WAFUASI wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima juzi walitinga mahakamani kumsindiza Askofu wao wakiwa wamevaa sare ya suti nyeusi, tai nyeusi na nyekundu.
Mwonekano wao ulishangaza watu waliokuwa kwenye Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Waumini hao waliofurika mahakamani hapo muda wote walikuwa vikundi vikundi wakisubiri kusikilizwa kwa kesi ya kutoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, inayomkabili Gwajima.
Kesi hiyo ilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha kwa ajili ya kutajwa na kuangalia rufaa iliyokatwa Mahakama Kuu na Jamhuri, kuhoji kwa nini CD inayomwonesha Askofu Gwajima akitoa maneno hayo kama kielelezo katika kesi hiyo, ilikataliwa.
Hakimu Mkeha alisema kesi hiyo imechukua miezi minne bila chochote kuendelea kutokana na rufaa hiyo kukatwa, kwa hiyo kama upande wa Jamhuri una nia ya kuondoa rufaa hiyo, iiondoe.
Kutokana na hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alidai kuwa wana nia ya kuondoa rufaa hiyo ili kesi iendelee ilipoishia.
Baada ya hapo, Hakimu Mkeha aliiahirisha hadi Septemba 29 itakapoletwa kutajwa na kuangalia upande wa Jamhuri ulikoishia na rufaa yao, ambapo pia Hakimu alimtaka shahidi aliyefika mahakamani kutoa ushahidi, awepo siku hiyo.
Awali Mahakama ilitupilia mbali maombi ya kupokea kielelezo hicho cha Jamhuri kwa kushindwa kutimiza kigezo cha kisheria cha vielelezo vya eletroniki mahakamani.
0 comments:
Post a Comment