Videos

Waliokumbwa tetemeko wasimulia masahibu


WAATHIRIKA wa tetemeko la ardhi lililokumba Mkoa wa Kagera wameeleza masahibu yaliyowakuta wakati wa tukio hilo la ghafla lililowaacha wengi bila makazi baada ya nyumba zao kubomoka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili walisema lilikuwa tukio la ghafla ambalo hawajapata kuliona tangu wazaliwe.

Mmoja wa waathirika hao, Emilius Lutajayana alisema wakati linatokea alikuwa ndani amelala lakini ghafla alishituliwa kwa kupondwa na kompyuta mpakato iliyokuwa juu ya kabati.

“Nilikuwa nimelala muda huo. Kilichonishitua kutoka usingizini ni kompyuta yangu iliyokuwa juu ya kabati kuniangukia na kuniponda. Nilinyanyuka lakini miguu ikawa haina uwiano na nyumba ilikuwa kama mawimbi ya ziwani,” alisema na kuongeza:

“Baada ya sekunde kadhaa nilitoka nje na tayari kuta za nyumba zilishaanguka ingawa hakuna mtu kwenye familia yangu aliyepoteza maisha, ila mbwa wangu walikufa kwenye tetemeko hilo.

“Kwa kweli tunamshukuru Mungu ila ni tukio la kusikitisha kwa jinsi watu walivyopoteza maisha na mali zao.”

Happyness Felician alieleza kuwa tetemeko lilimkuta ndani ya kibanda cha mabao na mtikisiko ulimfanya ashindwe kutambua kilichotokea na alishuhudia nyumba zikianguka bila kujua chanzo.

Alisema akiwa kwenye kibanda alikumbwa na hofu akidhani mwisho wa dunia umefika na baada ya hali kutulia, aliona watu wakikimbia ovyo huku wengine wakiangua vilio na ndipo fahamu zilimtuma kuchukua mwanawe mchanga na kutoka nje.

Linus Julius wa Hamugembe ambaye alivunjika mkono akieleza kuwa hakupata kuona jambo kama hilo maishani mwake, kwani akiwa nyumbani kwao, alishangaa kusikia mtikisiko mkubwa huku baadhi ya nyumba zikianguka.

“Ni ajabu na kweli hata nashindwa kueleza tukio hili lilivyo. Nikiwa nyumbani ulitokea mtikisiko mbao maishani mwangu sikuwahi kuusikia. Nilisikia kama upepo nilijikuta naangukiwa na ukuta na kuvunjika mkono. Nilitambua kuumia baada ya hali kutulia,” alisema Julius.

Godwin Laurian wa Rwamishenye alidai kuwa wakati tetemeko hilo linatokea, aliona ardhi ikipanda na kushuka mithili ya mawimbi ya ziwa na kujikuta akishindwa kukimbia kujiokoa na alipondwa na ukuta wa nyumba akajeruhiwa kichwani.

Mwingine ni mwanafunzi wa sekondari ya Ihungo, Emmanuel Renatus, ambaye alivunjika mguu wa kushoto akidai aliangukiwa na ukuta wa bweni wakati akijiokoa.

Enjoy Jovit wa Rwamishenye ambaye alivunjika uti wa mgongo alisema alikutwa na hali hiyo kwa kuangukiwa na ukuta wakati akijiokoa wakati anatoka ndani ya nyumba ukuta ukamwangukia.

“Nashindwa nianzie wapi kueleza tukio hili na sijui kama nimenusurika. Kila mahali hali ilikuwa mbaya kutokana na tetemeko na sikuwa nahafamu hadi nilipohamishwa baada ya kufika hospitalini.

“Ni mara yangu ya kwanza kuona jambo hili ila mwanzo nihisi ni mtikisiko wa umeme,” alisema Jovit akiwa hospitali ya rufaa ya Bukoba alikolazwa.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment