RAIS John Magufuliameonekana kuteswa na kusikitishwa na kitendo cha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kumnyima mkono Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alipomsalimia wakati wa maziko ya Rais wa Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi.
Masikitiko hayo aliyatoa jana wakati akihutubia kwenye mkutano wa hadhara wa kushukuru wananchi wa Zanzibar kwa kumchagua kuwa Rais wa Tanzania, katika viwanja vya Demokrasia Unguja, ambako alitumia muda mrefu kufafanua kuhusu mkono huo kwa kauli tofauti tofauti.
Alisema Dk Shein kwa upendo na moyo wake wa huruma, aliamua kumpa mkono mtu fulani (Maalim Seif), lakini cha kushangaza alikataa kupokea mkono na kibaya zaidi ilikuwa msibani.
“Juzi wote tumeshuhudia msibani na Watanzania wameona kwenye picha, Dk Shein kwa unyenyekevu alimsalimu mtu fulani, lakini akakataa. Mkono huo huo ambao ameukataa, ndio Rais Shein anautumia kusaini fedha za safari na matibabu.
“Kweli una moyo wa upendo, natamani ningekuwa na hata robo maana mimi nisingeweza kutumia mkono wangu kumsainia mtu akatibiwe, wakati mkono huo huo aliukataa,” alisema Dk.Magufuli.
Dk Magufuli alisema pamoja na mambo mengine, bado anampongeza Rais Shein kwa upole, ukarimu na uungwana kwani licha ya kupata asilimia 92 ya kura zote, ameingiza wapinzani kwenye serikali yake.
‘Hataki’ wapinzani
Alisema yeye hawezi kumuingiza mpinzani kwenye Serikali yake kama alivyofanya Dk Shein na kufafanua kuwa ndani ya Serikali yake, hatakuwa tayari kumuingiza mpinzani afanye naye kazi.
“Rais Shein muombe Mungu akupe hata robo ya mawazo yangu. Natamani niwe na moyo wa aina yako lakini siwezi maana kama mimi ningekuwa nimekataliwa mkono, tena msibani, nisingesaini hata kidogo fedha kwa ajili ya huyo mtu.
“Jana (juzi) nikiwa Pemba nilikuomba uongeze ukali hata kidogo. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 uchaguzi umekwisha na hautarudiwa tena ila uchaguzi mwingine ni mwaka 2020. Kwa sasa ni muda wa kufanya kazi tu,” alisisitiza Dk. Magufuli.
Alisema anafahamu kuwa Zanzibar kuna tatizo la maji lakini tayari kuna fedha Sh bilioni 200 zimetengwa kwa ajili hiyo, ambapo alirudia kuwa hata kama kuna watu wanamnyima mikono, aendelee na jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Magufuli alisema lazima watu watambue walikotoka, walipo na wanakokwenda kwa kuwa sasa Zanzibar ni tofauti na ile ya zamani.
Alikumbusha alipokuwa Waziri wa Ujenzi, kwamba alisimamia upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na anakumbuka hiyo ilikuwa ni kwenye utawala wa Awamu ya Tatu chini ya mzee Benjamin Mkapa.
Alielezea kushangaa kuona mtu anatoka Zanzibar na kwenda kuwaambia wageni wasije Zanzibar, lakini cha kufurahisha wamempuuza na wageni wameendelea kuja maana kuna usemi unaosema kuwa mgeni njoo mwenyeji apone.
*Kufuga ndevu
Magufuli alisema katika maisha yake hakuwahi kufikiria kuwa Rais, maana alitambua kuwa vyeo vinaletwa na Mungu na kama Mungu amesema hapana ni hapana tu, hata kama unafuga ndevu namna gani kama Mungu amekataa huwezi kuwa Rais.
“Rais Shein ana moyo wa upendo kwa watu wote lazima aachwe afanye kazi yake maana Wazanzibari wameamua ndio awe Rais,” alisema na kuongeza kuwa wakati Rais Shein anafanya mambo yote kwa ajili ya Zanzibar, anatokea mtu anamnyima mkono mbele ya waombolezaji waliopo msibani.
Alifafanua kuwa hakuna kitabu chochote au dini yoyote duniani kinachofundisha chuki badala yake pale watu wanapokoseana, basi wasameheane.
“Lakini hata kwenye msiba uuuwiii,” alisisitiza Rais Magufuli na kuongeza anatamani kuona nchi inakuwa ya viwanda ili watu wengi wapate ajira kwani hakuna mtu anayekula chama cha siasa.
Aliomba wananchi wa Zanzibar wadumishe umoja na mshikamano na kuweka chuki pembeni, kwani ni jambo baya kuona kuna watu wanafanya kazi ya kufarakanisha watu.
“Mnamkuta mtu na dada yake mmoja CUF na mwingine CCM wewe unamfarakanisha. Unakuta mtu na mkewe mmoja CUF na mwingine CCM unawafarakanisha mpaka wanashindwa kulala chumba kimoja, huu ni sawa na ushetani,” alisema.
*Fyoko fyoko
Wakati huohuo Rais Magufuli ameonya kuwa katika utawala wake, amani ataipa kipaumbele na yeyote atakayeleta fyokofyoko itamrudia mwenyewe.
Alisema msimamo wake hautabadilika na anayetaka kuvuruga amani atamshughulikia kwani hatamuachia iwe mchana au usiku, iwe asubuhi au jioni na hata akiwa kitandani, atakayejaribu kuleta chokochoko lazima atamshughulikia.
Magufuli alisema amekwenda Zanzibar kwa dhamira ya kuwaeleza wazi kuwa katika urais wake, amani itakuwa kitu cha kwanza ndio maana aliwahi kusema Dar es Salaam atakayeleta fyoko fyoko, atakiona cha mtema kuni.
Alisisitiza kuwa msimamo wake wa pili ni kudumisha Muungano uliopo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuulinda kwa nguvu zake zote.
Kipaumbele chake cha tatu, alisema ni kuleta maendeleo ya wananchi wote bila kujali vyama vyao. “Iwe CCM, iwe CUF, iwe Chadema na hata wasio na vyama wote nitahakikisha naleta maendeleo yao,” alisema.
*Dk Shein
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Magufuli, Dk Shein alisema vyama vya upinzani vitaiona Serikali ya Zanzibar kama ilivyo, kwa kuwa kwa kutumia utaratibu wa kidemokrasia CCM hawang’ooki kwani kila uchaguzi watashinda na kuwagaragaza.
“Baada ya uchaguzi zikatoka kauli kwamba utarudiwa tena, masikini roho zao, nami huwa nawauliza utarudiwa kwa Katiba gani, na kwa sheria gani? Maana chini ya Tume ya Uchaguzi ya Mwenyekiti Salimu Jecha, uchaguzi umemalizika.
“Sheria na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio iliyotoa mamlaka kwa Tume ya Uchaguzi kuendesha uchaguzi wa rais, wabunge, madiwani na wawakilishi. Ni katiba ya Zanzibar hakuna katiba nyingine duniani inayoweza kuitisha uchaguzi tena, hizi ni hadithi ziacheni mitaani, ukweli tutakutana mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Alisema hakutakuwa na Serikali ya mpito Zanzibar na wanaosema hivyo wanajidanganya kwani hakuna sababu ya kuwa na serikali ya aina hiyo, kwa sababu Serikali imeshakuwa madarakani.
*Mafuta na gesi
Kuhusu mafuta na gesi Zanzibar, alisema limepatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kushirikiana na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo walitunga Sheria ya Mafuta na Gesi na kwa sheria hiyo, Zanzibar ilipewa mamlaka ya kutunga sheria yake ya mafuta na gesi na imeshapelekwa kwenye Baraza la Wawakilishi na kikao kijacho cha Septemba 26, itasomwa tena.
“Baraza wakiipitisha wataileta kwangu, nitasaini na kuwa sheria na kuanza kutumika, baada ya hapo tutaanza kuita wawekezaji na Zanzibar itaanza kupiga hatua kwa kuwa tuna mambo mazuri ya mafuta na gesi,” alisema.
Alisema atashirikiana na Rais Magufuli kutekeleza sheria hiyo, pamoja na kuiwezesha Zanzibar kukuwa kiviwanda hasa vya samaki.
Aliongeza kuwa Zanzibar imeendelea kukusanya kodi ipasavyo, kwani hivi sasa mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Alitoa mfano wa 2011 walipokuwa wakikusanya Sh bilioni 13 kwa mwezi, wakati sasa wanakusanya Sh bilioni 52.
“Pesa hazitutoshi lakini tunazo, tumewalipa wastaafu takribani Sh bilioni 16, tunatoa mishahara kwa wakati na utalii umetuingizia fedha za kigeni kwa zaidi ya asilimia 80,” alisema.
0 comments:
Post a Comment