KUMETOKEA sintofahamu kuhusu wapi waliko wakurugenzi 12 kati ya 185 walioteuliwa na Rais John Magufuli.
Hali hiyo inachangiwa na uteuzi wa wakurugenzi wapya wa halmashauri, miji na manispaa ikiwa ni miezi miwili tu tangu uteuzi wa awali.
Hivi karibuni, Rais Magufuli aliteua wakurugenzi wapya 13, mmoja akijulikana kuwa anaziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Azimina Mbilinyi.
Kulingana na uchunguzi wa JAMBO LEO, hakuna taarifa ambayo iliwahi kutolewa na Serikali kupitia ofisi yoyote, kuhusu mabadiliko hayo, tofauti na Mbilinyi ambaye Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilitoa taarifa kuwa uteuzi wake umetenguliwa.
Kwa wakurugenzi wengine akiwamo wa Manispaa ya Dodoma, Dk Leonard Masale ambaye nafasi yake imechukuliwa na Godwin Kunambi, hakuna taarifa za wapi alipangiwa baada ya uteuzi wa awali.
Katika Halmashauri ya Tarime, Mkurugenzi wa awali alikuwa Apoo Tindwa na sasa ni Elias Ntiruhungwa, Bukoba nafasi ya Makonda Stephen ilichukuliwa na Mwantumu Dau na Ukerewe ya Tumaini Shija imechukuliwa na Frank Bahati.
Katika Halmashauri ya Mbulu, awali alikuwapo Festi Fwema na nafasi yake kuchukuliwa na Hudson Kamoga, Nsimbo ilikuwa ya Joachim Nchunda lakini kwa sasa ni ya Mwailwa Pangani, Nkalama alikuwapo Martin Mtanda lakini sasa amekwenda Godfrey Sanga.
Aidha, hali kama hiyo ilitokea katika Halmashauri ya Ulanga ambako Mkurugenzi aliyekuwapo kwa mujibu wa uteuzi wa awali, ni Audax Rukonge na mpya sasa ni Yusufu Semuguruka.
Nachingwea, Mkurugenzi alikuwa Bakari Mohamed Bakari na sasa ni Bakari Mohamed, Kibondo alikuwa Shelembi Manolo na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mnweke, Manispaa ya Moshi alikuwapo Michael Mwandezi na sasa yupo Butamo Ndalahwa huku Karatu ilikuwa ya Banda Sonoko lakini sasa ni Waziri Mourice.
Alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Musa Iyombe alisema wateule wapya walikuwa wanaziba nafasi zilizokuwa wazi, kwa kuwa wateule wa awali walishindwa kukidhi baadhi ya vigezo kama afya, udhuru na vingine.
“Walioteuliwa wanajaza nafasi badala ya wa awali kushindwa kukidhi baadhi ya vigezo vikiwamo vya afya, udhuru na vingine,” alisema.
Sababu hizo za Iyombe zinatia shaka kama wateule hufanyiwa uchunguzi kabla ya kupewa nafasi huzo na au kama huulizwa kabla.
Kwa kipindi cha miezi 10 ya uongozi wa Rais Magufuli ameondoa wateule wake wapya zaidi ya watano ambapo alianza na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anne Kilango-Malecela kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu wafanyakazi hewa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kwa kulewa bungeni, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi , Emil Ntakamulenga ambaye alitumbuliwa siku ya kiapo Ikulu na Mbilinyi.
0 comments:
Post a Comment