HOFU ya maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) yaliyokuwa yafanyike Alhamisi iliyopita, yamesababisha baadhi ya watalii waliokuwa wamedhamiria kuja nchini kuangalia kupatwa kwa jua, kuahirisha safari zao kwa sababu za kiusalama.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Uhusiano Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Sengeneza Geofrey alisema alipata taarifa kutoka kwa mwongoza watalii kuwa wageni hao walipata hofu kuja kuangalia kupatwa kwa jua Septemba mosi.
“Sisi hatufanyi biashara ya kuongoza watalii, kazi yetu ni kuhimiza watalii waje na kampuni za kupeleka watalii hao sehemu zao, hao wenye kampuni ndio wanajua,” alisema.
Alisema alipata taarifa kutoka kwa mwongozaji mmoja watalii kuwa kulikuwa na orodha ya watalii waliotakiwa kufika kuangalia kupatwa kwa mwezi lakini waliahirisha.
“Kuna kitu kama hicho kweli kilikuwapo, lakini nilikisikia tulipozungumza na hao waongozaji utalii lakini kwa idadi ni wengi kiasi gani hatuwezi kufahamu,” alisema.
Alisema mbali na hali hiyo, lakini walipata watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali huku akibainisha walioahirisha walikuwa wachache kuliko waliofika kuangalia kupatwa kwa jua.
Alitaja watalii hao ni kutoka nchi ya Marekani, Uholanzi, Canada, Ujerumani na hata India, huku bara la Afrika wakitoka Afrika Kusini, Zambia, Malawi, Kenya na wenyeji wa Tanzania ambapo walikuwapo wakazi kutoka Mwanza.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Universal Palagon Links (UPL), mkoani Mbeya, Gabriel Shawa alisema katika kampuni hiyo kulikuwa na wageni 11 ambao waliahirisha safari ya kufika kuangalia kupatwa kwa jua Septemba mosi, huku kadhaa wakipeleka tarehe za kuja nchini mbele.
“Siingiliani sana na kusema kuwa Ukuta ndio uliosababisha hilo kutokana na tamko la kiusalama kwa upande wao, labda waliamua kubadili tarehe ya kufika lakini bado biashara kwangu itaendelea,” alisema.
Alisema anachojali yeye ni kufika kwa wateja wake ambapo wengine waliahirisha kufika na kudadisi kutokana na taarifa ya kiusalama ambapo walikuwa na shaka.
“Huwezi kudadisi sana, kwa sababu nafanya biashara si siasa, 11 waliahirisha kufika lakini siwezi kudadisi sana kiukuta ingawa idadi hii haijawahi kutokea,” alisema.
0 comments:
Post a Comment