Videos

Kesi za mafisadi kumalizika ndani ya miezi tisa


JAJI Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande (pichani) amesema Sheria ya Mahakama ya Mafisadi imeanza kufanya kazi ikiwamo majaji 14 watakaofanya kazi, taratibu za kiutendaji na kesi za mafisadi zitachukua miezi tisa kusikilizwa na kutolewa hukumu.

Jaji Chande alisema hayo jana Dar es Salaam ambapo alieleza pia kwamba katika mpango mkakati
wa Idara ya Mahakama wa kipindi cha miaka mitano jumla ya Sh bilioni 238 zinatarajiwa kutumika kuboresha mahakama zote nchini, kwa lengo la kutoa haki kwa kila Mtanzania atakayefika mahakamani.

“Kwa ufupi tumeanza kazi, shauri lisizidi miezi tisa kusikilizwa, kama kutatatokea sababu ambazo hazizuiliki, itaongezwa miezi sita ya kumaliza shauri hilo:

“Kama zitatokea tena sababu ambazo haziepukiki, Mahakama imepewa iangalie muda iliyopewa, lakini kinachotakiwa ni uwajibikaji na tutaangalia nani anakwamisha ili tumchukulie hatua,” alisema Jaji Chande.

Alisema kesi hizo hazitakuwa zikiahirishwa bila sababu ya msingi tofauti na ilivyozoeleka sasa. “Tunataka kuangalia nani anakwamisha, hata kama Jaji anakwamisha atachukuliwa hatua,” alisema Jaji Mkuu na kusisitiza:

“Naweza kusema kuwa Mahakama hiyo imeanza kazi, kwa sababu sheria yake iko tayari na kanuni zake zilitolewa Septemba tisa kupitia Tangazo kwenye Gazeti la Serikali GN 20,” alisema Jaji Chande.

Alifafanua, kwamba kanuni hizo zinaelekeza jinsi mtu anavyofungua kesi, ambapo zikishafunguliwa siku hiyo hiyo atapewa Jaji ambaye ndani ya siku 30 atafanyika usikilizwaji wa awali kujua kama washitakiwa watakana makosa yao au watakiri.

Kuhusu majaji ambao watasikiliza kesi hizo, alisema majaji 14 wamechaguliwa na wamemaliza mafunzo na wapo katika masjala mbalimbali za Mahakama.

Mpango mkakati

Akizungumzia mpango huo, Jaji Chande alisema mpango huo ulishaanza kufanyika kwa Mahakama ya Tanzania kufanya tathmini juu ya hali ya Mahakama na utoaji haki kwa watu wanaopeleka kesi mahakamani.

Alibainisha kuwa mpango huo ndio utakuwa dira yao ya kupanga mambo yao,ambapo wanatarajia kutumia Sh bilioni 140 sawa na dola milioni 65 za Marekani lengo likiwa ni kuboresha utoaji haki kwa watu na pia kuwafanya watu wawe na imani na Mahakama, kwa sababu hivi sasa wengi hawana.

Alisema mpango huo una nguzo tatu, ambayo ni matokeo makubwa manane na malengo 17, kwa sababu ukiwa na mpango mkakati lazima ujue unafanya nini, ambapo nguzo ya kwanza ni utawala bora na uwajibikaji.

Pia alisema ipo na fursa ya kutoa na kupata haki na uharakishaji wa mashauri na kuongeza imani ya wananchi juu ya mahakama, kama wajibu wake wa kutenda haki unavyoeleza. Jaji Chande alisema Mahakama ilijipima kwa kuweka dira kwa sababu hakuna taasisi ambayo itapata maendeleo bila dira, ambapo dira ni mtu yeyote anayepeleka kesi apate haki sawa.

Alisema pia wataongeza ubora wa hukumu, usuluhishi ili watu waelewane na mkataba uandikwe uachwe mahakamani na kuimarisha ukaguzi wa mahakama zote kuanzia za mwanzo.

Jaji Mkuu alisema mkakati huo pia utasaidia huduma za kimahakama ziende kwa teknolojia, kwa sababu wanataka ifike hatua watu wafungue kesi kwenye mitandao na isaidie majaji na mahakimu kutoandika kwa mikono.

Alisema hadi sasa Mahakama ya Rufaa ambayo ndiyo kubwa, majaji wanatumia mikono kuandika wakati nchi zingine kitu kama hicho hakipo.

Alibainisha kuwa fedha hizo asilimia 60 zitatumika kuboresha miundombinu. Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ambao ni mradi wa Benki ya Dunia ndiyo utashughulikia maboresho hayo.

Alisema uzinduzi wa mpango huo utafanyika Kibaha, Pwani, Septemba 21 na Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais John Magufuli, ambapo huko ndiko wataeleza fedha zilizotolewa na Rais zilifanya nini.

Jaji Mkuu alisema Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiwasahau, lakini hivi sasa inawapa kipaumbele ili kuhakikisha haki inapatikana.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment