Wakazi hao wameilalamikia Serikali kwamba haikuwashirikisha katika hatua hiyo inayolenga kupisha mradi wa uchimbaji madini ya graphite unaoendeshwa na Kampuni ya TanGraphite, chini ya kampuni tanzu ya Kibaran Resources ya nchini Australia.
Wakazi hao waliliambia gazeti hili kuwa tangu mradi huo uanze mwaka 2012 na wao kutakiwa kuhama maeneo yao hayo ya asili, kumeibuka sintofahamu kubwa, huku mambo mengi yakiamuliwa bila wao kupewa fursa ya kushiriki. Walisema kumekuwa na matumizi ya nguvu hasa kwa wananchi wanaonekana kuhoji. Watu wanatishwa na wengine wanakamatwa na polisi, jambo ambalo linawafanya wakose amani, alisema mmoja wa wakazi hao ambaye hakutaka kutajwa kwa hofu ya kukamatwa kama ilivyotokea kwa wenzake kadhaa.
“Awali tulipopewa taarifa ya kuhama ili tupishe mradi, tulihoji mambo kadhaa, lakini inaonekana kwamba Kampuni hii ya TanGraphite ilishaanza kazi, hivyo wakatupuuza. Kuanzia viongozi wa kijiji hadi mkoa hakuna aliyetusikiliza,” alisema.
Mwanakijiji huyo aliyeambatana na wenzake kadhaa kwenye ofisi za gazetili kuleta malalamiko hayo alisema, kimsingi wakazi hao hawapingi mradi, ila wanataka kushirikishwa ili wajue hatima yao. “Kampuni imeshaanza kazi na wanatutaka tuhame, lakini hawatwambii twende wapi na tunaenda vipi. Sasa haya ndiyo mambo tunayosema kuwa hayako vizuri tunahitaji kushirikishwa tujue hatima yetu,” alisema.
Mkazi huyo alibainisha kuwa tangu mradi huo uanze hawakuambiwa chochote, lakini baada ya kulalamika Kampuni ya Mtei ilifika kijiji hapo kwa ajili ya kufanya tathmini ya makazi yao, lakini hata hivyo bado kuna usiri unagubika.
Kauli ya Serikali
Alipotakiwa kuzungumza suala hilo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitaka aulizwe Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Waziri Muhongo alisema haamini kama wananchi hao wanaonewa kwani alituma watu mara nyingi ili waweze kuwasaidia kumaliza mgogoro huo.
“Ngoja nikwambie waambie hao wananchi washike Msahafu na Biblia waseme kama hawajawahi kushirikishwa na Serikali ya Mtaa na kusaidiwa katika suala hilo,”alisema.
Alisema vitengo mbalimbali Serikaliani ikiwamo, Kamishna wa Madini, mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa wamekuwa mstari wa mbele kuwasaidia wananchi kwa namna tofauti.
Waziri Muhongo akamtaka mwandishi wa habari hii kuwasiliana na mkuu wa wilaya ya Ulanga kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari ofisi yake ilishatoa maelekezo kwake kushughulikia suala hilo.
DC anena
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Jacob Kasemma alisema katika jitihada za kutatua mgogoro huo, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya TanzGraphite waliamua kujenga ofisi ambayo itasikiliza malalamiko na maoni ya wananchi hao lakini baadhi yao waliivamia na kuivunja.
“Kule ni kijijini, tuliamua kujenga ofisi maalumu kusikiliza kero, malalamiko na maoni na madukuduku ya wananchi kwa lengo zuri kabisa ili kuondoa tofauti zilizopo, lakini baadhi ya wananchi walivamia ofisi hiyo na kuivunjavunja, huku wakitishia usalama wa maofisa waliowekwa pale. Kumbe unaweza kuona kuwa suala hilo lina changamoto kubwa,” alisema.
Akizungumzia madai ya wananchi hao kwamab wamekuwa wakikamatwa na polisi, mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa suala hilo halipo isipokuwa wananchi wanachojaribu kufanya ni kuihadaa jamii kuhusu jambo hilo.
“Kuna wananchi walivamia sehemu vilipowekwa vifaa vya kampuni ya TanzGraphite kwa lengo la kufanya uharibifu. Sasa suala la uharibifu wa mali ni jinai, hivyo Polisi lazima wachukue hatua. Jambo mbaya sana linalofanywa na hao watu wachache ni kwamba waliwatumia wanafunzi, na baada ya hapo walizusha habari kwamba Polisi imepiga mabomu wanafunzi,” alisema. Alibainisha kuwa anafahamu uwepo wa watu wachache kupinga mradi huo, lakini bado anafanya juhudi za kukutana nao ili kujua msingi wa madai yao.
Mkuu wa Wilaya wa zamani
Awali, aliyekuwa mkuu wa wilaya hiyo kabla ya Kasemma Christine Mndeme alisema madai ya wananchi hao hayana msingi kwa kuwa hayaeleweki.
“Mradi huo ulipitia hatua zote. Tulianza na vikao vya kijiji, lakini mkutano wa kijiji watu hawakuhudhuria. Binafsi kama Mkuu wa Wilaya niliwaita wananchi hao mmoja mmoja niwasikilize, lakini hawakufika. Baadaye wakazusha kwamba nimewaita ili niwahonge pesa na wengine wakasema nimewaita ili niwakamate, hivyo hadi naondoka tumeshindwa kujua hoja yao ni nini,’ alisema.
Mwekezaji anasemaje?
Mkurugenzi Mtendani wa Kampuni ya TanGraphite, Grant Pierce alisema hakuna sababu yoyote ya wananchi hao kuwa na wasiwasi juu ya mradi huo kwa kuwa mchakato wake bado unaendelea.
“Ni kweli hadi sasa hakuna mwananchi anayejua atahamia wapi kwa sababu kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa, Wilaya na Serikali ya kijiji tupo katika mchakato wa kutafuta maeneo ambayo tutawajengea makazi wananchi hao. Tumeunda kamati yenye wawakilishi wanne kutoka vitongoji sita vya kijiji hicho kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo,” alisema.
Mradi ukoje?
Mradi wa uchimbaji madini ya graphite, ulianza mwaka 2012 kwa kampuni ya TanzGraphite kuanza kufanya utafiti. Mradi huo utadumu kwa miaka 27 na utahusisha vitongoji vitatu katika kijiji cha Epanko. Wakati wa kitongoji cha Epanko A na Kazimoto watahamishwa kupisha mradi huo. Pia nusu ya wakazi wa Kitongoji cha Itatira watatakiwa kuhama. Mradi huo hautagusa vitongoji vingine viashughuli za uchumbaji wa madini hayo huku nusu ya kitongoji cha Itatira ikiguswa. Vitongoji vingine vitatu vya Epanko B Mbera na Lurina havitaguswa kabisa.
0 comments:
Post a Comment