Videos

Mgomo wanukia fao la wafanyakazi



MGOMO wa wafanyakazi nchi nzima unatarajiwa kuitishwa na vyama vya wafanyakazi, ikiwa Serikali itaendelea na mchakato wake wa chini chini kuondoa fao la kujitoa katika mifuko ya jamii.

Akizungumza jana Dar es Salaam na waandishi wa habari, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Gratius Mkoba, alisema mbali na kuitisha mgomo huo, pia watahamasisha wanachama kujitoa kwenye mifuko yote ya hifadhi ya jamii.

“Tunawaomba wabunge waliangalie hili, ni vigumu sana kuingia kichwani kama leo hii tumefikia hatua ya kutaka mtu anayeacha kazi akiwa na miaka 25 au 30, akae hadi kufikia miaka 60 ndipo achukue pesa zake, sawa na yule aliyefanya kazi kwa kipindi cha miaka 60 na kustaafu.

“Hapa inaonekana wameshindwa kuelewa dhana nzima ya matumuzi ya pesheni, kwani lengo lake ni kumsaidia mfanyakazi anapokosa kazi ili maisha yaendelee,” alisema Mkoba.

Mratibu wa Kitaifa wa Mitandao ya Asasi za Kiraia Tanzania chini ya Mwamvuli wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olenguruma, ambaye ameshirikishwa katika sakata hilo, alisema pia watashawishi waajiri kusitisha kupeleka mafao katika mifuko hiyo.

Mkakati wa Serikali
Taarifa zilizosambaa hivi karibuni katika mitandao ya kijamii, zimeeleza kuwa Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA), inatarajia kufuta fao hilo na kuanzisha fao la kukosa ajira.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa kuondoa fao hilo uko katika hatua za mwisho kukamilika ili uwasilishwe bungeni, ingawa Mkurugenzi wa SSRA, Irene Isaka, amekaririwa akisema muswada huo upo katika hatua za awali.

Athari
Akifafanua athari za kufutwa kwa fao hilo, Mkoba ambaye pia ni Rais wa Chama cha Walimu (CWT), alisema muswaada huo utawaumiza zaidi wafanyakazi wa sekta binafsi, ambao wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mikataba ya miaka miwili au mitatu, ambapo ukiisha atalazimika kusubiri miaka 60 ndio achukue fedha yake, jambo ambalo ni sawa na kumkandamiza na kumnyima fursa.

“Lazima tusimame na tupinge hili kwani watu wengi wanapoaacha kazi, wanatumia fedha kujianzishia miradi yao ya maendeleo na kujikimu, lakini leo unamvyomtaka achukue akiwa na umri wa miaka 60, ni kumyima fursa.

“Hata wanafunzi wanapomaliza vyuo, hupenda kujiunga na kazi za mikataba ili wanapomaliza mikataba yao watumie fedha za mifuko ya jamii kujiendeleza kimasomo,” alisema Mkoba.

Vyama vyaunga mkono
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani (Tuico), Jones Majura, alisema wamesikitishwa na hatua ya Serikali kuandaa mswaada huo kimya kimya bila kuwashirikisha.

Katibu mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi na Nisharti (NUMET), Nicomemas Kajungu, alisema muswada huo unatawaumiza wafanyakazi wa migodi ambao wengi wao wanafanya kazi kwa mikataba. Alifafanua kuwa wanaomiliki migodi hutoa mikataba ya miaka michache, hivyo kuwepo kwa sheria hiyo kutawaumiza.

Naye Olenguruma aliwataka wabunge kuondoa itikadi zao za vyama na kuweka mbele maslahi ya wananchi kwa kuungana kwa ajili ya kupinga muswaada huo kwani haufai kabisa.

“Tunaaamini wabunge wataungana na sisi kuzuia muswaada huo na kama sauti zetu zitapuuzwa, wafanyakazi wanaweza kuchukua hatua mbalimbali kama vile kwenda mahakamani, kugoma na kujitoa kwenye mifuko ya kijamii.

“Waajiri pia wanaweza kusitisha kupeleka michango kwenye mifuko hiyo na kufunga akaunti za mafao hayo hadi usalama wa fedha za wafanyakazi utakapopatikana katika mifuko ya jamii hasa suala la fao la kujitoa,” alisema Olenguruma.

Fao jipya
Mapendekezo ya utekelezaji wa fao jipya la kukosa ajira yaliyo katika muswada huo, imeelezwa kuwa litatolewa kwa mfanyakazi aliyechangia zaidi ya miezi 18, ambaye atalipwa asilimia 30 ya mshahara wake wa mwisho baada ya kupoteza ajira.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, fao hilo litalipwa kwa mfanyakazi ambaye ameacha kazi kwa hiyari na ulipaji utafanyika kwa miezi sita mfululizo, kisha utasitishwa. Baada ya kusitishwa kwa fao hilo, imeelezwa kuwa mfanyakazi atasubiri kwa miaka mitatu na kama hatakuwa amepata ajira, mfanyakazi huyo ataruhusiwa kuhamisha michango yake kutoka katika mfuko wa lazima kwenda katika mfuko wa hiyari.

Mapendekezo yaliyo katika muswada huo kwa mujibu wa taarifa hiyo, yameeleza kuwa ni katika mfuko huo wa hiyari, ambako mfanyakazi atakuwa na hiyari ya kuchukua mafao hayo au kuendelea kuchangia.

Kwa mfanyakazi aliyeachishwa kazi, huku akiwa amechangia chini ya miezi 18, mapendekezo ni awe na haki ya kuchukua asilimia 50 ya michango yake, mara baada ya ajira yake kukoma.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment