Videos

Vita Ukawa, Dk Tulia yaanza tena


WABUNGE wa vyama vinavyounda Ukawa jana walipinga kitendo chaNaibu Spika, Dk Tulia Ackson, kuwazuia kusoma utangulizi wa maoni ya wapinzani kuhusu miswada miwili iliyowasilishwa bungeni, kwa maelezo kuwa yana maneno yanayoiponda Serikali kuzuia vyama vya upinzani kufanya shughuli za siasa.

“Tuendelee ila nawaomba mkatizame filamu inaitwa The Great Dictator. Nadhani ujumbe umefika,” alisema Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) wakati akisoma maoni ya upinzani ya Wizara ya Afya, Maendelepo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa niaba ya msemaji wa upinzani wa wizara hiyo, Mbunge wa Siha, Godwin Mollel (Chadema).

Mbali na Matiko aliyesoma maoni ya Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Baraza la Wanataaluma wa Kemia, hata Mollel aliyesoma maoni ya Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, naye aliwataka wahusika kupokea ujumbe huo, hata kama umezuiwa kusoma.

Mara zote ambazo walianza kusoma utangulizi wa maoni hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Dk Abdallah Posi alisimama na kuomba mwongozo kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk Ackson kwamba kinachozungumzwa na wasemaji hao, hakiendani na maana ya miswada hiyo.

Tangu kuanza kwa vikao vya Bunge Jumanne iliyopita, jana ndio ilikuwa siku ya kwanza kwa Dk Tulia kuongoza kikao cha chombo hicho cha kutunga sheria, hivyo mvutano huo kutafsiriwa kama mwendelezo wa vita kati ya wapinzani na Naibu Spika huyo.

Katika mkutano wa Bunge wa Bajeti lililohitimishwa Juni 30, wabunge wa Ukawa, inayoundwa na vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF walikuwa wakitoka ukumbini kila wakati Dk Tulia alipoongoza vikao, wakidai kuwa hawana imani naye kwa kuwa anawabagua na kukandamiza demokrasia ndani ya chombo hicho.

Hata hivyo, uamuzi wa Spika wa Bunge Job Ndugai na viongozi wa dini kuonyesha utayari wa kushughulikia madai hayo, uliwarejesha wabunge hao bungeni na kumaliza siku 32 za kususia vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia.
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment