WAKATI agizo la siku saba la Rais John Magufuli likimalizika jana, Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) limesema bado linaendelea na makusanyo ya madeni ya wadaiwa sugu huku likieleza mwishoni mwa mwezi huu taarifa zitatolewa.
Akizungumza jana na JAMBO LEO, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NHC, Suzan Omari alisema baada ya tamko la Rais Magufuli, kitengo cha ukusanyaji bado kinaendelea na ukusanyaji madeni ya kila mwezi na mchakato utakapokamilika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nehemia Mchechu ataweka hadharani kiasi cha fedha kilicholipwa.
“Bado ukusanyaji madeni nchi nzima unaendelea, baadhi ya wadaiwa wamepunguza madeni yao taarifa halisi zitatolewa mwishoni wa mwezi huu katika utaratibu uliozoeleka,” alisema.
Alisema baada ya tamko, kuna wadaiwa waliomba wapewe muda wa kulipa fedha wanazodaiwa.
Alisisitiza kuwa kabla ya agizo hilo kutolewa, NHC ilikuwa ikidai wapangaji wake takribani Sh bilioni 15 zikiwamo taasisi za Serikali, wizara, taasisi na watu binafsi.
Hivi karibuni, Rais Magufuli akiwa Magomeni Kota alitoa siku saba kwa taasisi za Serikali zinazodaiwa malimbikizo ya madeni na shirika hilo zilipe madeni yao, la sivyo mali zao zitolewe nje.
Pia alimtaka Mkurugenzi wa NHC kutomwogopa mtu yeyote awe Rais, Waziri, Chadema au kiongozi wa Serikali na endapo atashindwa kulipa, mali zake zitolewe nje.
Miongoni mwa taasisi zinazoongoza kudaiwa na NHC madeni ambayo yamefikia zaidi ya Sh bilioni tisa ni Ofisi ya Rais inayodaiwa zaidi ya Sh milioni 10 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni mbili.
Taasisi zingine ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto I zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda Sh milioni 613 na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sh milioni 360.
Mchechu alisema pamoja na deni hilo, zimo taasisi na watu binafsi ikiwamo ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye hivi karibuni mali zake zilitolewa nje kwa kushindwa kulipa deni la Sh bilioni 1.1.
Wakati huo huo, Meneja Operesheni wa Kampuni ya Udalali ya Majembe, Nicholaus Mwanasenga amesema oparesheni ya kuwatolea vitu wadaiwa sugu wa NHC litaendelea Dar es Salaam Ijumaa na Jumtatu ijayo.
“Tunafanya kama kushitukiza tukiwaambia tunaanza leo inakuwa rahisi kujipanga, ukifanya kwa mtindo huu wengi unawabamba, “alisema Mwanasenga.
Ofisa Habari wa Kampuni ya Udalali ya Tambaza, Issa Ramadhan alisema kampuni iko katika hatua za mwisho za kukamilisha kusaini mkataba na NHC kwa ajili ya oparesheni hiyo na kati ya jana na leo ulitarajiwa kusainiwa.
0 comments:
Post a Comment