Videos

Vyuo vikuu binafsi hatarini kukosa wanafunzi


Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako
HATUA ya Serikali ya kupandisha kiwango cha ufaulu wa kujiunga na chuo kikuu kutoka alama mbili hadi nne, itavifanya vyuo vikuu binafsi vikose wanafunzi katika mwaka wa masomo 2016/17, JAMBOLEO limeelezwa. Habari kutoka baadhi ya vyuo hivyo, ikiwamo vilivyofungwa kudahili wanafunzi mwaka huu, imeeleza kuwa uamuzi huo wa Serikali utawaondoa kwenye udahili wanafunzi 16,000 waliopata alama mbili katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni.

“Kuna zaidi ya wanafunzi 16,000 ambao hawatapata fursa ya kujiunga na chuo kikuu mwaka huu, kulingana na mwongozo wa sasa kwamba waliopata alama mbili wasidahiliwe,” alisema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Baamoyo, Profesa Costa Mahalu na kuongeza:

“Hiki ni kiama kwa vyuo vikuu binafsi, maana idadi ya waliopata alama nne ni ndogo na inawezekana wote wakaenda kwenye vyuo vikuu vya umma. Kibaya zaidi hakuna mahala ambako Serikali imepanga kuwapeleka hao ambao hawatadahiliwa.”

Kauli ya Profesa Mahalu iliungwa mkono na wahadhiri wengine kadhaa, waliosema kuwa kitendo cha Serikali kupandisha alama ya ufaulu wa kujiunga na chuo kikuu, kitaongeza ‘vilaza’ badala ya kuwapunguza.

Mmoja wa wahadhili hao kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (IMTU), ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa si msemaji wa chuo, alisema: “Mtu hawezi kuwa ‘kilaza’ akiwa chuo kikuu.”

Alisema: “’Ukilaza’ unaanzia elimu ya msingi na sekondari. Jambo la maana hapa si kupandisha kiwango cha ufaulu ili kuondoa ‘vilaza’, muhimu ni kuangalia mfumo wetu wa elimu kuanzia chini. Elimu yetu haisaidii watoto kufanya kazi, inataka wawe na vyeti tu.”

Mhadhiri huyo alibainisha kuwa kwa sababu Serikali haijaandaa mahala pa kupeleka wanafunzi waliopata alama mbili, sasa watatafuta vyuo nje ya nchi kwa gharama ya vyuo vya ndani.

Alipoulizwa ilikuwaje ikakubalika wenye ufaulu wa alama mbili wajiunge na vyuo vikuu na sasa imefutwa, mhadhiri huyo alijibu: “Ndiyo maana nasema Waziri anakurupuka. Haya yalikuwa makubaliano kati ya vyuo na TCU. Sasa yeye anakuja kuyatengua bila kupata ushauri.”

Kufunga vyuo

Katika hatua nyingine, baadhi ya wahadhiri wa vyuo vitano vilivyofungwa kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2016/17 walimtuhumu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako kwamba anatumika kuvihujumu. Kwa nyakati tofauti wasomi hao walisema hakuna sheria inayompa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, mamlaka ya kufunga vyuo, badala yake kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) anapaswa kuvieleza kasoro na kusimamia kuzisahihisha.

“Kuna mambo mengi ambayo sisi wadau tukiyaangalia tunashindwa kuelewa waziri ana nia gani na elimu ya Tanzania. Amekuwa akijiamulia mambo bila ushauri na kibaya zaidi anaingilia kazi za TCU,” alisema mmoja wa wahadhiri hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini.

Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) alieleza kuwa tangu Mei, Waziri amekuwa akifanya mambo matatu yanayoingilia utendaji wa vyuo vikuu na hata kutia hofu kwamba chini ya uongozi wake, kiwango cha elimu kitashuka.

Alitaja mambo hayo kuwa ni kuvifunga vyuo kudahili wanafunzi mwaka huu wa masomo, sakata la wanafunzi hewa na kupandisha kiwango cha ufaulu wa kujiunga na vyuo vikuu. Mapema Julai, Waziri Ndalichako alitangaza kuvifunga vyuo vitano kudahili wanafunzi kwa madai kuwa havijakidhi vigezo vya kuendesha kozi husika.

Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Bagamoyo (kozi zote), Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba (IMTU), Chuo Kikuu cha Dodoma (Utabibu), Chuo kikuu cha St. Francis na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar. Mmoja wa wahadhiri wa vyuo hivyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini kwa alichoeleza kuwa anaweza kuandamwa na Waziri Ndalichako, alisema:

“Utadhani kuna uadui kati yetu na Waziri, kumbuka hakuna sheria ya kufunga vyuo, lakini pamoja na kwamba tayari ameagiza tusidahili wanafunzi mwaka huu, hatuna barua rasmi inayotuzuia kufanya hivyo.” Aliendelea “Kuna hatua kadhaa ambazo lazima zipitiwe, moja, wanakuja wakaguzi ambao kibaya zaidi wanaokagua vyuo hivyo wote wanatoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao ni washindani wetu katika kutafuta wanafunzi.

“Kama watabaini kasoro wanakieleza chuo husika na kukitaka kifanye marekebisho. Cha ajabu sisi tumefanya marekebisho na hawajaja kukagua tena, lakini tunasikia tu kwamba tumefungwa.”

Mhadhiri huyo alipendekeza iwepo Bodi maalumu ya kukagua vyuo, badala ya kutumia wakaguzi wa chuo kimoja cha Serikali ambao wanaweza kuwa na maslahi binafsi.

“Mwaka huu UDSM ilianzisha kozi tatu mpya; Udaktari Kilimo na Majenzi. Hapa unaona kwamba wanaleta ushindani katika vyuo vya Sokoine, Ardhi na vingine vinavyoendesha kozi hizo. Kwa nini wasiwe na maslahi wanapovikagua ili wawapoke wanafunzi?” Alihoji.

Wanafunzi hewa

Wahadhiri hao walisema uamuzi mwingine unaohatarisha uhai wa vyuo vikuu binafsi ni kutafuta wanafunzi hewa kuanzia Mei.

“Utekelezaji wake umetuathiri sana kwa kuwa tangu Mei, Bodi imesitisha mkopo kwa wanafunzi wote. Fikiria sisi (vyuo binafsi) tunajiendesha kwa ada za wanafunzi, halafu Bodi inasitisha mkopo, tutalipaje mishahara ya walimu, bili za umeme na maji?” Alihoji.

Aliendelea: “Julai 25, Waziri Ndalichako alikoleza moto kwa kutoa agizo la kuzuia wanafunzi wa kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kwa madai kuwa hakuna pesa. Wanafunzi wakaruhusiwa waende likizo, lakini baada ya wiki mbili akatoa tena tangazo kuwa wanafunzi wanatakiwa kwenda kwenye mafunzo hayo Agosti 8.

“Mwanafunzi aliye likizo utampata wapi asaini fomu ili aingiziwe pesa za vitendo?. Maana pesa haiwezi kuingizwa mpaka asaini,” alihoji na kubainisha kuwa maagizo kama hayo aliyoyaita ya kukurupuka, ndiyo yanayoleta picha kwamba kuna wanafunzi hewa.

Mhadhiri huyo aliponda uamuzi wa Serikali kutumia Takukuru kutafuta wanafunzi hewa vyuoni, akieleza kuwa hauna tija. “Kuna wanafunzi wanatumiwa fedha halafu wanakuja kusaini baadaye, unamwitaje hewa wakati tatizo hilo umelisababisha mwenyewe.”

Majibu ya Wizara

Waziri Ndalichako hakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Ofisa Habari wa Wizara, Oliva Kato alisema Waziri ndiye mwenye dhamana na mambo yote yanayohusu elimu, hivyo uamuzi ule aliufanya kama mtu aliye na mamlaka ya kusimamia elimu. “Kama Waziri ameingilia mamlaka ya TCU ambaye angetakiwa kuleta malalamiko ni TCU, umeshasikia wamelalamika au unajua ukomo wa majukumu ya Waziri?” Alihoji Kato.

Aidha, alisema kuhusu vyuo hivyo kutopelekewa barua rasmi ya kusimamishwa kufanya udahili wa wanafunzi mwenye majibu ni TCU.

Kaimu Mkurugenzi wa TCU, Profesa Eliuter Mwageni alipotafutwa kwa njia ya simu atoe majibu, alisema haamini kama anaongea na mwandishi wa habari.

“Nitajuaje kama naongea na mwandishi, nitafute ofisini tutazungumza,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment