Videos

Hakuna utabiri wa tetemeko la ardhi


William Shao

KUKIWA na majonzi yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera na kusababisha vifo na uharibifu wa mali, kitabu cha The WorldBook Encyclopedia kinasema “matetemeko ya ardhi ni mojawapo ya matukio yanayosababisha uharibifu mkubwa zaidi duniani.”

Utafiti mwingine unadai kuwa nishati ya tetemeko kubwa la ardhi inaweza kuwa mara 10,000 zaidi ya bomu la kwanza la nyuklia.

Jambo hilo linaogopesha zaidi kwa kuwa tetemeko linaweza kutokea katika tabia yoyote ya nchi, msimu wowote, na saa yoyote na mahali popote. Ingawa wanasayansi wanaweza kufahamu kwa kiasi fulani mahali ambapo tetemeko lenye nguvu litatokea, hawawezi kutabiri litatokea lini.

Ijumaa ya Machi 11, 2011, nchi ya Japan iliathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 9.0 kwenye kipimo cha Richter.

Tetemeko hilo lilisababisha Tsunami (mawimbi makakubwa ya baharini yaliyosababishwa na tetemeko) yaliyosababisha madhara makubwa. Ni bahati tu kuwa tetemeko kubwa la mfano huo ni nadra kutokea. Utabiri wa kutokea kwa tetemeko la ardhi kwa usahihi ungeweza kuokoa maisha ya watu wengi.

Hata hivyo, uwezekano wa kujua kutokea kwa tetemeko la ardhi baadaye kunaweza kutabiriwa kwa kutumia takwimu za kisayansi.

Ni jambo jema kujua kama matetemeko ya ardhi yanaweza kutabiriwa ili wakazi wa maeneo yanayoathiriwa waweze kujiandaa. Ni jambo jema zaidi ikiwa utabiri huo unaweza kutaja mahali na wakati. Watafiti katika Jumuia ya Jiolojia nchini Marekani (USGS), wanaamini kwamba huenda ukafika wakati wakaweza kutabiri matetemeko ya ardhi kwa asilimia 67.

Pamoja na kuwapo kwa jitihada nyingi za kisayansi za kutafuta njia ya kutabiri kutokea kwa matetemeko hayo, bado wanasayansi hao hawajaweza kugundua ishara ya kutokea kwa hali hiyo, na wanakiri kuwa hakuna ishara ya wazi inayoweza kuonesha kuwa kuna tetemeko litakalotokea karibuni. Mtikisiko unaweza kugunduliwa muda mfupi kabla ya tetemeko kutokea, lakini hiyo haitoi muda wa kutosha wa watu kujiandaa.

Matetemeko ya ardhi hutokea kwa sababu ya kusonga kwa miamba mikubwa ambayo iko chini ya uso wa dunia. Miamba hiyo husonga daima.

Mara nyingi, mawimbi ya tetemeko la ardhi ambayo hutokea huwa dhaifu kiasi kwamba hayawezi kutambuliwa waziwazi kwenye uso wa dunia, lakini yanaweza kutambuliwa na kurekodiwa na kipima tetemeko. Nyakati nyingine, miamba mingi huvunjika na kusongasonga kiasi cha kutetemesha ardhi.

Wanasayansi wa USGS na mashirika mengine ya utafiti wako katika jitihada kubwa ya kuendeleza mbinu zitakazowasaidia kutabiri tetemeko la ardhi. Ingawa hadi sasa utabiri huo umekuwa mgumu, watafiti hao wana matumaini kuwa hatimaye watagundua ili kuokoa maisha ya watu wanaouawa kutokana na tetemeko.

Kwanini kipimo cha Richter? Tetemeko la ardhi linaweza kupimwa kulingana na ukubwa au kiwango chake. Katika miaka ya 1930, Charles Richter alibuni kipimo cha kuonesha ukubwa wa tetemeko la ardhi.

Wakati vituo vya kupima tetemeko la ardhi vilipoongezeka, vipimo vipya vilibuniwa kwa kutumia uvumbuzi wa Richter. Mfano, kipimo cha nguvu za tetemeko la ardhi huonesha kiasi cha nishati kilichosababishwa na chanzo cha tetemeko la ardhi. Vyovyote iwavyo, bado watafiti hawajagundua mbinu ya kutabiri tetemeko la ardhi kabla halijatokea.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment