Videos

Safari ya Dodoma‘yaingiwa mdudu’

SAFARI ya kuhamia Dodoma inaweza kuwa ‘imeingia mdudu’ wa kigugumizi baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kutofautiana kuhusu wizara zitakazohamia makao makuu hayo ya Serikali.

Agosti 25, Waziri Mhagama alitangaza kwamba sasa mkoa wa Dodoma uko tayari kupokea wizara kwa asilimia 70 na kwamba nyumba kwa ajili ya watumishi zipo kwa asilimia 75.

Hata hivyo, juzi Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa awamu ya kwanza kuhamia Dodoma ni mwezi huu hadi Februari mwakani, yeye akiongoza na kufuatiwa na mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na idara angalau moja.

Hali hiyo ilitajwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia, kuwa ni sawa na kigugumizi akieleza kwamba tangu awali alishaeleza safari ya kuhamia Dodoma haiwezi kuwapo bila mipangilio au bajeti.

Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, alisema Julai 25 Waziri Mkuu alitamka kuwa atahamia Dodoma Septemba mosi, jambo ambalo halikutekelezwa, badala yake yeye na mawaziri wengine waliojipambanua kutangulia kutoa visingizio kuwa kukwama kwao kulitokana na mkutano wa Bunge.

Mbatia alisema kwa kawaida jambo lolote linalotakiwa kufanywa lazima liwe na mpangilio na si kwa fujo tena kiubabaishaji.

Aliongeza kuwa Waziri Mkuu alipaswa kutambua kwamba akitoa kauli inakuwa nzito kwa watu wanaosikiliza, hivyo ni muhimu ajipange kabla ya kutoa tamko.

Majaliwa

Juzi wakati anazungumza kwenye kipindi cha Safari ya Kuhamia Dodoma kilichoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Waziri Mkuu Majaliwa alisema mchakato wa kuhamia Dodoma utafanyika kwa awamu sita.

Alisema awamu ya kwanza itaanza mwezi huu hadi Februari mwakani, ikiongozwa na yeye, mawaziri wote, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu na idara angalau moja.

Aliongeza kuwa awamu ya pili itaanza Machi hadi Agosti mwakani, katika kipindi hicho makatibu wakuu watapendekeza na kuomba fedha bungeni kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa utaratibu wa Bunge, mikutano ya bajeti huanza Aprili hadi Julai ili kujadili na kuidhinisha mapato na matumizi ya Serikali ya mwaka mpya wa fedha.

Majaliwa alisema awamu ya tatu itaanza Septemba hadi Februari 2018 na zitaendelea zingine ya mwisho ikiwa ni mwaka 2020.

Mhagama

Akizungumza Dodoma baada ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhojiwa na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mhagama alisema kikosikazi kilichoundwa na Waziri Mkuu cha Mkoa wa Dodoma tayari kimewasilisha ripoti ya hali ya mazingira ilivyo.

“Kikosikazi cha Mkuu wa Mkoa kimefanya kazi nzuri, waliangalia miundombinu iliyopo hapa ipo kwa kiasai gani na tumegundua kuwa nafasi za ofisi za wizara zote zinaweza kupatikana kwa asilimia 70 hivi na nyumba za watumishi aslimia 75,” alisema.

Alisema barabara zote zitatengenezwa kwa ubora wa hali ya juu pia uwepo wa maji meta za ujazo milioni 16 ambazo hazifanyi kazi zinazotumika na umeme wa ziada wa megawati 23 ambazo pia hazitumiki na kilichobaki ni hatua ya Serikali yote kuhamia Dodoma.

Alisema wao ndani ya Serikali wamejipanga kuondoka kwa awamu, huku ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu ukiendelea na kilichobaki ni umeme na maji.

Kikubwa tumedhamiria na Waziri Mkuu alishasema mwanzoni mwa Septemba atahamia Dodoma. “Huko nyuma historia inaonesha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilishahamia huku na Ofisi ya Rais (Tamisemi) ipo huku, hivyo mimi ninayemsaidia Waziri Mkuu na manaibu wangu tayari tumehamia hapa,” alisema.

Alisema suala la kuhamia Dodoma bado lipo na uratibu unaendelea na watakuwa wanatoa taarifa kila baada ya muda kuwa ni kiongozi gani amehamia hasa baada ya Waziri mkuu kuingia Dodoma.

Aliongeza kuwa yapo majengo ya Serikali ambayo yanatumika kwa sasa yakiwamo ya Hazina na jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa linaendelea kukamilishwa pia kuna jengo jipya la Bodi ya Mfuko wa Barabara linaendelea kujengwa.

Alisema wanajiratibu ndani ya Serikali na kikubwa kwenye bajeti ya mwaka huu wanataka wahame kwa awamu ambayo haitaathiri bajeti ambayo ilishapitishwa na Bunge.

“Tutakuwa tunaangalia katika kila bajeti mazingira yakoje na yanawezaje kuturuhusu kuhama kwa awamu. Niwahakikishie Wa-tanzania, kuwa kilichopangwa kitapatikana kwa wakati kama ni barabara pia zitapatikana,” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment