Abraham Ntambara na Hussein Ndubikile
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi ya Abiria (Taboa), kimeibua hoja mpya ya kupinga Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu nchini (Sumatra), kufungia kampuni za mabasi, pale moja ya mabasi yanapopata ajali, wakati wakijiandaa na mgomo wa mabasi nchi nzima.
Kabla ya hoja hiyo mpya, Taboa walikuwa wakipinga kutangazwa kwa siku moja ya ukaguzi wa magari nchi nzima, wakidai watalazimika kusitisha huduma mpaka ukaguzi wa mabasi yote utakapokamilika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu aliyesisitiza nia ya kugoma kesho kutwa bado ipo, alipinga Sumatra kufungia kampuni za mabasi kufanya safari zake, mara baada ya kutokea ajali ya basi moja.
“Kama gari moja linapata ajali halafu wanafungia kampuni nzima, wao ndiyo walianza kuvunja sheria kwa sababu sheria inasema unatakiwa kufungia gari moja tu lililopata ajali,” alidai Mrutu.
Mrutu alisisitiza kuwa kugoma au kutokugoma siku hiyo ya Jumatatu, itategemeana na maridhiano yatakayofikiwa katika kikao cha leo, kitakachofanyika Wizara ya Ujenzi, Mawasialiano na Uchukuzi kikiwakutanisha wao, Sumatra na Kikosi cha Usalama Barabarani.
Aliitahadharisha Serikali kuwa wasiwasikilize baadhi ya madereva ambao wamekuwa wakiwapigia simu na kusema kuwa Taboa hawawezi kufanya mgomo.
“Hao madereva wasiwasikilize, wao tumewaajiri tu na sisi ndio wenye umiliki wa magari na tunaweza kufanya hivyo ila tunaiheshimu tu Serikali,”alisema.
Aliongeza kuwa umefika wakati Serikali isimamie na kufuata sheria zilizotungwa na Bunge badala ya kusimamia sheria zinazotoka vichwani mwao.
Wakati Mrutu akisema hayo, Mkurugenzi wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisisitiza kuwa sheria za leseni za usafirishaji, zinaipa nguvu mamlaka hiyo kuifungia kampuni bila kujali kuwa ajali imesababishwa na dereva au ubovu wa magari.
“Sheria za leseni za usafirishaji zilizopo zinatupa mamalaka hasa tatizo linapogundulika madereva wasio na sifa wamechangia ajali za mabasi ya waajiri wao,“ alisema.
Alisema endapo itabainika kampuni imeaajiri madereva wasiotakiwa, Sumatra hutoa muda kwa kampuni kuwafanyia mafunzo na usaili tena ndipo yafunguliwe.
Alisisitiza pia Sumatra pia hufungia kampuni za mabasi itakapogundulika kuwa kampuni yenye mabasi zaidi ya sita, imeajiri meneja asiye na vigezo vya kufanya kazi hiyo.
Aliwaagiza wamiliki wote wa mabasi ya masafa marefu, kuzingatia masharti ya leseni ya usafirishaji kwa kuendelea kutoa huduma hiyo hadi utaratibu mwingine wa ukaguzi wa magari hayo utakapotolewa.
Ngewe alisema Sumatra iko katika mchakato na Jeshi la Polisi wa kuweka utaratibu mzuri wa kutekeleza ukaguzi wa mabasi, ambao awali ulipangwa kufanyika Jumatatu kabla ya kuibuka kwa tishio hilo la mgomo.
Aliwataka wananchi kuondoa hofu ya habari zinazosambazwa na vyombo vya habari ya kuwepo kwa mgomo wa mabasi Agosti 22 mwaka huu, na kufafanua kuwa mamlaka hiyo inafuatilia jambo hilo kuhakikisha huduma ya usafiri inakuwepo wakati wote.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, ameionya Taboa kuwa wakigoma watakuwa wemeenda kinyume na sheria ya leseni waliyopewa na Sumatra.
“Wakigoma watakuwa wanaenda kinyume na watapatwa na madhara makubwa… sitarajii kama watafanya hivyo,”alisema Mpinga alipozungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio jana Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment