MWANASHERIA Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amejitosa kusaidia watuhumiwa 83, wanaodaiwa kukamatwa kutoka maeneo mbalimbali nchini na kushikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kwa kuisema vinaya Serikali, ikiwa ni pamoja na kutumia neno dikteta.
Ametoa kauli hiyo jana alipozungumzana waandishi wa habari, katika Makao Makuu ya chama hicho Dar es Salaam, kuhusu mambo yanayoendelea kutokea tena kimnya kimnya nchini.
Alidai kuwa watu hao wamekamatwa kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa agizo la wakuu wa Polisi, huku wengine wakiteswa kwa madai kuwa wameandika kauli zinazomhusu Rais John Magufuli na utendaji wake katika mitandao ya kijamii.
Alitaja waliotoa maagizo hayo kuwa ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Diwani Athumani, Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro na makamanda kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa madai ya Lissu, kukamatwa kwa watu na kuteswa kutokana na sababu zinazohusu Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta) na hali ya kisiasa nchini tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, kunazidi kushika kasi.
Alidai kati ya watu hao, watuhumiwa kumi amewatembelea walipo; nane wapo Kituo cha Polisi Olysterbay na wawili Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam huku watu wengine 73 taarifa zikikosekana kuhusu vituo walikopelekwa.
Lissu aliwataja kwa majina watu hao nane ambao wapo Kituo cha Polisi Oysterbay kuwa ni Aristotle Ngasi, Hosia Mbuba , Ignasia Mzenga, Shakira Abdallah Makame na Dk David Nicas ambaye alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Busega 2015.
Wengine ni Mdude Nyangali, Juma Salum na Suleiman Said na wawili wanaodaiwa kuwa Kituo Kikuu cha Polisi ni Ben Nzogu na Mussa Sikabwe.
Kwa mujibu wa madai ya Lissu, waliopo wa Kituo cha Oysterbay wamemweleza kuwa wamekuwa wakipata manyanyaso ya hali ya juu wakiwa mahabusu.
Alidai watu hao walimweleza kuwa wamekuwa wakitolewa mahabusu usiku na kupelekwa katika eneo la Mikocheni, ambako kuna kikosi kazi kinachojumuisha Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, ambao kazi yao ni kuwapiga na kuwatesa.
“Nchi si kwamba haina sheria zinazokataza mambo hayo na si kwamba yanayofanywa na Polisi hayakatazwi. Katiba ya Nchi ibara ya 13 kifungu kidogo cha 6 I, kinaeleza kuwa ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha,”alisema.
Alisema kupitia ibara hiyo ni wazi kuwa jeshi hilo linakiuka Katiba kutokana na kuwa kutoa habari kunalindwa na Katiba si Serikali ya Rais Magufuli. Aliongeza kuwa jambo la kushangaza, kuna baadhi ya watu hao wamekaa mahabusu kwa siku 46 bila kupelekwa mahakamani, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwani kisheria inabidi mtu akae mahabusu saa 24 tu.
“Kama watu hao wangekuwa kizuizini kwa kauli ya Rais, tungesema kuwa ni kizuizi kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1962 lakini kwa kuwa ni kwa mujibu wa Jeshi la Polisi ni ukiukwaji wa Katiba,” alisema.
Alisema kama watu hao hawataachiwa huru Jumanne ijayo, hasa wale 10 ambao wanafahamika au kama watakuwa hawajapelekwa mahakamani au kuachiliwa kwa dhamana ya Polisi, chama hicho kitakwenda Mahakama Kuu kufungua maombi kwa mujibu wa utaratibu wa sheria.
Alifafanua kuwa kifungu cha 390 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinaruhusu Mahakama Kuu kutoa amri ya kuelekeza mtu ambaye anashikiliwa kinyume cha sheria, kuletwa mahakamani au kuachiwa huru.
“Tunataka viongozi hao waseme ni lini Katiba imeruhusu wafanye hivyo, maana kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti kifungu cha 32 inaeleza kuwa halitakuwa kosa kutoa kauli ambazo lengo lake ni kuonesha Serikali imekosea na hatujafanya kosa la jinai, hivyo waliokamatwa kwa kosa hilo hawana kosa,”alisema na kuongeza.
“Kwa maoni yangu ni kuwa hakuna kosa pale, hivyo nitaisema kauli yangu popote na muda wowote labda nisiwe hai na hakuna mahabusu itakayonifunga mdomo.”
Gazeti hili lilimpigia simu IGP Mangu, ilia toe ufafanuzi wa madai hao, lakini ilipokewa na msaidizi wake aliyeagiza atafutwe msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, ambaye alielekeza makamanda wa mikoa ya kipolisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ndio wazungumze. Hata hivyo makamanda hao simu zao ziliita bila majibu.
0 comments:
Post a Comment