Videos

Tanzania kufuta ujinga 2030



SERIKALI imesema itashirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kuhakikisha hadi mwaka 2030 inafuta ujinga nchini. Hayo yalisemwa na Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene katika maadhimisho ya Siku ya Usomaji Duniani.

Alisema moja ya malengo katika ilani ya CCM ni kuhakikisha kila mtoto nchini anapata elimu bure kuanzia darasa la kwaza hadi kidato cha nne.

“Nafahamu shirika lenu la Room to Read limekuwa likitumia mbinu mbalimbali katika kuendeleza elimu bora kwa kujenga maabara katika shule zetu, kutoa vitabu na mambo mbalimbali katika kupambana na elimu,” alisema.

Alisema takwimu za kitaifa za Sensa ya Makazi na Watu ya mwaka 2012 zinaoonesha asilimia 22 ya Watanzania haiwezi kusoma na kuandika kwa ufasaha.

Takwimu hizo zilionesha pia asilimia 81.7 wana elimu ya msingi na asilimia 14.4 elimu ya sekondari na asilimia 2.3 elimu ya chuo.

“Kwa mfumo unaofanywa na Room to Read katika kuhakikisha wanafunzi wanajua kusoma na kuandika wafikapo darasa la tatu ... tunapaswa kujifunza ili kuhakikisha ifikapo 2030 tunakuwa tumefanikiwa,” alisema.

Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo inasema ‘Kuandika Yaliyopita, Kusoma Yajayo’ itumike kutafakari kufuta ujinga.

Awali Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Room to Read, Peter Mwakambwale alisema siku ya usomaji duniani ni muhimu kwa wadau wa elimu wakiwemo wanafunzi wenyewe, wazazi, walimu, mashirika yasio ya kiserikali na serikali.

Alisema siku hiyo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Septemba 9, ikiwa ni kutimiza Azimio la Tehran lililopitishwa mwaka 1965 ambapo kwamwaka huu wanaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1966.

“Kutokana na kuwepo kwa mitihani ya taifa ya darasa la saba, sisi Room to Read na washiriki wenzetu tuliona ni vema kuadhimisha siku hiyo ili kupisha tukio muhimu la wadau wetu,” alisema.

Mwakambwale alisema takwimu za Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) za mwaka 2015 zinaonesha hali ya usomaji duniani katika nchi saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Tanzania ni ya pili kwa kuwa na kiwango kikubwa cha Watanzania wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa ufasaha kwa asilimia 80.3.

Alisema Burundi inaongoza katika nchi za ukanda huo kwa asilimia 85.6 ya wananchi wake kujua kusoma na kuandika.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment