kikao na kwamba ndio kulikuwa na hoja ya Lowassa kuingia Ukawa, wakati Chadema walikuwa na msimamo kuwa kwenye Ukawa asikaribishwe mtu wa nje,”alifafanua.
Alisema Mbowe aliendelea kumweleza kuwa, baada ya kikao kile ndipo Chadema waligundua kuwa kuna sintofahamu ndani ya CUF, jambo lililowafanya wao Chadema watoe hoja ya kuwa na mgombea wao, kwakuwa watakuwa na wabunge wengi basi hata Waziri Mkuu atatoka huko na CUF itatoa mgombea mwenza.
Lipumba alisema baada ya hali hiyo kutokea; ya Maalim Seif kufanya vikao vingine bila kumshirikisha, alikuwa katika wakati mgumu maana hata mazungumzo yale hakushirikishwa, ilihali yeye ndio Mwenyekiti wa CUF na yalikuwa yanafanywa na Katibu kimnya kimnya.
0 comments:
Post a Comment