WAKATI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa(pichani) akisema Serikali haiwezi kukubali hoja za kupungua kwa mizigo bandarini na kudorora kwa uchumi wa Taifa zilizotolewa bungeni na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana, mpaka itakapopata taarifa sahihi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Hazina, wadau wameitaka iachane na utaratibu wa kusubiri takwimu badala kuchukua hatua stahiki.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana bungeni katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, baada ya Mbowe kumhoji kuhusu mkakati wa Serikali kukabiliana na mdororo wa uchumi na kupungua kwa mizigo kwenye bandari za Tanga na Dar es Salaam, huku kampuni za usafirishaji na hoteli zikifunga biashara.
Takribani wiki moja iliyopita, Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilitembelea bandari ya Dar es Salaam na kubaini kwamba mizigo inayoingia imepungua kutoka kontena 40,000 Agosti, mwaka jana hadi 1,000 katika mwezi kama huo mwaka huu.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Stephen Ngatunga na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja jana waliieleza JAMBO LEO sababu za mizigo kupungua na kuitaka Serikali kukubali hali halisi na kuitatua.
Katika swali la nyongeza, Mbowe alisema BoT ilitoa ripoti yake ya tathmini ya uchumi kwa miezi mitatu inayoonesha kushuka kwa usafirishaji na uingizaji wa mizigo nchini, kuporomoka kwa sekta ya ujenzi na mzunguko wa fedha.
Katika majibu yake, Majaliwa alisema Serikali itakutana na wadau kujadili jambo hilo huku akieleza sababu za kupungua kwa mizigo bandarini na jinsi nchi zilivyothibitisha kuanza kutumia bandari za Tanzania kupitisha mizigo yao.
“Mizigo katika bandari na mipaka yetu imepungua kwa zaidi ya asilimia 60, asilimia 40 ya baadhi ya kampuni za usafirishaji zimefunga kazi zao, hivi hali hii Serikali inaijua? Inachukua hatua gani za makusudi za kurekebisha hasa ikizingatiwa uchumi ukipo-romoka mazao ya wakulima nao yanauzwa kwa bei ndogo?” Alihoji Mbowe.
Majaliwa alijibu akisema ni lazima Serikali ipate takwimu kutoka taasisi zake hasa BoT na kuzilinganisha za miaka ya nyuma, ili kubaini kama kweli kauli ya kushuka kwa uchumi ina ukweli.
“Serikali hii jitihada zake ni kuhakikisha uchumi unakua katika nyanja zote. Kupungua kwa mizigo bandarini kumekuwa kukizungumzwa na watu wengi, hata Kamati ya Bunge, lakini wadau peke yao hawatoshi, lazima tupate taarifa kutoka ndani ya Serikali na mwenendo wa uendeshaji wa bandari na mipaka yetu,” alisema Majaliwa.
Alisema Serikali itaendelea kupokea ushauri wa wabunge na wadau kuhusu hatima ya uchumi wa nchi, ili kama kuna udhaifu ufanyiwe kazi na kusisitiza kuwa mara zitakapopatika takwimu sahihi za uchumi, Bunge litajulishwa.
Akijibu swali la nyongeza la Mbowe, Majaliwa alisema wafanyabiashara maarufu wa meli duniani walimweleza kuwa usafirishaji mizigo umeshuka duniani kote, kutokana na kuporomoka kwa bei ya gesi na mafuta.
“Tanzania tunategemea mizigo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi na Zambia. Wote mnajua DRC na Zambia ni nchi zilizokuwa zinaelekea kwenye uchaguzi na kulikuwa na migogoro mingi… wiki iliyopita Rwanda na Kongo walithibitisha kwa barua kuanza kutumia bandari zetu kupitisha mizigo,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema tayari wafanyabiashara wa Rwanda na DRC wameihakikishia Serikali kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya kisasa inayoanzia Dar es Salaam-Tabora - Isaka.
Wadau
Minja alisema: “Kontena na mizigo haviingii bandarini kwa sababu kodi zinazotozwa hazina uhalisia na hazifanani na wenzetu wa Afrika Mashariki, gharama zinaingia kwa bei kubwa na kuuzwa kwa bei juu, hivyo wafanyabiashara wanapata hasara.”
Aliitaka Serikali kusikiliza ushauri wa wadau huku akibainisha kuwa kodi hazieleweki kwa maelezo kuwa kontena moja linaweza kutozwa kodi ya Sh milioni 40, lakini kontena hilo hilo likiingia nchini baada ya wiki moja, litatozwa kodi ya Sh milioni 60.
Ngatunga alisema Taffa walilizungumza suala hilo kabla halijatokea, wakati linakaribia kutokea na sasa linatokea, lakini ushauri wao ulipuuzwa.
Alitaja sababu tatu za mizigo kupungua bandarini kuwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), mfumo wa himaya moja ya ushuru wa forodha na kukosekana ushirikiano kati ya wao na viongozi wa Mamlaka husika.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano iko macho, haijalala na haijashindwa kuongoza nchi bali imeji-panga kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
“Serikali haijashindwa kuongoza nchi. Nataka niwahakikishie wabunge na wananchi wote,” alisema.
0 comments:
Post a Comment