Videos

Siri JPM kukutana na Lowassa yatajwa


WASOMI na wanasiasa wameeleza siri ya Rais John Magufuli kukutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, huku baadhi wakibainisha kuwa kitendo hicho kinaweza kufungua njia ya mwafaka kati ya Serikali na chama hicho cha upinzani kilichotangaza kufanya maandamano yaliyopewa jina la Ukuta.

Lowassa alikutana na Rais Magufuli juzi katika hafla ya Jubilei ya  ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na mkewe Anna, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Peter jijini Dar es Salaam.

Wawili hao walipeana mikono kwa mara ya kwanza tangu kampeni na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka jana, jambo ambalo Magufuli alilitafsiri kama muujiza akieleza hawakuwahi kukutana wa kampeni ambazo alikiri zilikuwa na ushindani mkali.

Magufuli alipewa nafasi ya kuzungumza katika hafla hiyo ambapo alisema: "Nimepata muujiza wa tofauti leo kwasababu nimeshikana mkono na Mheshimiwa Lowassa,tumezunguka kampeni zote sikuwahi kukutana naye,miujiza ya ndoa yenu imekuwa ni miujiza pia kwetu wanasiasa ambao nikiri kweli tulikuwa na ushindani mkali."

Aliongeza kuwa Mkapa na Mkewe ni madhebu tofauti, Katoliki na  Lutheran, lakini wameishi miaka 50 na kwamba ana uhakika wataishi miaka yote iliyobaki .

Tukio la hilo la Dk Magufuli na Lowassa limezua hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa kisiasa na wasomi huku likitafsiriwa kama njia ya kupata suluhu kwa mvutano kuhusu kufanyika au kutofanyika kwa maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta) operesheni iliyoasisiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Chadema imepanga kufanya maandamano na mikutano na maandamano yasiyo na kikomo Septemba mosi, huku Serikali ikisisitiza kutofanyika kwa maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wasomi waliozungumza na JAMBO LEO walitaka tukio hilo lisaidie kuwakutanisha Chadema na Rais Magufuli katika meza ya mazungumzo kumaliza mvutano uliopo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema ingawa anatofautisha tukio la Ukuta na kukutana kwa Dk. Magufuli na Lowassa, lakini linaweza kutumika kama njia kuzikutanisha pande hizo katika meza ya mazungumzo kwani viongozi hao wameonyesha ukomavu.

"Rais Magufuli na Lowassa wameonyesha ukomavu wa kisiasa na utanzania wao bila kujali itikadi za vyama, wameonyesgha kuwa pamoja na tofauti zao wanaweza
kukaa, kula, kusalimiana pamoja," alisema Profesa Mkumbo.

Alisema kukutana kwao ni mwanya wa mazungumzo, ingawa Lowassa si kiongozi wa juu wa Chadema bali ni mtu anayekubalika na watu wengi katika jamii ndani na nje ya chama chake hivyo anaweza kusaidia kupata muafaka wa Ukuta katika meza ya mazungumzo.

"Waliochokifanya Magufuli na Lowassa ndio utanzania ambao sisi tunao, Lowassa ni mtu anayekubalika watu wengi wanalitambua hilo hivyo kukutana kwake na Magufuli jana (juzi) kutafungua njia ya mazungumzo ambayo inaweza kuridhiwa na wafuasi wa Chadema na hatimaye Ukuta usifanyike,"alisema Profesa Mkumbo.

Alisema alichokifanya Lowassa ‘kimemvua nguo’ Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye hivi karibuni alikataa kumpa mkono hasimu wake kisiasa Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein walipokutana kwenye msiba wa Rais Mstaafu wa Awamu wa Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi.

Kwa upande wake Mhandiri wa Chuo cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wanahofia siku hiyo ya Ukuta kwa jinsi hali ilivyokuwa,alitamani Magufuli awaite Chadema wazungumze ili suala hilo lisitokee.

"Sijawahi kutishwa na masuala ya kisiasa, lakini hili la Ukuta nilihofia. Nilikuwa namwomba Mungu Rais Magufili aone haja ya kuzungumza na Chadema ili suala hili lipate suluhu, ndicho kilichotokea kukutana kwao jana (juzi), kumenipa moyo kwamba mambo haya yatakwisha," alisema Shumbusho

Alisema kutokana na kukutana kwa wawili hao, haoni kama maandamano ya Ukuta yatatokea, bali viongozi watakaa meza moja na kuzungumza.

"Kukutana na wawili hawa na hotuba ya Rais Magufuli kumetoa mwanga tayari kwamba Ukuta hautakuwepo, haijalishi kama watakutana kwa siri au kwa uwazi,  tunachoshukuru ni kwamba kile tulichokuwa tunakiona ni kama kimetulia ghafla, jambo ambalo ni la kushukuru," alisema Profesa Shumbusho.

Naye Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema viongozi hao wameonyesha ukomavu wa kisiasa na wamewatoa hofu wananchi kuhusu hali ilivyokuwa ikiendelea nchini na wameona viongozi wao wanaweza kukaa pamoja na kuzungumza hata kama wana itikadi tofauti.

"Nasaha inaonyesha kuwa Ukuta mwisho wake ilikuwa jana (juzi) siasa sio uadui, nafasi waliyopata wanaweza kuitumia kuzungumza na kuachana na Ukuta ili kazi ziendelee kutokana na kuwa Magufuli anakubalika maeneo mengi ya nchi kwa kazi alizofanya, nipo mikoani wananchi wanamuunga mkono kuliko hiyo operesheni,'' alisema.

Alieleza kuwa kitendo alichokifanya Lowassa kinamfunza Maalim Seif na kumkumbusha kwamba hakufanya sahihi alipokataa kusalimiana na Dk Shein kwani siasa sio uadui,kuna mambo mengine watu wanaweza kufanya pamoja hata kama ni vyama tofauti.

Kwa upande wa Profesa Joseph Semboja alieleza kufurahishwa na viongozi hao akisema kimeuonyesha ulimwengu kwamba Watanzania ni watu wenye  amani na upendo.

“Hatua hiyo imeonyesha Watanzania wanaweza kuwa na tofauti zao kiitikadi, lakini wakaendelea kuishi pamoja na kushirikiana kwa maendeleo yao katika mambo mbalimbali ya kijamii,” alisema Profesa Semboja.


Kwa mujibu wa msomi huyo, Lowassa na Rais Magufuli  wameonyesha ni lazima wakae pamoja kwa ajili kushughulikia mambo muhimu ya maendeleo ya wananchi, badala kuendeleza tofauti zisizo na manufaa kwa Watanzania.

“Ipo haja ya kwenda zaidi ya hapo, waweke utaratibu kwa mustakabali wa taifa wakae pamoja na kujadiliana kuondoa migogoro kwa afya ya Taifa,” alisema.

Profesa alisema sio sahihi kutumia mfumo wa jino kwa jino kwani utaratibu huo ndio unaoweza kusababisha kukua zaidi kwa migogoro na wakati mwingine unasababisha umaskini kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwani muda mwingi wananchi hawana muda wa kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa sababu ya migogoro.

Kwa upande wake, Profesa Samwel Wangwe alisema hatua ya viongozi hao kukutana na kupeana mikono ni ishara kwamba Watanzania wajifunze kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa katika kuleta muafaka mgogoro wowote kuliko kutunishiana misuli.

Alisema kuwa mazungumzo yana nguvu kubwa katika kultea upatanishi katika migogoro mbalimbali inatokea katika jamii kuliko kutumia njia nyingine ambazo zinaweza kusababisha vurugu na uharibifu wa mali za watu na upotevu wa maisha ya watu.

Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema ni jambo jema kwa viongozi kukaa pamoja kwa sababu giyo mambo mengine yanaweza kwenda mbele.

“Wote wanajenga nyumba moja, Rais Magufuli na Lowassa wameonyesha ukomavu wa kisiasa na mambo mengine yanaweza kwenda mbele,” alisema Sendeka.

Alisema anaamini sasa Lowassa ameshaelewa kwamba anapogombania nafasi moja ni lazima mmoja apate na mwingine akose hivyo kukutana kwao na kupeana mkono ni ishara nzuri na busara zinazopaswa kuigwa.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment