TETEMEKO la Ardhi lililotokea juzi katika mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara na kusababisha vifo na majeruhi, lina uhusiano na tukio la kupatwa kwa jua lililotokea Septemba Mosi mwaka huu, JAMBO LEO limeelezwa.
Hayo yalielezwa jana na wataalamu wa miamba waliozungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kuhusu tukio hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augostino Olomi alisema kuwa hadi jana tukio hilo limethibitika kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 170.
Kati yao majeruhi 83 wamepata matibabu na kuruhusiwa kutoka hospitali.
Wataalamu hao kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walieleza kuwa kupatwa kwa jua kunaongeza nguvu ya kuzalisha tetemeko la ardhi, hasa kama tetemeko hilo lilikuwa linakaribia kutokea.
Ingawa watalaamu hao hawakueleza kwa hakika tofauti ya muda inayohitajika ili tukio moja liathiri lingine, tetemeko hilo la ardhi limetokea siku kumi tangu Jua lipatwe katika ardhi ya Tanzania eneo la Rujewa wilayani Wanging’ombe katika mkoa wa Njombe.
Walichosema
Mhadhiri wa chuo hicho, Dk Richard Wambura alisema kuwa ni dhahiri kwamba kupatwa kwa jua kuna uhusiano na tetemeko la ardhi.
“Kupatwa kwa jua kunapunguza mvuto wa dunia kwenye jua, kupunguza nguvu kunadisturb (sumbua) lakini haitoshi kuzalisha tetemeko, ila inaweza kuchangia endapo lilikuwa (tetemeko) karibu kuzalishwa na likawa halina nguvu,” alisema Dk Wambura.
Alisema kupatwa kwa jua kunaweza kuongeza nguvu na kusababisha tetemeko la ardhi, kwani tukio hilo linachangia msuguano wa miamba ambayo muda wote inakuwa inatembea.
“Tukio hilo sasa linatengeneza sura ya Bonde la Ufa,” alisema. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, uwepo wa mwezi katikati ya jua na dunia, husababisha umbo la dunia kubadilika kutokana na kukosa mvutano wa moja kwa moja kwa sababu dunia huwa imekandamizwa na hivyo kuzalisha vipande vilivyoungana.
“Vipande hivyo vikibonyezwa husababisha msuguano ambao huzalisha tetemeko la ardhi.
Katika tukio la kupatwa kwa jua, mwezi hukaa katikati ya dunia na jua, hivyo mvutano wa moja kwa moja wa dunia na jua hupunguzwa na uwepo wa mwezi katikati ya sayari hizo,” alisema. Alisema kupatwa kwa jua hakusababisha moja kwa moja kutokea tetemeko la ardhi, isipokuwa linachangia kulifanya tetemeko lililotaka kutokea litokee kabla ya muda wake.
“Mfano, kama tetemeko la ardhi lilipaswa kutokea miaka mitano au miwili, kupatwa kwa jua kunaweza kusogeza tukio hilo na kulifanya litokee kabla ya muda huo,” alisema Dk Wambura. Aliaongeza ‘’Japokuwa uhusiano wa kupatwa kwa jua na tetemeko la ardhi una mchan- go mdogo, moja likitokea linaweza kuathiri lingine,” alisema.
Alisema katika tetemeko la Kagera, Kuna ufa unaopita kutokea Ziwa Victoria, Bonde la Magharibi Rwanda, Kigoma na Nyasa ambao umezidiwa nguvu inayojikusanya kwa miaka mingi, ndiyo uliosababisha tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa Ritcher 5.9 .
Historia ya matetemeko ya ardhi nchini
Dk Wambura alisema tetemeko lingine kubwa la ardhi liliwahi kutokea eneo la Karema katika ukanda wa Ziwa Tanganyika upande wa Bonde la Ufa. Tetemeko hilo lilitokea mwaka 1910 likiwa na ukubwa wa ritcher 7.4.
Alisema mwaka 2005 tetemeko lingine lenye ukubwa wa ritcher 6.8 lilitokea Ziwa Tanganyika eneo la Karema na Karemee ambayo ipo upande wa Kongo.
Alisema ukanda wenye Bonde la Ufa mara kadhaa hurudiwa na tetemeko la ardhi kwani muda wote miamba inakuwa inakusanya nguvu ambayo inasukuma hiyo miamba na kusababisha tetemeko la ardhi.
Dk Wambura alifafanua kuwa dunia kama ilivyo sayari zingine, zilizo hai kuna miamba migumu juu yake na ndani ipo miamba laini ambayo inaleta volcano.
Alisema matetemeko ya ardhi yameendelea kutokea maeneo mengi ya nchi, lakini kwa kuwa hayakuleta madhara makubwa hayakufahamika.
Alieleza kuwa mwaka 2009 lilitokea tetemeko lingine katika maeneo ya Ziwa Natron. Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa ritcher 5.9 na mwaka 2008 kulitokea tetemeko la ardhi mkoani Morogoro. Mwaka huu limetokea tetemeko linguine mkoani Dodoma.
Naye David Kahumbi, alisema ikiwa tetemeko la ardhi lilipaswa kutokea lakini likawa halina nguvu, kupatwa kwa jua kunaweza kuchangia.
Alisema historia inaonyesha tetemeko kubwa zaidi ya hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa ritcher 7.2 lilitokea Julai 1919 katika Ziwa Tanganyika.
“Tetemeko lingine lilitokea Mwaka 2005 huko huko Kigoma katika Ziwa Tanganyika. Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa Ritcher 6.8. Pia mwaka 2007 kulitokea tetemeko lingine katika mkoa wa Arusha na Mashariki ya Bukoba nalo lilikuwa na ukubwa wa Ritcher 6.0’’ alisema.
0 comments:
Post a Comment