MTU aliyekuwa akihubiri Neno la Mungu kwenye mabasi ya abiria aliyejulikana kwa jina la Makoye Shigela (56) amefariki dunia baada ya kuanguka ndani ya basi alimokuwa akihubiri.
Tukio hilo lililoshitua abiria lilitokea mwishoni mwa wiki, baada ya mtumishi huyo wa Mungu anayetajwa kutoka Kanisa la Mashahidi wa Yehova, kupanda basi la Kampuni ya Nyehunge linalofanya safari zake kati ya mikoa ya Mwanza na Morogoro.
Alianguka na kufariki dunia wakati akikusanya sadaka kutoka kwa abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo, huku mwandishi wa habari hii akishuhudia tukio hilo.
Marehemu alipanda basi hilo maeneo ya Buhungumalwa akielekea mkoani Shinyanga na alipomaliza kutoa Neno la Mungu na kuhubiri, alianza kuomba sadaka kwa abiria na kuzikusanya. Ghafla alianguka na kupoteza fahamu.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alieleza kuwa marehemu alikuwa akijihusisha na kazi hiyo kwa muda mrefu akihubiri katika mabasi ya mikoani yanayotumia Barabara ya Mwanza Dar es Saalam.
Baada ya Shigela kuanguka, abiria waliopatwa na mshangao walimshauri dereva wa basi hilo, Emanuel Deus kumpeleka hospitali ya karibu ili apatiwe huduma, lakini kabla ya kufika eneo hilo la kutolea huduma, ilibainika amefariki dunia.
Kifo cha mhubiri huyo kilifanya dereva alipeleke basi hilo katika kituo cha polisi ambako alitoa taarifa na polisi kuuchukua mwili huyo na kuupeleka hospitali.
Kwa nyakati tofauti abiria walieleza kusikitishwa na tukio hilo na kusema ni muhimu kwa binadamu kupima afya zao kila mara kuliko badala ya kusubiri hadi wanapougua ili kuepuka vifo vya ghafla.
Mmoja wa abiria hao, Robert Tomas alisema: “ Watanzania wanatakiwa kujenga mazoea ya kupima afya zao ili kubaini matatizo yalioyo ndani ya miili yao. Dunia ya sasa ina magonjwa mengi yanayoua watu kila siku.”
0 comments:
Post a Comment