Rais John Magufuli |
Kwa mujibu wa Serikali, kati ya fedha hizo Sh trilioni 51, deni la Serikali lilikuwa dola bilioni 20.5 (Sh trilioni 42.9) huku la sekta binafsi likiwa dola bilioni 2.7(Sh trilioni 8.1).
Kwa maelezo ya Mbowe ina maana Watanzania takriban milioni 50 wakiwamo watumishi wa umma, sekta binafsi, wasio na kazi, wastaafu, vikongwe, wanafunzi hata vichanga, kila mmoja anabeba mzigo huo wa deni la Taifa kwa kiasi cha Sh milioni 1.3.
Maelezo hayo yalitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ambaye aliitaka Serikali ieleze deni lake ni kiasi gani na ina mikakati gani ya kukabiliana nalo.
Baada ya swali la Kubenea, Mbowe aliinuka na kuuliza swali la nyongeza ambapo alifafanua kiasi anachodaiwa kila Mtanzania, hali iliyomwinua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ambaye alisema deni hilo haliwezi kupimwa kwa utaratibu huo.
Katika swali la msingi, Kubenea alisema Serikali ya awamu iliyopita ilikopa fedha kwenye benki za nje na za kibiashara; mwaka 2011 ilikopa Sh trilioni 15 na kufanya deni kufikia Sh trilioni 21 kabla ya mwaka 2015, kwamba ilikopa tena Sh trilioni 9 na kulifanya deni kufikia Sh trilioni 39.
Akijibu swali hilo, Dk Kijaji alisema deni la Serikali lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo, ukiwamo wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga.
Miradi mingine ni mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafirisha gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.
Akieleza mikakati ya Serikali alisema ni pamoja na kuongeza ukusanyaji mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa miradi yenye kuchochea haraka ukuaji wa pato la Taifa.
Aidha, kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa makandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu.
Dk Kijaji alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/11 Serikali ilipokea mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara Sh trilioni 1.3 na mwaka 2014/15 ilipokea mkopo wa Sh trilioni 2.3 na kwamba mikopo hiyo haikufikia Sh trilioni 15 trilioni mwaka 2011 na Sh trilioni 9 kabla ya mwaka jana.
Katika swali la nyongeza, Mbowe alisema deni hilo ni mara mbili ya bajeti ya Serikali na kwamba kila wananchi milioni 45 wa Tanzania, kila mmoja anadaiwa Sh milioni 1.2.
“Ni kweli kukopa ni muhimu, lakini tunapaswa kukopa kwa kujidhibiti kwa kile ambacho tunaweza kulipa na kwa wakati, kwa nini Serikali isione uwezekano wa kurudishwa katika mpango wa kusamehewa madeni kama ilivyokuwa nyakati za Mkapa (Benjamin-Rais wa Awamu ya Tatu)?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Dk Kijaji alisema Serikali bado haijaondolewa kwenye mpango wa kusamehewa madeni isipokuwa nchi zilizokuwa zinatoa msamaha huo, zilisitisha mpango huo kutokana na kukumbwa na migogoro, zikiwamo Iraq na Iran.
Alisema bado Serikali inaendelea na mchakato wa kushawishi wadau wa maendeleo ili kuisamehe Tanzania deni hilo.
Akiongezea majibu katika swali hilo, Mwigulu alikanusha kauli ya Mbowe kwamba hakuna utaratibu wa kupima deni la Taifa kwa kuangalia wingi wa watu.
“Kwanza naomba niseme kwamba hakuna siku watagongewa mlango wakidaiwa deni hilo la Taifa, na wala katika Taifa lolote hakuna utaratibu wa kupima deni kwa kuangalia ujazo wa watu, deni la Taifa linapimwa kufuatana na uwezo wa ukusanyaji mapato wa nchi husika,” alisema Mwigulu.
0 comments:
Post a Comment