* Watu binafsi, mashirika, kampuni, balozi wachangia
* Baadhi watoa fedha taslimu, vifaa, saruji, kujenga shule
KUGUSWA na tukio la tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi mkoani Kagera na uhamasishaji uliofanywa na Serikali, umewezesha misaada mingi kutolewa kwa waathirika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana kutokana na vyanzo mbalimbali watu, binafsi, kampuni, mashirika na ofisi mbalimbali zikiwamo balozi zinazowakilisha nchi zao nchini zimechangia zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Makundi hayo yalikutana jana Ikulu Dar es Salaam katika mkutano maalumu wa kuchangia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Wafanyabiashara hao kwa nyakati tofauti walitoa ahadi za kuisaidia Serikali huku Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi akiwasihi kwamba kundi hilo ndilo linalopaswa kuchangia kwa wingi kutokana na kuwa ni nchi yao.
"Tanzania inapaswa kusaidiwa na Watanzania wenyewe hivyo ni vema kila mmoja kwa nafasi yake asaidie katika hili," aliasa.
Balozi
Ubalozi wa China nchini ulitoa Sh milioni 100 na kupeleka madaktari, helikopta sita, chakula, mahema na madawati huku wa Japan ukiahidi kuangalia namna utakavyoweza kuchangia.
Umoja wa Mataifa (UN) uliahidi kusaidia kurejesha miundombinu mkoani humo.
Wafanyabiashara
Mohamed Dewji kupitia kampuni ya Mohamed Enterprises na Mo Foundation walitoa Sh milioni 100, Salum Turky, kupitia kampuni ya Muza Oil Mills aliahidi kutoa saruji mifuko 5,000 na mabati 3,000 huku Mengi akiahidi Sh milioni 110.
Kampuni ya Toyota ilitoa Sh milioni 10, Subash Patel kupitia kampuni zake aliahidi Sh milioni 150, Kamal Group Sh milioni 50 na Urban Group Sh milioni 20 kusaidia ujenzi wa miundombinu.
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) iliahidi Sh milioni 100, IPTL Sh milioni 50, Azania Group walitoa Sh milioni 20, Tanzania Agricultural Processing Zone Sh milioni 30 na Tacosoa Sh milioni 250.
Pia Group Six walitoa tani 80 za saruji, Kagera Sugar Sh milioni 100 na tani 10 za sukari, Jambo Plastics Sh milioni 20, mdau wa Bukoba Melisa Kataraiya Sh milioni 20.
Kampuni nyingine ni Tanga Cement mifuko 1,000 ya saruji, Pepsi Sh milioni 50, Kiwanda cha Bia cha Serengeti mifuko 800 ya saruji, JBP, OIL COM na MOIL watajenga shule mbili zilizoharibika kwa tetemeko hilo.
Pia kampuni ya Puma waliahidi Sh milioni 50, Agusta Tanzania Sh milioni 10, Kampuni ya Tipper Sh milioni 20 kusaidia ujenzi wa miundo mbinu, Camel Oil kupitia kampuni ya Camel Cement mifuko 1,000 ya saruji kusaidia ujenzi wa nyumba zilizoharibika.
Jumuiya ya Waislamu wa Madhehebu ya Imamu Shafi Sh milioni 100, Sahara Tanzania Sh milioni 20, Engen Petroleum Sh milioni 10.
Awali Majaliwa aliwashukuru wafanyabishara na mabalozi hao kwamba alikuwa anatafuta nafasi ya kukutana nao kikao cha pamoja, akisema nafasi hiyo bado ipo na mkutano huo wa jana ulikuwa maalumu kwa ajili ya kuchangia waathirika wa mafuriko.
Alisema Serikali imefungua akaunti CRDB namba 015225617300 yenye jina la Kamati ya Maafa Kagera, na hivi karibuni zitatangazwa namba za M Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money kwa wanaoweza kuchangia kwa njia hiyo.
Pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Aziz Mlima, alisema Jumamosi yatafanyika matembezi ya hisani ya yatakayoanzia Oysterbey Polisi hadi Masaki ili kuchangia Sh milioni 10 kwa ajili hiyo.
Naye Fidelis Butahe, anaripoti kutoka Dodoma kwamba wabunge wote bila kujali itikadi zao waliridhia kwa kauli moja kukatwa Sh 220,000 ya posho ya kikao cha jana ili kusaidia maafa hayo.
“Posho ya leo ya wabunge itachangia maafa ya wananchi wa Kagera. Wabunge tusimame kwa dakika moja kama ishara ya kuwakumbuka ndugu zetu walioathirika na kupoteza maisha katika maafa haya,” alisema Dk Tulia jana.
Wakati Serikali ikitoa taarifa bungeni jana kuhusu maafa hayo iliyosomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kwa niaba ya Waziri Mkuu, wabunge wa upinzani walisema kilichopaswa kuelezwa si nyumba na shule ngapi zimebomoka, bali misaada waliyopewa wananchi waliopata maafa mpaka sasa.
0 comments:
Post a Comment