Profesa Ibrahim Lipumba |
Profesa Lipumba ambaye pia ni mchumi, aliitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Joto la Asubuhi kupitia kituo cha Clouds FM ambapo pia alisema mapendekezo ya awali yalikuwa ni kila chama kitoe mgombea urais lakini Maalim Seif Sharif Hamad alikiuka na kutaka Chadema pekee ndiyo itoe mgombea.
Swali: Ni kitu gani kilikuaminisha kuwa mtu anayefaa kugombea ndani ya Ukawa ni Jaji Warioba?
Lipumba: Nilipata fikra kuwa kwa sababu wanahitaji kutekeleza mambo ambayo Jaji Warioba amekuwa akiyasimamia na kuyaweka ndani ya Rasimu ya Katiba, ikiwamo ripoti ya kupambana na ufisadi ya mwaka 1996 wakati wa awamu ya Rais Benjamin Mkapa, na kwa kuwa ni mwadilifu, angeweza.
Baada ya kuona kuwa Jaji Warioba anafaa nilimfuata na kumwomba asimame kwa upande wa Ukawa kama mgombea urais, lakini alinigomea na kunieleza kuwa ameshastaafu siasa tangu mwaka 2002 hivyo hawezi kugombea.
Nilipoona mtu niliyekuwa namtarajia ambaye ni Jaji Warioba alinijibu kuwa amestaafu siasa na bado mwana CCM, aliniambia anakubali mambo ambayo tumefanya pamoja hasa kwenye uandaji wa Rasimu ya Katiba mpya, lakini suala la kujiunga na Ukawa kwake halikuwapo.
Baada ya kunijibu hivyo nilimweleza kuwa kutokana na kukataa kwake kunanifanya niamini kuwa yeye ndiye mtu sahihi zaidi, maana hakuwa tayari kukubali kirahisi lakini msimamo wake ukabaki kuwa haitawezekana.
Nilikuwa nafikiri kuwa ikiwa tunakwenda kutafuta mtu nje ya Ukawa na anayeweza kuwa na msimamo mzuri kwa misingi ya kuanzishwa Ukawa ya kuunga mkono Katiba ya Wananchi basi alikuwa Jaji Warioba.
Kama kuna watu ambao ndani ya CCM wangeweza kuchukuliwa kuwa wagombea wa urais kwenye Ukawa kwa misingi ya kuanzishwa kwake, mtu aliyekuwa anawekwa kwenye fikra hizo ni yeye.
Swali: Ulitumwa na Ukawa kumfuata Jaji Warioba?
Jibu: Hakuna aliyenituma ila mimi binafsi niliamini Jaji Warioba ndiye mtu sahihi kama tunataka mgombea kutoka nje ya Ukawa.
Swali: Uliposikia wanafanya mpango wa kumkaribisha Lowassa ndani ya Ukawa. Je, ulitumia nafasi yako kabla ya kuandika barua?
Lipumba: Nilikutana na Lowassa peke yangu, maana nilielezwa kuwa anataka kukutana nami. Akanieleza kuwa alifanya mazungumzo na wenzengu na kuhoji kama nina habari.
Nilimjibu sina taarifa nasikia tu ambapo nilishauri ni vema tuwe na kamati ya vyama vyote ili kujadili suala hilo kabla ya kulipatia ufumbuzi.
Nilikutana na Lowassa na kuzungumza naye kuhusu suala hilo kabla ya kwenda kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Baada ya hapo niliwapa taarifa Mbowe na Mbatia kuwa inabidi wakutane na Lowassa ili kujadili anayepaswa kugombea urais.
Ingawa Lowassa alikuwa na nafasi kubwa ya kupata uongozi ndani ya Serikali, lakini sidhani kama angeweza kutimiza matakwa ya wananchi.
Swali: Kama uliona Lowasa hawezi kutimiza matakwa ya wananchi, uliwashauri nini Ukawa?
Lipumba: Niliwashauri walipo wangeweza kutazama mtu anayeweza kuendana na mahitaji yao na mimi nikiwa ndani ya Ukawa kabla ya kupata mgombea urais.
Tungeweza kupata ushindi kupitia kwa Lowassa lakini hata ukipatikana ushindi tungekwenda kusimamia mambo gani na katika eneo lipi?
Suala lililopo katika siasa ni kuwa ukishachaguliwa unatakiwa uunde Serikali ili usimamie misingi fulani ambayo itakidhi mahitaji ya wananchi .
0 comments:
Post a Comment