Videos

Utumbuaji majipu ujibu hitaji la maisha bora


Mashaka Mgeta
TANGU alipoapishwa Novemba 5 na alipolizindua Bunge Novemba 20, mwaka jana, Rais John Magufuli alijinasibu kwa kipaumbele kikubwa katika utawala wake, yaani `kutumbua majipu’.

Dhana ya ‘kutumbua majipu’ ni isiyotofautiana kiutekelezaji na kauli mbiu kama ‘kupiga vita wahujumu uchumi’ iliyoasisiwa katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, ama ‘ufagio wa chuma’ wakati Rais akiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi.

Lakini kwa namna ya pekee, Rais Magufuli akalitangazia taifa na dunia kwa ujumla, kwamba atahakikisha anaishinda vita dhidi ya mafisadi wa aina tofauti wanaohujumu raslimali za umma, ili Tanzania iwe mahali salama pa kuishi.

Akilihutubia taifa kutokea bungeni mjini Dodoma, sura ya Rais Magufuli ilionyesha dalili za kudhamiria alichokuwa akikitamka, kwamba hakikutoka akilini tu bali na moyoni pia.

Umma uliipokea hotuba yake kwa shangwe, dunia iliitafsiri hotuba yake kama sehemu ya safari mpya kwa nchi za Afrika, iliyofunguliwa na Rais Magufuli ili watawala wengine hasa katika mataifa yaliyoghubikwa na ufisadi, wafuate nyayo zake.

Rais Magufuli akaiita dhamira yake hiyo ‘kutumbua majipu’. Mpaka sasa kutumbua majipu kumekuwa na maana halisi ya kuwashughulikia mafisadi wa aina tofauti wa uhujumu wa mali na raslimali za umma.

Ilikuwa mfano wa hadithi inayoanza huku miongoni mwa wasikilizaji wakitarajia itaishia njiani pasipo kukidhi kiu ya wao. Lakini ikawa jioni, ikawa asubuhi, Rais Magufuli bado `anatumbua majipu’ Anasafisha uozo ndani ya sekta ya umma.

Walio wengi wanampongeza Rais Magufuli kwa hatua iliyopo sasa na inayoendelea katika `kutumbua majipu’.

Wapo wanaomkosoa wakitumia kigezo kuwa Rais Magufuli anatoa kauli zilizo mfano wa maagizo kwa mahakama, akiwakandamiza watuhumiwa wanaokabiliwa na ‘kutumbuliwa majipu’.

Lakini wanaomtetea Rais Magufuli wanaweka wazi kwamba hatua zinazofikiwa ni kujibu hitaji la kuchukua uamuzi mgumu dhidi ya watumishi wa umma waliotumia mianya ya udhaifu wa sheria zilizopo, ili kuliibia taifa na kujineemesha kulikopita ukomo, wakawa mfano wa watu wanaoishi peponi!

Mbali na ‘kutumbua majipu’, Rais Magufuli amefikia hatua ya kushusha kiwango cha kipato kwa watumishi wa umma, waliokuwa wanalipwa mishahara minono, kwa wengine isiyolingana na majukumu ya kazi zao.

Inapofikia hatua hiyo, Rais Magufuli anaistahili pongezi. Anastahili kupigiwa makofi ikibidi kuimbiwa nyimbo za shangwe na mapambio. Pamoja na mafanikio hayo, ipo haja kwa wasaidizi wake na jamii kwa ujumla, kumsaidia. Tanzania haiwezi kujengwa na mtu mmoja ama kikundi cha watu wachache waliopo Ikulu, kwenye baraza la mawaziri ama ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ujenzi wa taifa wenye tija unawahitaji watu wa kada zote, Imani zote, itikadi za vyama vyote, wenye taaluma tofauti, japo kutaja kwa uchache.

Kwa mfano haiwezekani kwa Watanzania wote kushiriki mipango ya namna bora ya kukuza uchumi na kustawisha maisha ya watu.

Ama wanasiasa wote, waandishi wa habari wote, wabunge wote ama asasi zote za kiraia. Lakini kupitia kupazwa kwa sauti ama kueneza maandiko yenye utashi mwema kwa nchi, serikali inaweza kuchukua mambo ya msingi, ikayatumia kuboresha mipango ya wataalamu ili azma ya kuwa na maendeleo endelevu ifikiwe.

Ni kwa hali hiyo, kada hizo hazipaswi kufumba midomo yao kama ambavyo isivyostahili kufumbwa midomo yao. Wanapaswa waachwe wakidhibitiwa kwa misingi ya Katiba na sheria zilizopo, kuteta ili kutoa mchango wa kuchagiza kasi ya maendeleo ya nchi.

Kuachwa huru kwa kada nyingine zilizo nje ya serikali, hakuna manufaa kwao binafsi bali kwa jamii pana wakiwamo waliomo kwenye mifumo rasmi ya utawala wa nchi.

Ndivyo ilivyokuwa kwa taifa tangu utawala wa Mwalimu Nyerere, ambaye baada ya kustaafu kwake alisema si kweli katika miaka 24 ya utawala (viongozi wa serikali) hawakufanya mambo ya hovyo.

Ni kwa hali hiyo, kada zilizo nje ya utawala zinapopewa fursa kutumia haki za kikatiba na sheria, kuikosoa, kuishauri na kuielekaza serikali iliyopo madakarani, linakuwa jambo lenye tija na si udhaifu kwa watawala. Kwa mfano, yapo mambo ya kufanywa baada ya ‘kutumbua majipu’, ili kutoa jawabu la maisha bora kwa Mtanzania.

Kwa maana haitakuwa na maana sana ikiwa ufanisi wa ‘utumbuaji majipu’ hautajibu hitaji la kuondokana na umasikini.

Ama kupunguza kipato cha ‘mabosi; katika sekta ya umma hakutakuwa na tija ikiwa wenye kipato duni wataendelea ‘kusota’ wakishindwa kumudu gharama za maisha, wakajikuta wanaendelea kuambulia mlo mmoja kwa siku.

Hongera Rais Magufuli kwa ‘utumbuaji majipu’. Lakini umma unahitajika kumsaidia ili hatua hiyo ijibu hitaji la kuondokana na umasikini.

0754691540
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment