Videos

Muswada Fao la Kujitoa wazua balaa



VYAMA vya Wafanyakazi na Asasi za Kiraia Nchini, vimetaka wabunge kukataa mjadala wa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii unaotarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni, usisomwe hadi Serikali irejeshe kipengele cha fao la kujitoa.

Hayo yamo kwenye tamko lililotolewa jana kwa vyombo vya habari na likiwa limesainiwa na jumuiya za wafanyakazi zikiwamo NUMET, TUCTA, RAAWU, TUIKO, CWT, CHODAWU na Mitandao ya Asasi za Kiraia Tanzania chini ya Mwavuli wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Muungano huo ulisikitishwa na lengo la Serikali kutaka kuondoa utaratibu wa Fao la Kujitoa kupitia Muswada huo.

“Tunawasihi wabunge kama wawakilishi wetu, na wao kama waathirika wa mabadiliko haya, kusitisha majadlilano ya Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii unaotarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza kwenye vikao vinavyoendelea vya Bunge la Nne, usisomwe hadi Serikali irejeshe kipengele cha fao la kujitoa,” lilieleza.

Muungano huo ulizitaka jumuiya hizo kutumia muda kutetea maslahi ya wafanyakazi wao, kwani kutofanya hivyo kunaweza kuleta tafsiri mbaya ya kuwepo kwa jumuiya hizo.

“Watanzania wote wapaze sauti kuukataa Muswada huu, kwani unakwenda kuminya haki za Watanzania wengi wanaofanya kazi kwa jasho lao katika maeneo mbalimbali,” taarifa hiyo ilisema.

Iliongeza kuwa mchakato huo wa kubadilisha Sheria za Mafao ulipaswa kuwa shirikishi kwa kuhusisha wenye mifuko hiyo- wafanyakazi-kupitia vyama na vikundi vyao vinavyotambuliwa kisheria.

"Kinachoshangaza ni usiri mkubwa katika hili hasa lengo la kutaka kupeleka Muswada huo kwa hati ya dharura bila ushiriki wa wadau," lilisema tamko hilo.

Lilieleza kuwa pamoja na changamoto nyingi kwenye Muswada huo, lakini haki ya fao la kujitoa kwa mfanyakazi anayeacha kazi kabla ya muda wa kustaafu iko pale pale.

Lilisema Watanzania wafanyakazi hasa katika maeneo yasiyokuwa na ajira za kudumu kama migodini, viwandani, mashambani na kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali (AZAKI) wanastahili kupata fao la kujitoa.

Tamko hilo liliongeza kuwa ni haki ya wafanyakazi kudai fao la kujitoa kutokana na kuwa ajira katika sekta binafisi si za kudumu, ni za mikataba ya muda mfupi, wanafunzi wengi wanapomaliza shule au vyuo hupenda kufanya kazi kwa muda na baadaye kutumia fao la kujitoa kujiendeleza kielimu.

Vyama hivyo viliitaka Serikali itoe tamko mara moja la kuruhusu mafao hayo kutolewa kwa wafanyakazi ambao hawako kazini kwa sasa, kuishauri Serikali kuacha utaratibu uliokuwapo uendelee, kwa maana kwamba, mfanyakazi awe na hiari ya kuchukua mafao yake au kusubiri kustaafu badala ya kuwawekea vikwazo kwenye pesa zao.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment