CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimepongeza hotuba ya Rais John Magufuli aliyotoa kwenye ziara yake visiwani humo kwani ameonesha ana dhamira ya kuharakisha maendeleo ya wananchi bila kujali tofauti za kisiasa.
Akizungumza mjini humo jana, Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Waride Bakari Jabu, alisema CCM inaunga mkono na kupongeza hotuba zilizotolewa na Rais Magufuli huko Unguja na Pemba kwa kusisitiza dhamira ya Serikali zote mbili kuwaletea wananchi maendeleo.
Waride alisema viongozi wa chama chake na wananchi kwa wote sasa wanatakiwa kushirikiana katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa ili Zanzibar iweze kufikia uchumi mkubwa katika nchi za Afrika.
“Ziara ya Rais Magufuli imetoa mwongozo imara wa kuwakumbusha watendaji na viongozi nchini juu ya dhamana na mambo ya msingi wanayotakiwa kuyatekeleza kwa wananchi,” alisema
Alifafanua kuwa,”CCM tunaunga mkono kwa nguvu zote hotuba ya Rais Magufuli kwani imezungumzia na kugusia mambo ya msingi yanayogusa maisha ya wananchi, hasa wa kipato cha chini na kutoa mwongozo wa namna Serikali zinavyoendelea na mikakati imara ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya Taifa kwa jumla.
“Pia tunatakiwa kuendelea kuwa wamoja na wazalendo bila ya kujali tofauti zetu za kidini, kisiasa na kikabila kwa kulinda amani na utulivu wa nchi zetu kwani ndiyo siri ya mafanikio ya nchi zetu”. Katibu huyo alisema Dk. Magufuli ameonesha nia ya dhati ya kuendelea kutafuta fursa mbalimbali za miradi ya maendeleo itakayoweza kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.
Alisema miongozo mwa mambo ya msingi yaliyosisitizwa na Dk. Magufuli pia yanaungwa mkono na CCM Zanzibar ni dhamira ya kuhakikisha Zanzibar inakuwa ni nchi ya viwanda vya kusindika samaki wanaotokana na uvuvi wa kisasa wa bahari kuu vitakavyotoa fursa za ajira kwa vijana na wananchi.
Waride alipongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua milango ya wawekezaji wakubwa kuwekeza Zanzibar huku wakitafuta wahisani kutoa mamilioni ya fedha za kuendesha miradi ya kijamii ukiwemo mradi wa maji safi Unguja uliotolewa fedha za mkopo na Serikali ya India.
Alisema kwa ushirikiano wa Rais Dk. Magufuli na Dk. Shein, CCM inaamini kwamba Tanzania bara na Zanzibar kwa ujumla zitakuwa nchi za kupigiwa mfano duniani katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo, kisiasa na kijamii.
0 comments:
Post a Comment