Yusufu Makamba |
*Amtaka asisubiri nyumba kukamilika
*Yeye asema safari imeiva, anahamia
Na Mashaka Mgeta
KATIBU Mkuu mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hana sababu ya kubaki Dar es Salaam badala ya kuhamia Dodoma wakati huu.
Makamba aliyeshika nafasi hiyo kati ya mwaka 2007 na 2011, alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na JAMBO LEO nyumbani kwake, Tegeta, Dar es Salaam juzi.
Akizungumzia masuala ya siasa na utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, alisema uamuzi wa Rais John Magufuli kuhamishia Serikali Dodoma, ni sahihi na unapaswa kutekelezwa kwa kasi anayoihitaji.
Alisema wapo viongozi na watumishi wa umma wanaotumia kigezo cha ukosefu wa makazi na ofisi kutohamia Dodoma kwa wakati huu.
“Nilimsikia hata Waziri Mkuu akisema anasubiri nyumba ya kule juu imalizike ndipo ahamie Dodoma, pale (Dodoma) kuna makazi anayofikia hata sasa, kwa nini asiende kukaa humo mpaka hiyo nyumba itakapokamilika,” alisema Makamba.
Alisema Waziri Mkuu kama ilivyo kwa mawaziri wengine, wana makazi na ofisi ndogo za kufanyia shughuli zao hasa wanapokuwa mjini humo wakati wa mikutano na vikao vya Bunge.
Alihoji: “Kwani wanapokuwa Dodoma wanaishi wapi, wanafanyia wapi kazi zao, si wana ofisi ndogo …ninavyojua ni kwamba kila Waziri ana nyumba kule, mimi ninaijua ya mwanangu Januari,” alisema.
Januari Makamba ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano ambaye ni Mbunge wa Bumbuli kupitia CCM.
Makamba alitoa mfano, kwamba alipoteuliwa mara ya kwanza kuwa Katibu Tarafa, miaka ya mwanzoni mwa 1970, alikwenda kwa Waziri Mkuu wakati huo, Rashid Kawawa (marehemu) kudai kwamba hapana nyumba kwa ajili yao.
“Kawawa aliniambia, Makamba walimu wako huko wanaishi wapi, kuna watumishi wengi sasa ukiulizia suala la nyumba ya kuishi hata hiyo kazi utaikosa,” alisema na kuongeza:
“Sasa hawa viongozi na watumishi wajue kwamba Dodoma wapo waandishi wa habari, walimu, wanajeshi, polisi wakifanya kazi, kuhamia Dodoma kunatekelezwa kwa dhamira licha ya kuwapo changamoto hasa za miundombinu,” alisema.
Julai 23 Rais Magufuli alitangaza Serikali kuhamia Dodoma ili ifikapo mwaka 2020, mji huo ulio katikati ya nchi uwe Makao Makuu halisi ya nchi.
Majaliwa
Hata hivyo, akizungumza jana na watumishi wa ofisi yake walio Dar es Salaam Waziri Mkuu aliwataka kujiandaa kisaikolojia kwani safari ya Dodoma imeiva.
Hivi karibuni Waziri Mkuu alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa ifikapo Septemba atakuwa amehamia Dodoma.
“Mtambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao chimbuko lake ni agizo la Oktoba mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa TANU,” alisema Majaliwa na kuongeza:
“Tangu wakati huo kuna juhudi zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo."
Waziri Mkuu pia alitumia nafasi hiyo kuwatoa hofu watumishi hao na kuwahakikishia kuwa mambo yanakwenda vizuri na kuwataka wajiandae kuhama kwa awamu.
"Napenda kuwatoa hofu, mambo yanakwenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva, kikubwa ni kwamba tutakwenda kwa awamu kama ilivyopangwa,” alisema Waziri Mkuu.
Majaliwa aliwataka watumishi hao kuzingatia uamuzi wa Serikali akisema: "Pia tukumbuke kauli ya Rais kwenye hotuba yake ya Julai 23, alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, akairudia Julai 25, kwenye maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo nikaweka msisitizo."
Kupitia taarifa hiyo, pia aliwataka watumishi hao wazidishe mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana ya kutumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu.
"Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo.
0 comments:
Post a Comment