MWANASHERIA Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina hali mbaya kifedha kutokana na madeni inayoidai Serikali na ndiyo maana inataka kuondoa fao la kujitoa.
Lissu ametaka wafanyakazi kutetea maslahi ya mafao yao ambayo yanatumika vibaya na kwamba hawatakuwa na chochote cha kupoteza watakaposimama kidete kuyatetea.
Akizungumza na JAMBO LEO jana kuhusu tamko lake lililosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Lissu alisema wafanyakazi wakikaa kimya, watapoteza fedha na kuwataka kuacha kusikiliza wanasiasa uchwara wanaowashauri kukubali kuacha mafao yao hadi wafikie umri wa miaka 60.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema: “Ukweli, kama alivyosema CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kwenye moja ya taarifa zake za mwaka, mifuko ina hali mbaya ya kifedha.
Hii ndio sababu wenye mamlaka wanataka kuondoa fao la kujitoa. Wameigeuza mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa ‘shamba la bibi’ mpaka inakaribia kufilisika.”
Alisema wanasiasa wanaojivika uzalendo uchwara kuhusu fedha za wafanyakazi, wao wametengenezewa utaratibu maalumu ambapo wanakatwa na NSSF baada ya kumaliza ubunge wanarudishiwa fedha zao.
“Wanasiasa uchwara hawasubiri wafikishe miaka 60 ndipo wapate mafao yao ya kujitoa, wanachowahubiria wao hawakifanyi, wana ndimi mbili kama za nyoka, wafanyakazi amkeni, hamna chochote cha kupoteza isipokuwa minyororo yenu,” alisema Lissu.
Alieleza kuwa fedha za mifuko hiyo hazitajenga kiwanda chochote, ni siasa kutokana na kuwa si za Serikali, ni za wafanyakazi zinazotokana na makato yao ya mishahara.
Alisema Serikali imekuwa inatumia fedha hizo kama zake, wakati si zake, inafanya makosa kuzichota inapojisikia bila kurudisha. “Tumeshuhudia mara kadhaa fedha za wafanyakazi zikitumika kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwa makubaliano, kwamba Serikali ingerudisha kwa mifuko hiyo, lakini haijarudisha hata senti moja,’’ alisema Lissu.
Alisema fedha hizo zimejenga jengo la Usalama wa Taifa Oysterbay, nyumba za Polisi na Machinga Complex, hadi sasa haijarudishwa hata shilingi, ndiyo maana mifuko inayumba. Alisema fedha hizo zilijenga Daraja la Mwalimu Nyerere la Kigamboni na kwamba ana uhakika haitarudi hata senti moja.
0 comments:
Post a Comment