Na Peter Kimath, Morogoro
ZAIDI ya sh. bilioni 1 zimetolewa na Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kunusuru kaya maskini 4,039.
Hayo yalisemwa na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Paschal Kihanga na kubainisha kuwa fedha hizo zilitolewa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Juni mwaka huu.
Akizungumza katika wa kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa manispaa hiyo, alisema kiasi hicho kilitolewa katika kaya hizo baada ya kukidhi vigezo.
Kihanga alisema katika kutekeleza maagizo ya Serikali ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia kaya maskini zisilipwe kwa kaya ambazo si maskini hivyo kaya 157 zilihakikiwa na kuondolewa katika mpango huo.
Hata hivyo, alisema bado kuna kaya ambazo zina vigezo vya kaya maskini ambazo zimetambuliwa na kuandikishwa na manispaa imepeleka maombi ya kufanya mchakato wa utambuzi wa nyongeza ili waweze kuingizwa katika mpango huo.
Meya alisema Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa halmashauri 161 zinazotekeleza Mpango wa TASAF awamu ya tatu kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini wenye malengo ya kuziwezesha kuongeza kipato.
Kwa upande mwingine, meya huyo alisema manispaa hiyo ilitoa mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana yenye jumla ya sh. milioni 100.
Alisema kwa vikundi vya wanawake 50 vilipatiwa mkopo wa sh. milioni 50 na vikundi 28 vya vijana vilipatiwa sh. milioni 50.
0 comments:
Post a Comment