SIKU 86 tangu Rais John Magufuli, ‘awateme’ wakuu wa wilaya zaidi ya 100, bado ‘wastaafu’ hao hawajalipwa mafao yao, baadhi yao wakiwa hoi na wengine wakiamua kujikita kwenye kilimo. Baadhi ya wateule hao wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete wanaishi hivyo kutokana na kilichoelezwa kutotarajia kuachwa kwenye uteuzi wa Rais Magufuli na kutegemea mafao hayo ya kustaafu.
Kwa mujibu wa mtoa habari wa JAMBO LEO ambaye pia alikuwa mkuu wa wilaya, baadhi ya rafiki zake walioshushwa wadhifa huo, wanaishi maisha ya kuungaunga kutokana na kutojipanga.
“Unajua hizi nafasi zinatokea kama bahati, wapo baadhi ya marafiki zangu walijiachia wakijua wanaweza kupata nafasi nyingine katika awamu hii, hivyo hawakujiandaa, ndiyo maana sasa ukiwasikia wanalalamikia mafao tu na wanaishi maisha magumu,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
DC huyo wa zamani alisema wapo wengine ambao wanaishi vizuri, lakini akashauri kwa ambao wanapata tabu akisema ni vema Serikali ikawapa mafao yao ili kuwafichia aibu mtaani.
“Kuna mmoja hana hata pa kukaa hivyo amerudi kwao, nadhani kitakachomwokoa ni hayo mafao,’’ alisema.
Wakuu wa wilaya waliozungumza na JAMBO LEO kwa sharti la kutotajwa majina walikiri kuwa na hali mbaya kiuchumi wakieleza hawajalipwa mafao yao. Mmoja wa wakuu wa wilaya walioachwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa aliyeomba kuhifadhiwa jina, alisema: “Kweli hali ni mbaya hatujalipwa, lakini najua Serikali ina mipango yake kwetu, naamini itatenda haki.”
Mwingine aliyekuwa mikoa ya Kanda ya Kati alisema: “Unajua kwa hali ilivyo lazima hali iwe ngumu kwani hatujapata mafao yetu na kama unavyojua, wengine hatukutarajia kuondolewa. Lakini kwa usikivu wake, Rais Magufuli ni vizuri akatulipa wakati huu ili kutuondolea aibu inayotukumba.”
Mwenyekiti wa Chama cha Kuweka na Kukopa (Saccos) cha MaDC hao walioachwa, Maneno Ramadhani alipoulizwa kuhusu suala la kiinua mgongo alikiri kutolipwa, lakini akasema Serikali imeahidi kulipa.
Hata hivyo, alisema ameamua kurudi kijijini na kujikita katika kilimo akiwa na imani Serikali itawalipa mafao yao.
Alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alikutana nao hivi karibuni kwenye uzinduzi wa Saccos yao na kuahidi kwamba mafao yao yanashughulikiwa.
“Tulikutana na Simbachawene kwenye uzinduzi wa Saccos yetu ambapo tulimwalika Rais John Magufuli lakini alibanwa na majukumu mengine, hivyo akamtuma waziri atueleze kuwa anajua kuwa tunadai mafao yetu lakini yanashughulikiwa,” alisema.
Maneno alisema hata hivyo, Simbachawene hakuahidi lini watalipwa fedha zao na kueleza wanasubiri namna itakavyokuwa bila kueleza kwamba watakwenda kumwona Rais Magufuli au la.
“Ajenda yetu haikuwa suala la mafao yetu, kwa kuwa tunajua ni haki yetu tutalipwa, lakini Waziri alilizungumzia akijua kwamba Serikali inadaiwa, hivyo alikuwa sahihi kutueleza, ingawa hajatwambia tutapewa lini,” alisema.
Alisema umoja huo ambao una wanachama zaidi ya 100 wote wa awamu ya nne, utajiendeleza na kwamba waliamua kuwa waliostaafu katika awamu hiyo kutokana na kujuana na kuzoeana tofauti na awamu zingine.
Alipoulizwa endapo wengine waliostaafu au watakaostaafu baadaye wanaruhusiwa kujiunga na umoja huo, alisema Katiba yao itaeleza kila kitu kuhusu watakaotaka kujiunga.
0 comments:
Post a Comment