Videos

Nyuma ya pazia la Msondo Ngoma kuna rekodi kali


Mawazo Lusonzo
HISTORIA ni mwalimu wa kudumu, anayefundisha kwa njia ya kumbukumbu ambayo ni elimu ya kudumu pia!

Ukiuzungumzia muziki wa dansi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, una rekodi na kumbukumbu kubwa za aina ya bendi ambazo zilikuwamo katika orodha, lakini zikafutika katika ramani ya dunia.

Tunapouzungumzia muziki wa dansi leo, hatuwezi kukamilisha historia na kumbukumbu sahihi bila kuzitaja baadhi ya bendi zilizoingia katika orodha ya bendi kongwe zilizokuwa sehemu ya uasisi wa miondoko mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika.

Jamhuri ya Watu wa Congo, DRC (Zaire ya zamani) inatajwa kama ndiyo chimbuko la bendi nyingi zilizoutangaza muziki wa aina ya rhumba na dansi la mirindimo ya kasi ya rhumba na hatimaye ‘Kavasha’ na Soukous, ambalo ndilo dansi lenyewe.

Ujio wa muziki wa dansi lililochangamka ulianzia mwanzoni mwa miaka ya 50 hadi 70 baada ya kuingia kwa teknolojia ya magitaa ya moto na ala za upepo, ambapo bendi chache zilizoanzishwa katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zililitangaza bara la Afrika hadi ndani ya mabara mengi duniani.

Ni katika miaka hiyo, bendi kubwa zilianzishwa, lakini zilizoteka nyoyo na ushabiki mkubwa nyingi ni zile za kutoka DRC, ambazo nyingi zilianzishwa mwishoni na mwaka 1950 na ndani ya miaka ya ilianzia 1960 na kuendelea.

TP OK Jazz iliyoasisiwa mwaka 1956 ilipata mafanikio makubwa na kuutalawa muziki wa rhumba la ndani na nje ya DRC hadi miaka ya 80 na ndiyo inayotajwa kama chimbuko la bendi nyingi zilizopiga muziki wa dansi la kizazi cha dansi la hivi sasa.

Lakini, jambo linaloweza kuwa ndiyo msingi wa hoja ya leo ni kwamba, pamoja na TP OK Jazz kuwa mwasisi wa bendi nyingi za kizazi cha baadae, lakini ilikosa jambo moja la msingi, nalo ni hili la kutoweka duniani kwa kifo cha kimya kimya hadi sasa.

Kutoweka kwa bendi hiyo iliyokuwa chini ya Luambo Lwanzo Makiadi, maarufu kama Franco ilizimika rasmi mwaka 1993 kulikochangiwa na kifo cha mwasisi huyo (Franco) na hadi sasa hakuna bendi inayoitwa kwa jina hilo, zaidi ya wanamuziki waliowahi kuitumikia kuendelea na muziki kivyaovyao.

Zaiko Langa langa iliyoasisiwa mwaka 1969 ndiyo bendi pekee ya kizazi cha miaka ya 60 ambayo bado ipo hai ikiendeleza muziki wa wa dansi la kizazi hiki, huku ikiwa inaendeleza mirindimo ya kisasa na ile ya kizamani.

Zaiko iliyoanzishwa ikiwa na jina la ‘Bel Guide National’ iliasisiwa na wanamuziki wengi vijana ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi wa shule za masomo ya juu ya jiji la Kinshasa, ambayo ndiyo Langa Langa ya sasa.

Ikiwa chini ya uongozi wa mwanamuziki mkongwe, Nyoka Longo, Zaiko inaingia katika rekodi ambayo wengi hawaifahamu. Nayo ni hii ya kuwa ni bendi iliyoanzishwa miaka ya 60 lakini bado ipo hai hadi leo hii.

Bendi ya muziki ya Msondo Ngoma ya sasa ya nchini Tanzania ndiyo inayoingia katika rekodi hii ya kihistoria inayofanana na Zaiko Langa Langa. Zinafanana katika matukio yanayozifanya ziwe hai, japo zimepitia katika majina tofauti!

Kwa faida ya wadau wa muziki wa dansi wa kizazi hiki wanapaswa kuitambua Msondo Ngoma kama ndiyo iliyokuwa ikiitwa NUTA Jazz, ambayo pamoja na kubadilika badilika, lakini historia inabakia kuwa ndiyo bendi kongwe zaidi nchini, ambayo hadi sasa bado ipo hai!

Ikiwa na jina la NUTA Jazz, bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1964 ikiwa chini ya Chama cha Wafanyakazi wa iliyokuwa Tanganyika ambapo, katika vipindi tofauti imekuwa ikibadilisha jina kadri chama hicho cha wafanyakazi kilivyokuwa kikibadilika!

Hadi ilipokuja kuitwa ‘Msondo Ngoma’, bendi hiyo iliwahi kuitwa JUWATA na OTTU Jazz, hadi pale mfumo wa uendeshaji ulipobadilika kwa wanamuziki wenyewe kukabidhiwa umiliki huu wa sasa.

Nimewahi kuzungumza na baadhi ya wadau wa bendi hiyo nikiwa na swali kama wanatambua historia na rekodi hii muhimu iliyopo nyuma ya pazia? Jibu limenipa faraja iliyonifanya niandike makala haya.

Shaaban Dede, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma alizungumzia suala la kuitambua historia ya rekodi hii na kusema, ni hatua inayofanya wajipongeze kwani ndiyo bendi kongwe iliyoanzishwa mwaka 1964 na kubakia kuwa hai hadi sasa.

Abdulfareed Hussein, huyu ni mmoja wa kundi la ‘Maseneta’ wa bendi hiyo ambaye alikiri kuitambua kwa kuienzi rekodi hii kwa kuasisi siku maalum katika kila mwezi inayojulikana kama ‘Msondo Ngoma Family Day’, ambayo itafanyika Septemba 30 katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kwa namna yoyote, hoja hapa ni historia iliyo nyuma ya pazia ya bendi ya Msondo Ngoma na uhai wa bendi hiyo iliyoasisiwa mwaka 1964 lakini bado ipo hai kama ilivyo kwa Zaiko Langa Langa ya DRC. Kazi kwao wana familia ya Msondo Ngoma kuienzi historia hii na kuiendeleza hadi vizazi vijavyo.

Maoni: 0782 151 409
Share on Google Plus

About Unknown

0 comments:

Post a Comment