Charles James |
NAITAZAMA nembo ya Taifa kabla ya kuandika Makala haya na kuvutiwa na maneno ya Uhuru ni Umoja yaliyowekwa kutokana na busara za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Umoja ambao Mwalimu Nyerere aliuasisi haukujali itikadi za kiimani, kisiasa ama aina yoyote ya ubaguzi. Aliliunganisha taifa ambalo licha ya tofauti mbalimbali za kijamii zilizokuwapo, watu wakawa wamoja katika utanzania wao.
Mwalimu Nyerere aliamini umoja ni njia pekee ya kuifanya Tanzania kupata maendeleo, na kwamba kama hakuna (umoja) kutakuwa na machafuko kama vita ambavyo kwa asili vinazibomoa jamii badala ya kuzijenga. Rwanda iliwahi kuingia kwenye machafuko ya kisiasa yaliyosababisha mauaji ya kimbari mwaka 1994, yakawahusisha watu wa kabila za Wahutu na Watutsi.
Vita kama hiyo, ingawa kwa matokeo yanayotofautiana imewahi kutokea kwa mataifa jirani ya Burundi na sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo (DRC).
Nchini Kenya, ubaguzi uliojikita katika misingi ya kikabila ukaibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007. Sehemu kubwa ubaguzi huo ulizihusisha jamii za Wakalenjin waliokuwa wanaungwa mkono na Waluo dhidi ya Wakikuyu.
Ni vurugu hizo ziliowafikisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Rais Uhuru Kenyetta na Makamu wake, William Ruto.
Wakati Kenyatta alishutumiwa, pamoja na mambo mengine, kusaidia kundi la Mungiki kuwaua Wakelenjing na Waluo, Ruto alihusishwa na mauaji yaliyofanywa na Wakelenjing dhidi ya Wakikuyu na Waluo.
Hiyo ni mifano michache inayothibitisha hatari inayozikabili jamii zinapoingia katika machafuko hasa yanayotokana na siasa.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa mataifa hayo, Tanzania ikabaki kuwa mfano wa kisiwa cha Amani katika Mashariki mwa Afrika na ukanda wa maziwa makuu. Umoja na ukarimu wa raia wake ukatumika kuwa mfano kwa nchi nyingine za Afrika hasa zilizokabiliwa na machafuko ya kisiasa.
Lakini hivi sasa hali ilivyo Tanzania ni kama ipo tenge. Tenzi za amani zimegeuzwa kupitia ndimi za viongozi na raia wa kawaida wanaotaja vurugu na machafuko kila wakati.
Machafuko na hatari za kuvurugika kwa amani zimekuwa kauli zilizo karibu, hivyo kutoka vinywani mwa wanasiasa kwa haraka na urahisi. Kengele ya hatari inagonga kichwani mwangu, inakuwa vigumu kukiamini kinachotokea hapa nchini.
Wapo wanaotaja Mwalimu Nyerere aliyefariki Oktoba 14, 1999, kwamba kama angekuwa hai basi angesaidia ‘kupozesha’ tishio la kuvunjika kwa amani.
Hakuna maelewano ndani ya vyama vya siasa, hakuna maelewano kati ya watawala na wapinzani, ushirikiano wa polisi na raia wa kawaida unadorora, vyombo vya habari vinaendeshwa kwa hofu ya kuhusishwa na uchochezi.
Siasa zinaonekana kugeuka kutoka uwanja wa kushindana kwa hoja kuwa uadui. Mwenye ushawishi mkubwa kwa jamii anataka kuidhihirisha ‘nguvu ya umma’ wakati watawala wanawadhibiti kupitia vyombo vya dola.
Kidogo kidogo, Taifa linashuhudia matukio ambayo hayakuzoeleka, yakiwa na athari kubwa kwa fikra na ukuaji wa kizazi cha sasa. Swali la kujiuliza ni kwamba umoja ulioasisiwa tangu kabla na baada ya uhuru wa Desemba 9, 1961, umekwenda wapi?
Amani inatoweka hadi ndani ya Bunge, chombo chenye uwakilishi mpana wa raia. Malumbano yanawaibua majemedari washindi na wanyonge wanaokimbilia kwa wananchi, wakilalamika kuonewa.
Wanaolia kuminywa uhuru wa kuzungumza ndani ya Bunge na kuamua kwenda kwa wananchi, ‘wanapigwa stop’ kwa tamko la kutokuwapo mikutano ya kisiasa hadi 2020!
Hatua hiyo inawafanya wafikie ukomo wa uvumilivu na kuamua kutangaza kwamba utawala uliopo sasa ni wa kidikteta, wanaunganisha nguvu zao kupitia Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Matukio yote hayo hayatoi dalili njema kwa nchi kwa maana yanaondoa dhana na uwapo wa amani ya kweli. Angalau kunakuwa na faraja wanapojitokeza viongozi wa dini na kuushawishi upinzani hususani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoendelea na maandamano na mikutano ya kisiasa nchi nzima, ili kuepusha shari.
Amani ambayo Mwalimu Nyerere aliiasisi na kuihubiri inatafuta njia ya kuelekea wapi ili itoweke katika ardhi ya ardhi ya Tanzania? Tutumize wajibu. Si muda wa kuonyeshana ubabe hasa kwa wanasiasa. Taifa liwe tayari kuilinda na kuitetea amani iliyopo.
jambonewspaper@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment