Hayati Aboud Jumbe Mwinyi |
Na Suleiman Msuya
ALIYEKUWA Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Makamu wa Kwanza wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi (pichani) amefariki dunia jana nyumbani kwake Mjimwema, jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kifo cha Jumbe zilianza kuzagaa jana mchna kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari kisha Ikulu kutoa taarifa ikimnukuu Rais John Magufuli kutoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Mustafa, Jumbe alifariki dunia saa 7 mchana jana na anatarajiwa kuzikwa leo visiwani Zanzibar.
Marehemu Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania kuanzia Mwaka 1972 akichukua nafasi ya hayati Sheikh Abeid Amani Karume aliyeuawa, hadi 1984 alilazimishwa kujiuzulu madaraka kufuatia kutokea kwa kilichoelezwa ni machafuko ya hali ya hewa Zanzibar.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Magufuli alisema: "Nimeshtushwa sana na kifo cha Mzee wetu Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake alitoa mchango mkubwa wa kupigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo."
Aliongeza: "Napenda kuwapa pole familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki wote, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa jumla kwa kufikwa na msiba huo mkubwa" Rais Magufuli alisema Taifa limempoteza mtu muhimu aliyejitoa kupigania uhuru, umoja, haki na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilipitia.
Aboud Jumbe Mwinyi, alizaliwa Juni 14 mwaka 1920 na amefariki Agosti 14 mwaka huu akiwa na miaka 96. Enzi za uhai wake, mbali na urais wa Zanzibar na uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Jumbe aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia kiongozi wa Chama cha Afro Shiraz (ASP) kabla ya kuungana na Tanu na kuzaliwa CCM.
Aidha Jumbe anatajwa kutoa mchango mkubwa wakati vyama vya Tanu na ASP vilipoungana mwaka 1977 kwa kuridhia muungano huo. Mwaka 1979, Jumbe alikuwa mwanzilishi wa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kwa mara ya kwanza ambayo ilisababisha kutenganishwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi.
Mapema mwaka 1984 Jumbe alienguliwa kwenye nyadhifa zote hizo kwa kile kilichodaiwa kuchafua hali ya kisiasa Zanzibar.
Jumbe pia ndiye aliyeanzisha mfumo wa uwakilishi baada ya kufutwa, kufuatia Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyouondoa utawala wa Sultani.
Taarifa zinaonesha kuwaJanuari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, iliyoketi mjini Dodoma kwa dharura, ilimvua Jumbe nafasi zote za uongozi, ikidaiwa alihoji muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mazrui
Akimzungumzia marehemu Jumbe Naibu Katibu Mkuu waChama cha Wananchi (CUF), Nassor Mazrui alisema Wazanzibar wamepata pigo kubwa ambalo hawawezi kulisahau. Mazrui alisema Jumbe alikuwa msomi wa kwanza kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar hali iliyochangia awe na mitazamo chanya kwa nchi yake.
"Kwa kizazi cha sasa hamuwezi kuwa na kumbukumbu ila huyo Jumbe ni msomi wa kwanza katika kipindi cha Mapinduzi lakini alikutana na changamoto nyingi hali ambayo watu wamebakia kumsoma katika vyombo vya habari pekee," alisema.
Mbowe
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kiongozi huyo ni moja ya vielelezo visivyo na mfano katika nchi kwa kile alichodai kuwa alitengwa na Serikali na CCM kwa misimamo na ukweli ambao aliamini.
"Mimi namkumbuka kama kiongozi ambaye alisimamia misimamo yake bila woga hivyo kwa viongozi ambao hawakupenda ukweli, waliamua kumtenga na jamii," alisema. Mbowe alisema kiongozi huyo kwa mchango wake alioutoa katika Taifa hasa Zanzibar alipaswa kuenziwa ili vizazi vya sasa viweze kumtambua na kumuenzi.
Ligora
Katibu wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni mstaafu Mohamed Ligora alisema kifo cha Jumbe ni msiba mzito kwa jamii ya Tanzania na kuwa Jumbe alikuwa mtumishi mwadilifu na mwenye kujiamini. Alisema marehemu alikuwa mvumilivu na mwenye kunyamazia mambo hata kama yalikuwa linamkwaza jambo ambalo kwa sasa viongozi wengi hawana.
Ngayoga
Mtangazaji wa zamani wa Radio Tanzania(RTD), sasa TBC Taifa, Mohamed Ngayonga alisema anamkumbuka Mzee Jumbe kwa mengi huku akibainisha jambo kubwa alikuwa ni mtu mwenye msimamo, asiyeyumbishwa na kukubalika kwa Wazanzibar.
0 comments:
Post a Comment