RAIS John Magufuli amelitaka Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kutimua wapangaji wasiolipa kodi za pango zikiwamo asasi za Serikali, kama ilivyofanya hivi karibuni kwa mmoja wa wapangaji wake Dar es Salaam.
Ingawa Rais Magufuli hakumtaja kwa jina mpangaji huyo, lakini Septemba mosi, NHC iliondoa samani kwenye jengo ilimo klabu ya Billicanas inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kampuni ya Free Media iliyo chini ya familia ya mwanasiasa huyo.
Rais Magufuli, amesema asasi za Serikali zinazodaiwa kodi na NHC zinapaswa kufukuzwa na kuondolewa vitu vyao kwenye nyumba hizo ndani ya siku saba kuanzia jana.
Alisema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika eneo maarufu kama ‘Kota za Magomeni’, alipokuwa katika ziara yake katika manispaa ya Kinondoni.
Pamoja na kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, Rais Magufuli alisema: “Usiogope kumtolea mpangaji vitu nje hata kama ni waziri au mwanachama cha CCM, Ukawa au CUF,” alisema.
Aliongeza: “Kama hawataki kulipa kodi ni vema kuwatolea vitu vyao nje, kwani haiwezekani mtu akae bure.”
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kutolewa nje kwa vifaa vya taasisi kama wizara, itakuwa chanzo cha kuzifanya ziharakishe kuhamia Dodoma.
Rais Magufuli alisema haiwezekani kuwapo watu wakiwamo wanaosafiri nje ya nchi, lakini wanashindwa kulipa kodi za pango kwa NHC.
Wakati akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM Julai 23 Dodoma, Rais Magufuli aliahidi Serikali kuwa imehamia mjini humo ifikapo mwaka 2020.
Alieleza kushangazwa na baadhi ya wizara kuendelea kung’ang’ania Dar es Salaam, akitolea mfano Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.
Alisema wizara hiyo inastahili kuwa Dodoma sasa ikitekeleza ujenzi wa barabara nchi nzima.
Makazi
Rais alisema ziara yake ililenga kuhakikishia wakazi 644 waliobolewa nyumba za ‘kota’ za Magomeni mwaka 2012, kwamba watajengewa nyumba za ghorofa ndani ya kipindi cha takribani mwaka mmoja.
Alisema wakazi wa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 33 wal-ishapewa ahadi nyingi tangu mwaka 2012 bila utekelezaji hivyo kulifanya eneo hilo ligeuzwe maegesho ya magari.
Siri
Pia Rais Magufuli alieleza kile alichokiita kuwa siri, kuhusu eneo hilo kutaka kukabidhiwa kwa mwekezaji badala ya walengwa husi-ka.
“Haiwezekani mtu akavunjiwa nyumba na kuambiwa akapange, halafu asilipiwe kodi wakati ameondolewa mahali alipokuwa akiishi,” alisema.
Alisema ujenzi wa nyumba mpya utakapokamilika, zitapangishwa kwa waliokuwa wakazi wa eneo hilo na kutolipa kodi kwa kipindi cha miaka mitano.
“Katika hii miaka mitano mtakaokuwa mkiishi ndani ya hizo ny-umba, tutakuwa tunafanya mikakati ya kuwauzia ili mmiliki wenyewe,” alisema.
Maeneo ya NHC
Rais Magufuli alisema Serikali yake imeamua kuchukua maeneo yanayosimamiwa na NHC katika mikoa 20 nchini, ili kuhakikisha hakuna hujuma zinazofanywa dhidi ya maeneo hayo.
Alisema maendeleo hayapaswi kuathiriwa na itikadi za kisiasa aka-toa mfano wa mwanasheria aliyetetea wakazi wa ‘kota’ za Magomeni kwamba alikuwa Twaha Taslima ambaye ni mwanachama wa CUF.
Ashangiliwa
Taslima alipoingia eneo la mkutano alishangiliwa na kupongezwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Alipohojiwa na JAMBO LEO kuhusu hatua ya Rais Magufuli, alisema: “Nimefurahi kuona Rais amesimamia haki katika hili, hivyo ninawaambia wateja wangu wasiwe na wasiwasi.”
Mmoja wa waliokuwa wakazi wa eneo hilo, Mohamed Said, alimshukuru Rais Magufuli kwa uamuzi wake wenye kujali wanyonge.
Haiwezekani mtu akavunjiwa nyumba na kuambiwa akapange, halafu asilipiwe kodi wakati ameondolewa mahali alipokuwa akiishi
Rais John Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wanaojenga mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipokagua ujenzi huo jana. Kushoto kwake ni Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. (PICHA YA IKULU)
Ushirika wetu kwenye UKAWA haukuwa na umoja. Katibu Mkuu alitumia utaratibu kama alivyofanya kipindi cha 1984 dhidi ya Jumbe hali iliyosababisha Jumbe (marehemu Aboud) kuvuliwa madaraka
0 comments:
Post a Comment